![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PMO_0305-1024x597.jpg)
*Asema ikithibitika ni kweli, lazima warudishe fedha hizo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili Elinipenda
achunguze watumishi 48 waliojihusisha na upotevu wa fedha kwa njia za
udanganyifu.
Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akizungumza na madiwani na watumishi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwenye mkutano uliofanyika kwenye
ukumbi wa Halmshauri hiyo.
Waziri Mkuu ametoa maeneo saba
ambayo ametaka yafanyiwe uchunguzi wa kina ili kubaini upotevu huo. Eneo
la kwanza ni upotevu wa makusanyo ya ndani kupitia mawakala wa
ukusanyaji mapato (POS) ambapo mawakala wanaokusanya fedha
wanashirikiana na watumishi wa Halmashauri na kuzitumia bila kuziingiza
benki.
Kuna kundi la watumishi 10
wakiongozwa na mtu wa TEHAMA, wameshirikiana kupata password na fedha
zikishakusanywa wanazitoa na kuzitumia bila kuzipelekea benki. Wamesahau
kwamba malipo yalipoingizwa mara ya kwanza, data ilirekodiwa kwenye
mfumo wa malipo na sisi tunaona ni kiasi gani kimekusanywa.”
Watumishi hao ni Salum Omari
(Mtaalamu wa TEHAMA); Adam Mzengi (Mhasibu kahamishiwa Gairo); Rafaeli
Nasari; Caroline Makundi (kahamishiwa Singida Manispaa), Edson S. Ally
(Afisa Biashara); Martin Kimisho (Mhasibu Msaidizi); Prosper Banzi
(Afisa Biashara); Hassan Ponda (Mhasibu kituo cha afya Ndago); Hafidh
Ngayunda (Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya) na Muhidin Mohammed (Mweka
Hazina wa Wilaya) ambaye tayari amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma
hizo.
Kutokana na upotevu huo, Waziri
Mkuu ameagiza Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya akae pembeni hadi uchunguzi
wa TAKUKURU utakapokamilika.
Akibainisha mchezo mwingine
uliochezwa na watumishi wa Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu amesema kuna
watumishi 38 ambao walilipwa kiasi cha sh milioni 46 ambazo zilikuwa
sehemu ya sh. milioni 400 za kujenga vituo vya afya vya Ndago na
Kinampanda wilayani humo.
“Hapa nina vocha zote za malipo
walipeana fedha watu hawa akiwemo Mkurugenzi wao. Lakini ni kazi gani
ambayo kundi lote hili lilikuwa likiisimamia na kustahili kupata malipo
hayo? Kutoka makao makuu ya wilaya hadi Ndago au Kinampanda kuna umbali
gani?” alihoji Waziri Mkuu.
“Kamanda wa TAKUKURU fanya
uchunguzi, fuatilia wote waliohusika sababu majina tunayo, kama
hawastahili kulipwa ni lazima warudishe fedha yetu. Hii ni sehemu ya sh.
milioni 90 ambazo hazijulikani ziliko na zilikuja kujenga kituo cha
afya. Fedha hizi zimekuja na maelekezo rasmi, ni kwa nini zilibadilishwa
matumizi,” alihoji.
Waziri Mkuu alisema kuna fedha ya
walimu sh. milioni 29 ambayo ilitumwa na TAMISEMI ili kulipa likizo zao
lakini Mkurugenzi alitumia kulipia usafirishaji wa makontena ya vifaa
vya tiba kutoka Sweden hadi Singida wakati mkataba wa malipo unasema
Halmashauri ilipaswa kulipia kutoka bandari ya Tanga hadi Singida.
“Hii fedha ya walimu ya likizo
nataka irudishwe mara moja. Pia kuna shilingi milioni 6.86 ambazo mmedai
ni malipo ya kukomboa mizigo bandarini wakati vifaa hivyo vilipata
msamaha wa kodi. Tena kuna sh. milioni 34 ambazo zililetwa kurekebisha
Ikama za walimu lakini hadi leo hazijalipwa. “Kamanda wa TAKUKURU nataka
uniambie nafasi ya Afisa Elimu ikoje kwenye suala hili,” alisema.
Pia alisema kuna fedha kujenga
machinjio ya kisasa ambayo ililetwa lakini machinjio hayajakamilika hadi
sasa. “Tumeleta sh. milioni 100 za machinjio lakini Afisa Mifugo
anasema wametumi sh. milioni 20 tu, nataka sh. milioni 80 zimeenda
wapi.”
Waziri Mkuu alisema kuna sh.
18,090,000 za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kutoka vituo vya afya 13
ambazo zimetumika kusafirisha hayo makontena nayo pia irudishwe. “Hivi
mnachangisha watu sh. 30,000 kwa ajili ya kupata dawa wakienda kutibiwa
lakini leo hawana dawa kwa sababu mmezitumia ndivyo sivyo na wao hawana
dawa kwenye vituo hivyo kwa sababu hamjazirejesha.”
“Kamanda wa TAKUKURU fanya
uchunguzi kwenye fedha ya mikopo ya akinamama, vijana na wenye ulemavu
ambayo ni asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri. Fedha hii haijatoka
tangu mwaka 2017/2018 na 2018/2019.
0 comments:
Post a Comment