WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa
siku tatu Kaimu Mweka Hazina wa wilaya ya Itigi, Bw. Optatus Likiliwike
ahakikishe anarejesha sh. milioni 1.6 ambazo alijilipa posho kinyume
cha utaratibu.
“Kabla sijamaliza ziara tarehe 7, nataka nione pay in slip kuthibitisha kuwa fedha hiyo imerudishwa. Adhabu yako kaweke fedha benki, niione hiyo pay in slip kabla sijaondoka,” amesema Waziri Mkuu.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa,
Oktoba 4, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Manyoni
ambao wanajumuisha Halmashauri za Wilaya za Itigi na Manyoni.
“Wewe si ndiye Otto au
Optatus? Mwezi Julai ulilipwa posho ya safari ili uende Dodoma
kukamilisha mahesabu ya bajeti lakini hukwenda. Taratibu za fedha
zinasema ukitumia fedha, urejeshe, wewe ulifanyaje?,” alihoji Waziri
Mkuu.
“Nilichukua fedha lakini
kutokana na majukumu mengi niliyo nayo, sikwenda nikawa naenda
wikiendi na kuna kazi nyingine haikuwa ni lazima niwepo Dodoma,” alijibu
Bw. Likiliwike.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amemtaka afisa huyo arejeshe sh. milioni 196 za ujenzi wa ofisi ya
Halmashauri ambazo zimetumika kinyume na zilivyopangwa.
“Hizi fedha zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi. Hizi ni fedha za retention,
ni nani alikiuka maelekezo na kuamua kuzitumia kwa kazi nyingine?”
Waziri Mkuu alijibiwa kwamba ni Mkurugenzi na Mweka hazina waliokuwepo
kabla yake.
Waziri Mkuu amemwagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Bw. John Mgalula ambaye aliteuliwa
wiki iliyopita asimamie marejesho ya posho za Bw. Likiliwike pamoja na
marejesho ya sh. milioni 196 ambazo mweka hazina huyo ameahidi kuwa
Halmashauri yake imetenga sh. milioni 70 ili zirejeshwe kila mwaka.
Waziri Mkuu amesema wanapaswa
kutenga fedha zaidi ili fedha hiyo iweze kurejeshwa haraka kwa Wakala wa
Majengo nchini (TBA) ambaye ni mkandarasi wa jengo la ofisi za
Halmashauri hiyo.
Naye Bw. Optatus Otto Likiliwike
alisema kwamba fedha zinazodaiwa kutumika zilikuwa zimetumwa na HAZINA
kwa ajili ya ujenzi wa ofisi lakini zililazimika kuchotwa na uongozi
uliopita ili zitumike kuweka miundombinu ya kuanzisha Halmashauri mpya
ya Itigi.
Alisema waliohusika ukiukwaji
huo ni Mkurugenzi aliyepita, Bw. Pius Luhende na Mweka Hazina aliyepita
Bw. Charles Mnamba. Hata hivyo, alikiri kwamba fedha hizo hazikuombewa
kibali cha matumizi hayo.
Akiweka jiwe la msingi kwenye
jengo hilo, Waziri Mkuu alisema anaweka jiwe hilo kwa sababu
ameridhishwa na maelezo ya Meneja wa TBA kuhusu ujenzi wa jengo hilo.
Amewataka madiwani wa
Halmashauri hiyo wahoji matumizi ya fedha hizo na wawaorodheshe wote
waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo. “Kaeni na mkaguzi wenu wa
ndani, awape taarifa juu ya matumizi hayo,” alisema.
Pia amewataka watumishi wa
umma waheshimiane na watambue Mamlaka nyingine kama za madiwani. Pia
aliwataka wafuate taratibu na kanuni za utumishi na siyo wajifanyie
mambo kwa holela.
Awali, Waziri Mkuu alimwagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Bw. Charles Fussi
ahakikishe anarejesha mkopo wa sh. milioni 100 kutoka benki ya CRDB
ambazo walikopeshwa madiwani, wakarejesha kiasi lakini Halmashuri
haijazipeleka benki.
Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa deni hilo kutokana na malimbikizo ya muda mrefu na riba zinazotozwa na benki.
“Hakikisha unamaliza hilo deni
la sivyo hawa Waheshimiwa hawatapata stahili zao hadi deni liishe. Pia
unataka kusababisha mgogoro baina ya benki na Halmashauri.”
Aliwataka wadiwani hao
waisimamie kwa karibu Halmashauri yao. “Madiwani muiangalie Halmashauri
yenu kwa kina. Hatuwezi kuendesha Halmashauri kwa utaratibu huu wa kila
mmoja kufanya kazi anavyotaka.”
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Itigi.
0 comments:
Post a Comment