Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile
(katikati) baada ya Waziri Mkuu kufungua Mkutano wa Wadau wa Lishe
kwenye ukumbi wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma, Oktoba 3, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa
katika picha ya pamoja na viongozi na Wadau wa Lishe baada ya kufungua
Mkutano wa Wadau wa Lishe kwenye Ukumbi wa Kambararage, Hazina jijini
Dodoma, Oktoba 3, 2019. Kushoto kwake ni Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo
Pinda na kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Wadau wa Lishe kwenye ukumbi
wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma, Oktoba 3, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda wakati alipowasili
kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma kufungua Mkutano wa Wadau wa
Lishe, Oktoba 3, 2019. Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema utapiamlo ni miongoni mwa vikwazo vya kutimiza dhamira ya
Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda ambao utawezesha
Taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Amesema bila ya kuwa na lishe
bora na afya njema, vinavyosaidia kuongeza uwezo wa kuelewa na ubunifu
ili kuhimili ushindani wa kiuchumi nchi haitafika kwa wakati kwenye
uchumi wa kati na wa viwanda uliokusudiwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Alhamisi, Oktoba 3, 2019) wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wadau
wa Lishe uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. Amesema ni
muhimu elimu ya lishe ikatolewa kwa wananchi wote.
“Pamoja na tafiti kuonesha
kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu wa damu bado viwango
vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna viwango vya utapiamlo
ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki kimataifa ikiwemo uzito
uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa.”
Amesema hali hiyo ni hatari
kwa nchi ambayo inayokabiliwa na aina nyingine za utapiamlo
unaosababishwa na lishe duni kama udumavu, utapiamlo mkali na wa kadiri
ambapo athari zake ni kubwa katika ukuaji wa watoto wenye umri wa chini
ya miaka mitano. “Hii ni ishara tosha kwamba tunatakiwa kuongeza juhudi
katika kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia viwango
vinavyokubalika Kimataifa.”
Amesema Serikali kwa
kushirikiana na wadau itaendelea kutoa kipaumbele kwa maeneo ambayo
yameathirika zaidi na ambayo yanatekeleza miradi inayolenga kupunguza
udumavu kwa watoto, matatizo ya upungufu wa vitamin na madini.
Kipaumbele kitatolewa katika
kuimarisha matibabu ya utapiamlo mkali na wa kadiri, kupunguza tatizo la
uzito uliokithiri na viriba tumbo na tatizo la upungufu wa damu kwa
wanawake na watoto ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaleta matokeo
chanya katika maeneo hayo.
Amesema kuwa mipango yoyote
wanayojiwekea haiwezi kuleta matokeo chanya bila kuitengenezea mikakati
thabiti ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kutenga rasilimali za kutosha,
ambapo wataalamu hao waibue mikakati itakayoweza kutumika katika
kupunguza tatizo la utapiamlo.
Pia, Waziri Mkuu amewataka
waajiri wote waandae fursa na kuwaalika mahala pa kazi maafisa lishe ili
kuongeza ufahamu wa watumishi kuhusu lishe bora. Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zimetakiwa ziweke
mipango ya kuhakikisha maafisa lishe wanaalikwa kutoa elimu sambamba na
ufundishaji shuleni.
Kwa upande wake,Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu
Jenista Mhagama amesema bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na afya
bora Taifa haliwezi kufanikiwa kwenye masuala ya elimu, kilimo, viwanda
hivyo kukwamisha jitihada za Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi
wa viwanda.
“Kwa hali iliyopo sasa ni wazi
kuwa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuondokana na utapiamlo nchini.
Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea
katika Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe (2016/17 – 2020/21), ambayo ni
pamoja na kupunguza udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano
kufikia asilimia 28 na uzito uliozidi kufikia asilimia 30.”
Amesema Serikali inatambua kuwa
lishe ni suala mtambuka linalotegemea jitihada za sekta mbalimbali,
ambapo waliandaa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa miaka mitano kuanzia
mwaka 2015/16 hadi 2020/21 ili kutoa muongozo katika utekelezaji wa afua
mbalimbali za masuala ya lishe.
Naye, Waziri Mkuu Mstaafu
Mizengo Pinda amesema katika jitihada za kupambana na umasikini ni vema
elimu ya lishe bora ikatolewa kwa wananchi wote, ambapo amemshauri
Waziri Mkuu aibebe agenda ya lishe, ambapo Waziri Mkuu amekubali.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu
ameongeza kuwa, mila potofu nazo zimechangia suala la utapiamlo nchini
kwa sababu katika familia nyingi nchini vyakula vingi vizuri wanapewa
wanaume na vyakula vibovu wanakula wanawake na Watoto.
Awali, Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile
amesema udumavu umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 na kufikia
asilimia 31.5 mwaka huu.
Dkt. Ndungulile alisema licha
kupungua kwa udumavu, changamoto iliyopo kwa sasa ni suala la
unyonyeshaji kwa watoto walio na umri wa chini ya miezi sita,
wanaonyenyeshwa ni asilimia 58 tu, huku asilimia 30 ya Watoto wenye umri
wa zaidi ya miezi sita hawalishwi vizuri.”Theruthi moja ya wanawake
nchini wana viribatumbo na utapiamlo wa lishe iliyopitiliza.
0 comments:
Post a Comment