![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PMO_0372-1024x716.jpg)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na mtaalam wa maabara, Bahati Ipunda, wakati akikagua kituo
cha afya cha Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Oktoba 6.2019.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PMO_0305-1024x597.jpg)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na wananchi, baada ya kukagua kituo cha afya cha Wilaya ya
Ikungi, mkoani Singida, Oktoba 6.2019.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PMO_0350-1024x663.jpg)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akikagua kituo cha afya cha Ndago, kilichopo katika Wilaya ya Iramba,
mkoani Singida, Oktoba 6.2019.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PMO_0362-1024x662.jpg)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa
ameshika kipande cha tofali, kilichobomoka, wakati akikagua kituo cha
afya cha Ndago, wilayani Iramba, katika Mkoa wa Singida, na
kutoridhishwa na ujenzi wa kituo hicho, Oktoba 6.2019.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hajaridhishwa na ujenzi wa kituo cha afya cha Ndago, wilayani
Iramba mkoani Singida kwa sababu uko chini ya kiwango.
Ametoa kauli hiyo leo
(Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akizungumza na wananchi wa kata ya
Ndago mara baada ya kukagua majengo ya kituo hicho.
“Nimepita kote nchini kukagua
vituo hivi lakini hapa wamenikasirisha. Wamenileta kwenye jengo
nilikaguem nikajua ni jipya kumbe ni la zamani. Lazima nikiri kwamba
fedha yetu hapa haijakamilika, jengo la mama na mtoto halijakamilika.
Nilipouliza linakamilika lini, wananijibu tuko kwenye final touches (tuko hatua za mwisho),” amesema.
“Jengo lile halivutii kabisa,
wanaotoa maelezo hakuna kinachoeleweka. Sijaridhishwa kabisa na hali
hii. Jengo la upasuaji nalo pia nimeona ni la zamani. Hii ina maana
hamjajenga jengo jipya. Mimi nataka nione jengo jipya hapa,”
amesisitiza.
Alipomuuliza Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo Bw, Leno Mwageni amebakiza kiasi gani cha fedha katika
sh. milioni 400 ambazo zililetwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo,
Mkurugenzi huyo alijibu kwamba hakuna kiasi cha fedha kilichobakia.
Waziri Mkuu aliwaeleza
wananchi hao kwamba Mheshimiwa Rais John Magufuli anatambua wao hawana
uwezo, na tena wanaugua na kuna watu ambao wanapoteza maisha kwa sababu
hawawezi kufika kwenye tiba kwa wakati.
“Vituo vya afya vinajengwa
kila mahali nchini ili wewe mwananchi usilipe nauli kwenda Iramba mjini
au Singida mjini kutafuta tiba, bali upate vipimo vyote hapa hapa ulipo.
Vipimo vya magonjwa yote vinapatikana hapa hapa.”
“Fedha hizi zikiletwa zinataka
pajengwe maabara, chumba cha upasuaji mdogo na mkubwa, chumba cha
huduma ya mama na mtoto, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya mkuu
wa kituo, lakini hapa Ndago fedha yetu imeharibika,” amesema.
Alipoenda kukagua chumba cha
kuhifadhia maiti, Waziri Mkuu alikuta limewekwa mlango wa mbele tu na
vyumba vingine vyote havina milango wala mabomba na masinki
hayajakamilika tofauti na taarifa aliyopewa kwamba jengo hilo liko
tayari.
“Mkurugenzi nimekuta wagonjwa
wamelazwa katika baadhi ya vyumba na kazi haijakamilika. Huwezi kupanga
vifaa wakati ujenzi unaoendelea ili kumdanganya Waziri Mkuu. Na wala
hunidanganyi mimi bali unawadanganya wananchi.”
“Ninazo taarifa kwamba jana
mlikesha kupanga vitu ndani. Nenda kaondoe vifaa vyote hadi ujenzi
utakapokamilika ndipo madaktari warudi kuendelea na kazi. Serikali hii
haiwezi kuvumilia vitu vya hovyo. Hatua kali zitachukuliwa,”
alisisitiza.
Mapema, Mbunge wa jimbo hilo,
Bw. Mwigulu Nchemba alimweleza Waziri Mkuu kwamba alichangia mifuko 400
ya saruji na wananchi wa kata hiyo walichangia mawe na ujenzi wa msingi.
Alitumia fursa hiyo kumshukuru
Rais Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa vituo vya afya.
“Tunashukuru kwa sababu fedha hizi zimekuja kamili, na siyo kwa mafungu.
Wananchi wamechangia nguvu zao na mimi mwenyewe nilitoa mifuko 400 ya
saruji,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kumuomba
Waziri Mkuu awasaidie wananchi wa kata ya Ndago wapate barabara ya lami
ya kutoka Singida-Sepuka-Ndago-Kizaga yenye urefu wa kilometa 76. “Hii
ni tarafa kubwa kuliko zote na huku ndiko uzalishaji mkubwa uliko. Hii
barabara imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, kilio na furaha ya wana-Ndago
ni barabara hii kuwekwa lami,” alisema.
0 comments:
Post a Comment