*************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Justice Kijazi kwa kuamua kuchapa kazi
na kuweka mbele maslahi ya wananchi.
“Moja ya
Hamashauri zilizotulia ni Ikungi. Hii ni Halmashauri pekee ambayo Mkuu
wa Wilaya ya Mkurugenzi wake wanaongea lugha moja. Endelezeni kazi hii
nzuri ili viongozi wengine waje kujifunza kwenu,” alisema na kuamsha
shangwe miongoni mwa watumishi waliohudhuria mkutano wa hadhara.
Alitoa
pongezi hizo jana jioni (Ijumaa, Oktoba 4, 2019), wakati akizungumza na
wananchi na watumishi wa Halmashauri hiyo kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika wilayani Ikungi.
Aliwataka
watumishi wa Halmashauri hiyo watambue kwamba wako chini ya wananchi na
kwamba bila ya uwepo wao, hata wao wasingepata kazi wilayani humo. “Mimi
na ninyi sote ni watumishi wa hawa wananchi. Bila wao, tusingekuwa na
utumishi hapa. Lazima mtambue kwamba mmeletwa hapa ili muwahudumie wao,”
alisisitiza.
“Nendeni
vijijini, wahudumieni bila kujali umri wao, dini, rangi au itikadi zao.
Wakiuliza masuala ya kilimo au maji au afya, washughulikieni na muwape
majibu huko huko. Wananchi wengine wanaishi vijiji vya mbali na hapa,
wengine hawana nauli, wengine hawajui hata wakija mjini waanzie wapi,”
alisisitiza.
“Nimekuwa
nikisisitiza kwamba wakuu wa idara wasikae ofisini kwa wiki nzima.
Nendeni vijijini mkawasikilize wananchi. Wakuu wa idara tofauti,
jipangeni mtumie gari moja; siku nne kati ya tano za wiki, nendeni
vijijini mkasikilize wananchi na siku mbili zilizobakia mje muandike
taarifa zenu ofisini,” alisema.
“Mkuu wa
Wilaya na Mkurugenzi simamieni hili, kwa sababu ni mojawapo ya matakwa
ya Serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa
ipasavyo.
Mapema, akitoa
salamu, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Edward Mpogolo alimweleza Waziri Mkuu
kwamba uuzaji wa pamba katika wilaya hiyo unaendelea na hadi sasa
wameshauza tani milioni 1.4 kati ya tani milioni 2.5 walizojiwekea
malengo.
“Pamba
imeendelea kununuliwa kwa bei ya sh. 1,200 kama ilivyoelekezwa na hadi
sasa tani milioni 1.4 zenye thamani ya sh. bilioni 1.7 zimenunuliwa
viwandani. Tunaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuwawezesha
wananchi hawa kupata fedha hiyo,” alisema.
Alisema
anaishukru Serikali kwa kuboresha huduma za afya, mikopo kwa wanawake na
vijana, umeme na elimu ambapo ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 64
hadi asilimia 83.
0 comments:
Post a Comment