Mtendaji Mkuu wa wakala ya
Serikali Dkt.Bakari Bakari,akiongea katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM)
kuhusu jitihada za utekelezaji wa Serikali Mtandao.
Ukurasa wa 152
Realistic device mockup white color smartphone
Ukurasa wa kuingilia ( log in page) wa mfumo Shirikishi wa kusimamia Rasimali za Taasisi
Ukurasa wa ndani wa mfumo Shirikishi wa Kusimamia Rasimali za Taasisi ukionyesha Moduli zote.
………………….
Uvumbuzi wa matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) umeleta fursa za maendeleo kwa mtu
binafsi au kwa taasisi husika na faida nyingi zisizomithilika katika
uendeshaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na maisha kwa ujumla
TEHAMA imekuwa ni njia mbadala ya kuhudumia wananchi na inapotumiwa na
taasisi za umma katika utekelezaji wa shughuli zake na katika
kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na kwa gharama nafuu ndiyo hujulika
kama serikali mtandao.
Hivyo, Serikali ya Tanzania katika
kuhakikisha inapata faida zitokanazo na matumizi ya TEHAMA kwa ufanisi,
iliamua kuundaa taasisi mpya ambayo ilipewa majukumu ya kuratibu na
kusimamia matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi za umma ili ziweze
kunufaika ipasavyo katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma
kwa wananchi.
Hivyo, kwa kuzingatia hili
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala
Bora, Mh. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Mb), anasema Serikali
ilianzisha Wakala ya Serikali Mtandao iliundwa kwa mujibu wa sheria Na.
30, Sura ya 245 ya mwaka 1997 chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikuwa na jukumu la kusimamia serikali
mtandao na kuratibu maendeleo ya TEHAMA ndani ya Serikali na taasisi
zake, baada ya kupitia matokeo ya tathmini ya hali halisi ya matumizi ya
TEHAMA katika utoaji wa huduma za serikali ambapo taasisi nyingi
zilionyesha kujitengenezea mifumo na raslimali nyingine za TEHAMA bila
kujali uwepo wa jitihata hizo katika taasisi nyingine. Hali hiyo
ilichochea kuwa na urudufu wa jitihata za TEHAMA zinazofanana na
zisizowasiliana wala kubadilishana taarifa.
Akizungumzia hali ilivyokuwa kabla
ya Serikali kujikita katika matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma kwa
umma, Mhe. Waziri anaelezea kuwa, Serikali mtandao ni nyenzo
inayotumika katika kubadili na kuboresha utendaji kazi katika taasisi za
umma na utoaji wa huduma kwa wananchi. “Kazi hii sio rahisi
kuifanikisha, inahitaji rasilimali za kutosha, utashi wa kisiasa,
watumishi waliobadilika kimtazamo na kimatendo ili kuhakikisha serikali
mtandao inatumika ipasavyo ndani ya Serikali na taasisi zake (G2G), kati
ya Serikali na sekta ya biashara (G2B) na kati ya Serikali na wananchi
(G2C). Ili kuyafikia yote haya, tunahitaji kubadili mifumo ya utendaji
katika Serikali kwa ujumla”.
Naye Mkurugenzi wa TEHAMA
Serikalini, Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
bora, Bw. Priscus anasema kuwa mwananchi anapata manufaa mengi kutokana
na matumizi ya TEHAMA kwa kuwa anarahisishiwa upataji wa huduma
mbalimbali hapo alipo bila kutembea umbali mrefu na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wa taasisi za umma, TEHAMA inarahisisha utendaji kazi na
kuongeza ufanisi katika kuhudumia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja
kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Akizungumzia mafanikio ya
serikali mtandao yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Wakala ya Serikali
Mtandao mwaka 2012 hadi sasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala, Dkt. Jabiri
Bakari anaeleza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa
serikali mtandao, husan katika maeneo ya sera, sheria na miongozo,
usimamizi, utengenezaji wa mifumo tumizi na ya kimkakati ya TEHAMA, na
ujenzi wa miundombinu ya pamoja ya TEHAMA.
