Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Imeelezwa kuwa Mabadiliko Makubwa
yaliyofanywa na Serikali katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na
Marekebisho yake ya Mwaka 2017, yalilenga kuhakikisha rasilimali madini
inabaki mikononi mwa Watanzania chini ya Usimamizi wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard
Kalemani kwa niaba ya Waziri wa Madini ameieleza hayo Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Sheria Ndogo katika Semina iliyolenga kuongeza uelewa kwa
Kamati hiyo kuhusu Kanuni mbalimbali zilizoundwa zinazohusu Sekta ya
Madini na kuwasilishwa na Wataalam wa Sheria wa Wizara ya Madini
wakiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria , Edwin Igenge.
Kanuni zilizowasilishwa kwa kamati
hiyo ni pamoja na Kanuni za Madini (Udhibiti wa Eneo la Mirerani),
Kanuni zinazohusu Biashara ya Almasi, Kanuni za Masoko ya Madini pamoja
na Marekebisho ya Sheria ya Madini.
” Mhe. Mwenyekiti kuna zaidi ya
Kanuni 13 zilizoundwa amabazo zote zimelenga katika kurahisisha
usimamizi wa Sekta ya Madini na kuwanufaisha Watanzania,” amesema Dkt.
Kalemani.
Aidha, ameongeza kuwa, masuala
mengine ni pamoja na namna ambavyo watanzania wanashiriki katika umiliki
wa asilimia 16 hadi 50 kwenye uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini
na kueleza kuwa, awali suala hilo halikuwepo.
“Mhe. Mwenyekiti hii ndiyo sababu
tuko hapa pamoja na Kamati yako ambayo inahusika moja kwa moja na
masuala haya, ni masuala muhimu ambayo kamati yako inapaswa kuyajua,”
amesisitiza Dkt. Kalemani.
Ameongeza suala ni usimamizi wa
sekta ya Madini kuwekwa chini ya Tume ya Madini pamoja na Serikali
kupitia Benki Kuu ya Tanzania kuwa na akiba ya madini ya Dhahabu na
kusema, “Mhe. Mwenyekiti suala hili lilikuwepo awali lakini sasa
tumelirejesha tena”.
Aidha, Waziri Kalemani amesema
mabadiliko hayo yaliyofanywa katika sekta ya madini yamepelekea
kupunguza nguvu ya wachimbaji wakubwa na kutoa nafasi kwa watanzania
wengi kunufaika na rasilimali madini ikiwemo kuweka biashara ya madini
wazi na uanzishwaji wa masoko ya madini ambayo yameleta manufaa kwa
sekta.
katika hatua nyingine, Waziri
Kalemani amesema kufuatia serikali kuweka mazingira mazuri hususani kwa
wachimbaji wadogo wa madini, serikali kupitia Wizara ya Nishati
imewezesha kufikisha nishati ya umeme kwenye migodi 32 ya wachimbaji
wadogo wa madini suala ambalo linawawezesha kuchimba kwa faida na
kuachana na matumizi ya mafuta.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo William Ngeleja, akizungumza katika
semina hiyo ameipongeza Serikali hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli kwa Maamuzi makubwa aliyoyafanya katika
Sekta ya Madini ambayo yalipelekea kufanyika kwa Mabadiliko ya Sheria ya
Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na kueleza kuwa,
manufaa yake yanaonekana.
Pia, ameipongeza Serikali kwa
uazishwaji wa Masoko ya Madini pamoja na Ujenzi wa Ukuta unaozunguka
Migodi ya Tanzanite Mirerani na kueleza kuwa, ukuta huo umeongeza tija
kwa taifa kutokana na mapato yanayopatikana baada ya udhibiti wa
utoroshaji wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee ikiwemo
usimamizi wa rasilimali hiyo.
” Mhe. Mwenyekiti kuna zaidi ya
kanuni 13 zilizoundwa amabazo zote zimelenga ktika urahisisha usimamizi
wa Sekta ya Madini na kuwanufaisha Watanzania, “
Vilevile, amesema semina hiyo
imewaongezea weledi wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mabadiliko ya Sheria
ya madini. Aidha, amempongeza Waziri Biteko kutokana na ushirikiano na
usimamizi mzuri wa rasilimali madini unaofanywa na kusema “Watendaji
tembeeni vifua mbele mnaye kiongozi anayewawakilisha vizuri,” amesema
Ngeleja.
Pia, amechukua fursa hiyo
kuipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi mzuri wa sekta ya Nishati na
kusema kwamba,”Wewe Waziri Kalemani na mwenzio wa Madini mnamwakilisha
vizuri Rais wetu sisi sote tunaona”.
Aidha, kamati hiyo imeishauri
Wizara kuhusu masuala kadhaa yanayohusu sekta ya madini yakilenga
katika kusimamia na kuboresha sekta husika ili kuhakikisha kwamba
rasilimali madini inawanufaisha zaidi watanzania, ambapo Waziri Kalemani
ameahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa na kamat hiyo. Pia, kamati
imeitaka wizara kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo madini
kuhusu masuala yanayohusu kodi pamoja na mambo mengine ya muhimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akijibu hoja zilizowasilishwa na
Kamati hiyo, ameeleza kwamba, zipo tofauti za kabla na baada ya
kujengwa kwa Ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani na kueleza
kwamba, mapato yameongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.
“Lakini Mhe. Mwenyekiti sisi na
wizara tunafanya kazi kama Timu, tunaendelea na majukumu yetu ya
usimamizi wa sekta ya madini lakini pia tayari serikali imetoa magari 36
, tumeongeza watumishi wapya 180 bado tunaendelea na kufanyia kazi
lengo la kukusanya shilingi bilioni 470 kwa Mwaka wa Fedha 2019/20,”
amesema Prof Kikula.
Kuhusu udanganyifu unaofanywa na
baadhi ya vituo vya uchenjuaji dhahabu, amesema Tume ya madini
ilikwisha baini udanganyifu huo na suala hilo linadhibitiwa.
Wataalam wengine waliowasilisha
Mada katika semina hiyo kutoka wizara ya madini ni pamoja na Maafisa
Sheria Waandamizi Semeni Kakunda, Julieth Moshi pamoja na Afisa Sheria
Godfrey Nyamsenda.
Wengine waliohudhuria semina hiyo ni Wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
0 comments:
Post a Comment