METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 1, 2019

NAIBU WAZIRI MABULA ATAKA MAJINA YA WATUMISHI WA ARDHI WALIOKACHA KWENDA MAFIA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Mafia mkoani Pwani Shaib Nnunduma baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mafia jana kuanza ziara ya siku mbili wilayani humo. Katikati ni Mbunge wa jimbo la Mafia Mbaraka Dau.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na uongozi wa wilaya ya Mafia mkoani Pwani baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mafia jana kuanza ziara ya siku mbili wilayani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mafia Shaib Nnunduma.
Mbunge wa jimbo la Mafia Mbaraka Dau akisisitiza jambo mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mafia wakati Naibu Waziri alipoanza ziara yake ya siku mbili wilayani Mafia mkoani Pwani. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mafia Shaib Nnenduma.
……………………
Na Munir Shemweta, MAFIA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kupatiwa majina ya watumishi saba wa sekta ya ardhi awaliopangiwa kuhamia halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani lakini wameshindwa kuripoti katika kituo chao kipya cha kazi.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana mwamzoni mwa ziara yake ya siku mbili katika wilaya ya Mafia mkoani Pwani kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kukagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki, kukagua Masijala ya ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi.
Kauli ya Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inafuatia kuelezwa na Mkuu wa wilaya ya Mafia Shaib Nnunduma kuwa wilaya yake ina mtumishi mmoja wa sekta ya ardhi jambo linaloifanya wilaya hiyo kushindwa kutekeleza majukumu ya sekta hiyo ipasavyo.
Dkt Mabula alisema, Wizara yake italifanyia kazi suala hilo mapema kwa kuwa ni vigumu wilaya kufanya kazi vizuri katika sekta ya ardhi kwa kutegemea mtumishi mmoja hasa ikizingatiwa sekta hiyo inahitaji kuwa na wapimaji, wathamini pamoja na wataalamu wa mipango miji.
‘’Mafia mna mtumishi mmoja wa sekta ya ardhi? Suala hili inabidi lifanyiwe kazi mapema na wizara yangu italifanyia kazi kuhakikisha wilaya inakuwa na watumishi wa njanja zote katika sekta ya ardhi’’ alisema Dkt Mabula
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mafia Shaib Nnunduma alimueleza Naibu Waziri Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, changamoto kubwa inayoikabili wilaya yake kwa upande wa sekta ya ardhi ni kukosekana watumishi wa kutosha ambapo wilaya hiyo imekuwa na mtumishi mmoja wa sekta hiyo kwa muda mrefu baada ya mtumishi mmoja wa Uthamini kupangiwa majukumu mengine.
Kwa mujibu wa Nnunduma, jitihada za wilaya yake kufuatilia upatikanaji Watumishi wa sekta ya ardhi zimeonekana kukwama kwa kuwa hadi sasa hawajapata mtumishi mwingine jambo linaloifanya wilaya hiyo kushindwa kutekeleza vyema majukumu ya sekta hiyo.
‘’Watumishi saba walipangiwa kuja Mafia lakini wameshindwa kuripoti na hapa unavyotuona tuna mtumishi mmoja, hatuna wataalamu kama wangekuwepo wangesaidia upangaji. Wilaya ni kama imesimama katika sekta ya ardhi’’ alisema Nnunduma
Nnunduma alisema, ujio wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaweza kuwa faraja kwao kupata watumishi kwa kuwa tangu kuteuliwa kwake na Rais John Pombe Magufuli kuongoza wilaya ya Mafia ndiyo anashuhudia Waziri wa kwanza wa sekta ya ardhi kwenda wilaya hiyo aliyoieleza kuwa kama itatumiwa vizuri basi itaiwezesha serikali kuingiza mapato mengi kupitia sekta ya utalii.
Mbunge wa jimbo la Mafia Mbaraka Dau alimueleza Dkt Mabula kuwa, pamoja na changamoto nyingine lakini Wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa la Baraza la Ardhi la nyumba  la wilaya jambo linalowalazimu wananchi kufunga safari hadi katika Baraza la Mkuranga kitu alichokieleza kinawafanya baadhi ya wananchi kushindwa kwenda na hivyo kupoteza haki zao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com