*******************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya za Itigi na Ikungi na
Wakurugenzi wao wafanye misako kwenye stendi za mabasi ili kuwabaini
watoto wasiokwenda shule.
Ametoa agizo
hilo kwa nyakati tofauti jana (Ijumaa, Oktoba 4, 2019) wakati akihutubia
mamia ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye mikutano ya hadhara
aliyoifanya kwenye wilaya hizo.
Alisema
Serikali ya awamu ya tano imeondoa michango kwenye sekta ya elimu na kwa
maana hiyo watoto wenye umri wa kwenda shule wanapaswa wawe shuleni.
“Michango ya
hovyohovyo haipo. Vinginevyo, fedha ambazo wazazi mmeokoa, peleka kwa
mtoto. Mnunulie sare, kiatu kizuri, begi la shule na madaftari. Ale
vizuri asubuhi na aende shule,” alisisitiza Waziri Mkuu.
“Hatutarajii
kuona vijana wadogo wanauza biashara kwenye vituo vya mabasi. Mkurugenzi
chukua OCD siku moja, nenda kwenye miji yenu midogo, saka watoto wote
wanaofanya biashara stendi.”
“Watambue
wazazi wao, halafu kamata wazazi hao wajieleze ni kwa nini wanawaacha
watoto wao waende kuhangaika stendi badala ya kwenda shule. Tunataka
kila mtoto wa Kitanzania aende shule,” alisisitiza.
Alisema
Serikali imetoa maelekezo kwamba kila kijiji kinapaswa kiwe na shule ya
msingi na kila shule lazima iwe na darasa la awali ili watoto wenye umri
wa miaka minne hadi mitano waanze shule mara moja.
0 comments:
Post a Comment