Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Jijini Dar es salaam katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo tarehe 3 Octoba 2019 kwa ajili ya kutangaza bei elekezi ya mbolea ya kukuzia (UREA) kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Jijini Dar es salaam katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo tarehe 3 Octoba 2019 kwa ajili ya kutangaza bei elekezi ya mbolea ya kukuzia (UREA) kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Katika kuhakikisha kuwa tija ya
uzalishaji wa mazao ya kilimo inaongezeka ili kujitosheleza kwa chakula na malighafi
za viwandani; serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya mbolea ili kufikia
kilo 50 za virutubisho kwa hekta moja kama ilivyopendekezwa na wakuu wa nchi za
Afrika kupitia Azimio la Abuja la mwaka 2006. Ili kufikia lengo hilo Wizara ya
Kilimo ilianzisha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS - Bulk Procurement System), kufuta tozo mbalimbali za mbolea, kusimamia
utaratibu wa usafirishaji wa mbolea na kuweka bei elekezi za mbolea kwa
mkulima.
Uingizaji wa mbolea kupitia BPS
unahusu mbolea za Urea, DAP, NPK, CAN na SA. Hata hivyo, kwa sasa BPS inatumika
kuingiza mbolea za DAP na Urea ambazo zinazotumika kwa zaidi ya asilimia 50.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
ameyasema hayo leo tarehe 3 Octoba 2019 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza
kwenye mkutano wa waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo.
Alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu
cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Na. 9 ya mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya
Kanuni za Mbolea, 2011 na marekebisho yake ya mwaka 2017 (The Fertilizer (Amendment) Regulations, 2017), mbolea aina zote
zinatakiwa kuuzwa kwa bei iliyopangwa na Serikali. Hata hivyo, bei elekezi zinazotangazwa
ni kwa mbolea zinazoagizwa kupitia BPS ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na ya
kukuzia (Urea).
1.
Zabuni za Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS)
Waziri Hasunga amesema kuwa Mfumo wa
Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) umeanzishwa kwa lengo la kupata punguzo la
bei litokanalo na kununua na kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja (Economies of scale). Tangu kuanza kwa
BPS mwaka 2017, huu ni msimu wa tatu wa kilimo wa utekelezaji wake ambapo
mbolea zimeingizwa nchini kwa punguzo la bei katika chanzo (FOB – Free on Board) kwa asilimia 6 – 17
ikilinganishwa na bei katika soko la Dunia inayosimamiwa na taasisi
inayofuatilia bei ya mbolea katika soko la Dunia iitwayo Argus Gmbh. Aidha, BPS imefanya gharama za usafirishaji wa mbolea
baharini kushuka kwa kiasi kikubwa kutoka Tshs 23,000/= hadi Tshs 3,500/= kwa
mfuko mmoja wa kilo 50. Kutokana na BPS, matumizi ya mbolea yamekuwa
yakiongezeka kila mwaka.
2.
Mjengeko wa bei elekezi
Ikumbukwe kuwa, zaidi ya asilimia 90
ya mbolea zinazotumika nchini kwa sasa huagizwa kutoka nje ya nchi. Hivyo, katika kutengeneza mjengeko wa
bei, gharama mbalimbali huzingatiwa hususan bei ya ununuzi katika chanzo,
usafirishaji wa mbolea baharini, bima, tozo za Mamlaka ya Bandari (TPA) na taasisi
mbalimbali za udhibiti, gharama za vifungashio, kufungasha, usafirishaji hadi
kwa muuzaji wa rejareja na faida ya mfanyabiashara.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa bei
elekezi za mbolea hutegemea umbali wa sehemu inakopelekwa kutokea bandarini. Maeneo
yote itakapopelekwa mbolea yana umbali kati ya kilometa 1 na 1,600 kutoka
bandari ya Dar es salaam. Kwa Wastani, gharama ya kusafirisha mfuko mmoja wa
mbolea wa Kilo 50 kwa barabara kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi makao makuu
ya Halmashauri kwa barabara ni Sh. 5,500/= kwa kilometa 1,000. Gharama hii
hupanda na kushuka kutegemeana na hali ya barabara na hali ya hewa (masika au
kiangazi). Aidha, usafiri kwa njia ya
Reli ni nafuu zaidi kwa sababu gharama za kusafirisha mbolea kwa kilometa 1,000
kwa mfuko wa kilo 50 ni Tshs
4,160 (TRC) au Tshs 4,600 (TAZARA).
3.
Mwenendo na mchanganuo wa bei elekezi za mbolea ya kukuzia
(Urea)
4.1.Mwenendo wa bei elekezi katika soko la ndani ya nchi
Ushindani wa zabuni za BPS
zilizofunguliwa Julai 04, 2019 ulifanya bei za mbolea aina ya Urea kununuliwa
kwenye chanzo kwa punguzo la dola saba (7) za kimarekani ikililinganishwa na
bei za zabuni ya Julai, 2018.
Sambamba na punguzo lililotokana na
zabuni hizo, Wizara ya kilimo ilifanya utafiti kati ya Juni na Julai, 2019 wenye
lengo la kufanya marejeo ya kikokotoo cha bei elekezi ambacho kimetumika kwa
misimu ya kilimo 2017/2018 na 2018/2019. Utafiti huo ulishirikisha wadau wa
mbolea wakiwemo wauzaji (waingizaji, wasambazaji, wauzaji wa jumla na
rejareja), wanunuzi (wakulima wadogo kupitia vyama vyao vya ushirika, wakulima
wakubwa, viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na wanunuzi wa mazao).
Ushindani wa zabuni za
BPS pamoja pamoja na utafiti wa kupitia upya kikokotoo umefanya bei ya mkulima kupungua kwa wastani kimkoa kutoka
Tshs 57,482 hadi wastani wa Tshs 53,997/=. Hili ni punguzo la wastani wa Tshs 3,485/=
au asilimia 6 kwa mfuko wenye uzito wa kilo 50.
0 comments:
Post a Comment