METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 3, 2019

MHE IKUPA: WENYE ULEMAVU WAJUMUISHWE KATIKA MASUALA YA UKIMWI


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akisalimiana na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wakati wa ziara yake wilayani hapo ili kukagua utekelezaji wa masuala ya Ukimwi katika Wilaya hiyo Oktoba 2, 2019.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akizungumza wakati wa kikao cha kupokea taarifa za wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua na kuangalia shughuli za utekelezaji wa masuala ya Ukimwi wilayani hapo..
Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akiuliza jambo kwa Mratibu wa Kudhibiti masula ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo Herieth Nyangasa (hayupo pichani)  wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi wa Utafiti na Tathimini kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) Dkt.Jerome Kamwela akifafanua jambo kuhusu masuala ya ukimwi nchini kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa wakati wa kikao hicho.
Mratibu wa Kudhibiti masula ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo Herieth Nyangasa akifafanua kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala ya ukimwi kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya wilaya alipotembelea Oktoba 2, 2019.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa (katikati) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab (wa pili kutoka kulia waliokaa), Katibu Tawala wa wilaya hiyo Desderia Haule (wa kwanza kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kikao katika ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo Oktoba 2, 2019.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
………………..
NA.MWANDISHI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masula ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa ameuasa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kushirikisha kundi la wenye ulemavu katika masuala ya UKIMWI ili kuhakikisha jamii nzima inapata elimu na huduma ya masuala hayo.
Ametoa kauli hiyo oktoba 2, 2019 wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani Tanga alipofanya ziara yake ya siku tatu mkoani hapo ili kutembelea na kukagua shughuli zinazotekelezwa wilayani hapo kuhusu masuala ya UKIMWI.
Alieleza kuwa kundi la wenye ulemavu limekuwa nyuma kwa muda mrefu katika kujumuishwa hususan katika masuala ya elimu na huduma za kijamii hivyo ni lazima kuzingatia mahitaji yao katika kuendelea kuwapa elimu na huduma za masuala hayo ili waweze kunufaika na huduma ili kupunguza na kuondoa maambukizi mapya katika mkoa mzima wa Tanga.
“Ni vyema kuhusisha kundi la wenye ulemavu katika upatikanaji wa huduma za masuala ya Ukimwi kwa kuzingatia kundi hili limekuwa likisahaurika na kutofikiwa kama yalivyo makundi mengine,”alieleza Mhe.Ikupa
Aliongezea kuwa miongoni mwa mikakati ya Halmashauri ni vyema kuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha huduma za masuala ya Ukimwi ikiwemo, utoaji elimu juu ya mabadiliko ya tabia na kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, kuwashirikisha katika program mbalimbali zinazojikita katika kuimarisha mifumo utoaji wa elimu ya masuala ya watu wanaoishi na VVU na mikakati ya kusaidia makundi hayo.
Alifafanua kuwa, kwa kufanya hivyo itasaidia kupungua kwa masuala ya ubaguzi katika jamii ili kuwa na usawa na haki kwani wenye ulemavu wanastahili kupewa huduma sawa katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Mwanashaa Rajab alieleza kuwa wameendelea kuwafikia watu wenye ulemavu katika huduma za upimaji, utoaji wa huduma za dawa na kuahidi kuendelea kuwajumusha katika shughuli zote zinazohusu masuala ya ukimwi ili kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na tisini tatu (909090).
“Tunakushukuru kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zetu na kukuahidi tutatekeleza maagizo yako ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti zinazojumuisha mahitaji maalum ya wenye ulemavu, kuwapatia elimu, kuwafikia na kuendelea kuwashirikisha katika program mbalimbali za kimaendeleo,”alisema Mwanashaa.
Naye Mratibu wa Kudhibiti masula ya Ukimwi katika Halmashauri hiyo Herieth Nyangasa alieleza kuwa hali ya maambukizi kipindi cha mwaka 2018 ni asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.6 kwa mwaka 2017 ambapo imechangiwa na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuwafikiwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili kuhakikisha maambukizi mapya yanapungua.
“Zipo jitihada nyingi zimefanyika kuhakikisha wanapunguza hali ya maambukizi mapya na kuwapatia huduma watu wanaoishi na VVU ikiwa ni pamoja na wilaya kuwa na vituo 445 vya kutolea huduma ya ushauri nasihi na upimaji wa VVU, vituo 20 vya upimaji kwa hiari, vituo 38 upimaji kwa ushawishi na vituo 45 vya huduma ya kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,”Alesema Nyangasa
Kwa upande wake Mratibu wa kudhibiti Ukimwi Wilayani humo Dkt. Yahaya Mbura alieleza changamoto zinazokwamisha jitihada za serikali katika kuwahudumia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuwa ni pamoja na tatizo la  utoro wa watumiaji wa dawa za kufubaza Virusi vya ukimwi ambapo alieleza imechangia kwa kikasi kikubwa kudhoofisha jitihada hizo.
“Hadi sasa tuna ripoti za utoro kwa wanaotumia dawa wapatao 388 na hii imechangiwa na changamto za miundombinu kipindi cha mvua, umbali wa vituo kutoka katika makazi yao pamoja na uwepo wa imani potofu kuhusu matumizi ya dawa hizo,”alisisitiza Dkt. Yahaya.
Aliongezea kuwa pamoja na changamoto hiyo, tayari zaidi ya watoro 212 walifanikiwa kuwarejesha katika huduma za upatiwaji wa dawa na kuendelea kutumia dawa.
AWALI
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ni moja kati ya Halmashauri 11 zilizopo Mkoa wa Tanga yeye jumla ya hekta za mraba 1,974 na jumla ya wakazi 204,461 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ambapo kati yao wanawake ni 103,618 na wanaume ni 100,843.Aidha ina jumla ya Kaya 47,920 yenye Tarafa 4, kata 37, vijiji 126 na Vitongoji 494 ambapo wilaya hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza afua za VVU na UKIMWI hasa zisizo za kitabibu.Wadau hao ni pamoja na SWAAT, SHDEPHA, WORLD VISION,KONGA,SHIVYAWATA,ZICOSAD,TIWAMWE, AMREF, AWCYS, MKUTA pamoja na BAKWATA.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com