![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/kassim.jpg)
*************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kupunguza uagizaji wa baadhi
ya bidhaa zinazozalishwa nje na kuongeza ununuzi wa bidhaa
zinazozalishwa ndani ili kukuza viwanda vya ndani mfano ni bidhaa za
mbao na mafuta ya kula.
“Napenda
kuwahakikishia kuwa, bidhaa zetu ni nzuri na zinapendwa na watu wengi
hata wa nje ya nchi. Mnachotakiwa kukifanya ni kuzalisha bidhaa kwa
wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye maeneo yenu, hii
itawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei
shindani katika soko.”
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 7, 2019) wakati akifungua Maonesho
ya Sido Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya BomberdiaManispaa ya
Singida. Amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwa na
viwanda vya kuongeza thamani ya madini nchini.
“Niwasihi
Watanzania wote hasa wale wanaofikiria kuwa bidhaa zinazotoka nje ya
nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kuachana na dhana hiyo
potofu, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili.”
Amesema
wakizalisha bidhaa kwa kutumia malighafi za ndaniitawezesha ajira
endelevu kuwepo kwa vijana, itasaidia malighafi kutoharibika lakini pia
bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa na thamani kubwa badala ya kuuza
malighafi kwa bei ya chini.
Pia, Waziri
Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuifikisha nchi
kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Amesema
uanzishwaji wa viwanda umejikita zaidi katika uongezaji wa thamani wa
mazao ya kilimo na maliasili yanayopatikana nchini, kama, kilimo,
mifugo, misitu, uvuvi na madini kwani wananchi wengi wanategemea mazao
na rasilimali hizo kwa maisha yao.
Waziri Mkuu
amesema Serikali itaendelea kuhimiza uongezaji thamani wa mazao husika
kwa kuwa ndiyo njia sahihi. “Kwa misingi hiyo, usindikaji, uchakataji
na uchenjuaji, vitachangia kupunguza upotevu unaotokea msimu wa mavuno,
kuongeza ajira na thamani ya mazao kwa lengo la kuwapatia wazalishaji
kipato.”
Amesema
uongezaji thamani utahitaji teknolojia (mashine na ujuzi), ambapo baadhi
ya teknolojia hizo zimeoneshwa kwenye maonesho hayo. “Vilevile,
maonesho hayo yametoa fursa ya kuonesha teknolojia zinazoweza
kurahisisha uzalishaji na kuleta ufanisi zaidi ili kuongeza tija na
kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.”
Mapema,
akitoa taarifa kuhusu maonesho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
wa SIDO, Prof. Elifas Bisanda alisema wamekuwa wakiandaa maonesho hayo
ili kuwahamasisha wajasiriamali wadogo na wa kati wapate mbinu mpya juu
ya viwanda vidogo.
“Pia tumekuwa
tukifanya maonesho haya ili kuwapa wananchi uelewa kuhusu bidhaa
zinazozalishwa nchini. Tangu mwaka 2006, yalikuwa yakifanyika kikanda,
lakini kwa sasa yanafanyika kitaifa,” alisema.
Alisema
kupitia maonesho hayo, wajasiriamali hupata mafunzo ya ufungashaji wa
bidhaa lakini pia hupata fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwao na
kupata taarifa kutoka kwenye taasisi zinazojihusisha na viwanda vidogo
na vya kati.
Alisema
anaiomba Serikali iwapatie fedha zaidi ili waweze kuwafikia wananchi
wengi zaidi hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imepeleka umeme hadi
vijijini lakini wananchi wengi hawanufaiki na uwepo wa umeme huo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alisema hii ni mara ya pili maonesho hayo yanafanyika mkoani humo.
0 comments:
Post a Comment