Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akizungumza na watumishi wa Mkoa wa Rukwa (hawapo pichani)
Wakuu wa taasisi mbalimbali zinazohudumu katika mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (hayupo pichani)
Wakuu wa Idara na vitengo katika
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakimsikiliza kwa makini Wazriri Mkuu
Mstaafu Mizengo Pinda (hayupo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akitoa pongezi zake kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda
(aliyepo kushoto kwake) muda mfupi kabla ya kumkaribisha kuwasalimu
watumishi wa mkoa wa Rukwa.
…………………
Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania
Mizengo Pinda amewasisitiza watumishi mkoani Rukwa kuhakikisha kila
mmoja katika nafasi yake anafanya kazi kwa uadilifu na kueleza kuwa
utendaji kazi wa aina hiyo ndio njia pekee ya kupeleka maendeleo ya mkoa
mbele na hatimae kuutoa mkoa katika umasikini.
Amesema kuwa amesikitishwa na
taarifa iliyolewa hivi karibuni kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka
2018 ambapo mkoa wa rukwa umeonekana kushika mkia kwa kuwa na asilimia
45 ya umasikini nchini kwa mahitaji ya msingi huku mkoa wa Dar es Salaam
ukiwa na asilimia 8 ya kiwango hicho huku mkoa wa Katavi uliozaliwa
kutoka mkoa wa rukwa ukiwa na asilimia 29
Pia ameshtushwa kuwa mkoa wa Rukwa
ambao ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa
chakula nchini kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu pamoja na kuongoza
kuwa na kiwango kikubwa cha umasikini wa chakula kwa asilimia 19 wakati
Katavi ukiwa na asilimia 9.
“Tukikaa sisi kama wataalamu,
najua baadhi ya wilaya wameshapata maafisa lishe, tutawatengenezea mfumo
tuwaonganishe na majukumu ya zahanati na vituo vya afya na hospitali
zetu za wilaya, mama anapokuwa ametunga mimba lazima aambiwe aende
kliniki, lakini kliniki si kupima tu uzito nakadhalika, hapana, kubwa ni
kuona kwamba huyu mama mzazi anapata lishe stahiki?” Alihoji.
Amesema kuwa fikra zilizopo katika
makabila yaliyopo mkoa wa Rukwa na Katavi wanaamini kuwa kula mboga za
majani ni umasikini wa kutupwa kwahiyo kama mkoa una kazi kubwa ya
kubadili fikra za watu hao na kuonyesha umuhimu wa kula mboga za majani.
Ameyasema hayo katika salamu zake
kwa watumishi wa mkoa wa Rukwa hivi karibuni ambapo kikao hicho
kiliwajumuisha wakuu wa taasisi, idara, wakala za serikali pamoja na
watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa
huo Mh. Joachim Wangabo.
Wakati akimkaribisha Waziri Mkuu
Mstaafu, Mh. Joachim Wangabo alimpongeza Mh. Pinda kwa kuhakikisha
anasogeza huduma muhimu kwa wananchi kwa kuugawa mkoa wa Rukwa na
kuzaliwa Mkoa wa Katavi ambapo hivi sasa wananchi wa mkoa wa Katavi
wanafaidika na maendeleo yanayopatikana kutokana na uwepo wa huduma
muhimu za kijamii katika halmashauri tano za mkoa huo.
“ Wilaya ya Mpanda ilikuwa
inapakana na Kaliua, Uvinza na inapakana na Sikonge Mkoa wa Tabora, Sasa
fikiria huyo RC aliyekuwa anatoka Sumbawanga kwenda mpaka huko, huenda
ukakaa miaka mitano usifike maeneo mingine, ilikuwa ni shida kweli na
miundombinu yake ilikuwa ni matatizo makubwa sana kwahiyo kuugawa huu
mkoa wa Rukwa kuwa mikoa miwili umetoa unafuu mkubwa sana wa
kimaendeleo” Alisema.
Mkoa wa Rukwa ulianzishwa mwaka
1974 kwa kumega sehemu ya Mikoa ya Tabora na Mbeya. Mkoa una eneo la
kilomita za mraba 27,765, kati ya hizo Kilomita za mraba 22,844 (82.3%)
ni za nchi kavu na Kilomita za mraba 4,921 (17.7%) ni za maji. Mkoa una
jumla ya Wilaya tatu (3), zenye Halmashauri nne (4), Tarafa 16, Kata
97, Vijiji 339, Vitongoji 1,825, Mitaa 167 na Kaya 199,766. Mwaka 2010
mkoa uligawanywa na kuzaliwa mkoa wa Katavi.
No comments:
Post a Comment