Dkt. Bakari anafafanua kuwa,
katika hatua za utekelezaji wa majukumu yake, Wakala ilianza na
utayarishaji wa mpango mkakati wa miaka mitano ya kwanza (2012/2013 –
2016/2017), ambao ulihuishwa na kutoa mpango mkakati wa pili wa mwaka
2016/2017 hadi 2020/2021. Anaendelea kufafanua kuwa jitihada za awali za
kutekeleza malengo haya zilikuwa katika kushiriki katika matayarisho ya
sheria mbalimbali zinazohusiana na utekelezaji wa serikali mtandao kama
vile sheria ya miamala ya mwaka 2015, muswada wa sheria ya uhalifu wa
mtandao wa mwaka 2015 na kuandaa sheria ya serikali mtandao ambapo
muswada wake uliwasilishwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2019.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti wa
Huduma za Serikali Mtandao, Bw. Michael Moshiro, anaeleza kuwa
Mafanikio katika utekelezaji wa serikali mtandao yanapatikana kwa kuwa
na usimamizi imara. Katika kutekeleza hili Wakala imetayarisha
Miongozo, Viwango na Taratibu mbalimbali zinazotumiwa na taasisi za umma
katika kubuni, kujenga na kusimamia jitihada mbalimbali za TEHAMA ili
kuhakikisha inakidhi mahitaji halisi na kupunguza gharama za uwekezaji
na uendeshaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA.
Aidha anaeleza kuwa Viwango, Miongozo na Taratibu hizi zinazopatikana katika Tovuti ya Wakala sehemu ya Miongozo na Viwango https://www.ega.go.tz//standards
zinasaidia kuondoa urudufu wa mifumo na kuwezesha mifumo kuwasiliana,
kubadilishana taarifa pamoja, kulinda usalama wa taarifa, kuhuisha
mifumo kulingana na mahitaji mapya kwa urahisi na kuongeza uwazi na
udhibiti wa mifumo hasa inayojihusisha na ukusanyaji na usimamizi wa
Fedha kwa ile mifumo iliyotengenezwa au kufanyiwa mapitio na Wakala.
Naye Afisa TEHAMA Mwandamizi
kutoka RITA Bi. Robby Otaigo anasema Miongozo na Viwango vinavyotolewa
na Serikali Mtandao vikifuatwa vyema vinaleta tija ikiwa ni pamoja na
kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Aidha, Wakala inatekeleza
mkakati wa kuhakikisha inakuwa na watalaamu wabobezi wa ndani ambao
inawatumia katika maeneo yote ya utekelezaji wa serikali mtandao katika
kusanifu, kutengeneza, kusimamia na kuendesha mifumo na miundombinu
shirikishi ya TEHAMA, kusimamia usalama wa mifumo, miundombinu na
taarifa zilizomo na katika usimamizi wa utoaji wa huduma za serikali
mtandao kwa taasisi za umma na kusimamia shughuli za ubunifu na utafiti
wa jitihada za serikali mtandao kupitia kituo cha utafiti na ubunifu.
Anaeleza Dkt. Bakari.
Dkt Bakari anafafanua zaidi
kuwa kwa kutumia wataamu wabobezi wa ndani, Wakala ilifanikiwa
kusanifu, kutengeneza au kusimamia utengenezaji na uendeshaji wa mifumo
tumizi na shirikishi
mbalimbali ikiwemo ile ya
kimkakati kwa ajili yake yenyewe au kwa ajili ya matumizi ya taasisi
mbalimbali za umma kama vile Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS)
unaotumiwa na taasisi za umma 401 zikiwemo ofisi za Ubalozi nje ya nchi
kwa ajili ya kubadilishana taarifa Serikalini na Mfumo wa ofisi mtandao
(GeOS) unaotumiwa na taasisi 60 unarahisisha shughuli za utawala za kila
siku hususani mzunguko wa majalada na nyaraka ndani na miongoni mwa
taasisi za umma.
Mifumo mingine ni pamoja na Mfumo
wa Malipo ya Serikali Kielektroni (GePG) uliotengenezwa kwa
kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango unaotumika kusimamia
ukusanyaji wa mapato ya taasisi za umma. Mfumo huu unatumiwa na taasisi
za umma 524, watoa huduma za malipo 19 ambao ni Benki Kubwa 12 (NMB,
STANBIC, NBC, CRDB, EXIM, TIB, BOT, ECOBANK, PBZ, DCB, DTB, na TPB),
Mifumo ya Fedha ya Simu za Mkononi 5 (Tpesa, TigoPesa, HaloPesa, Mpesa,
EzyPesa na Airtel Money), mpaka sasa.
Anaendelea kufafanua mifumo mingine kuwa ni pamoja na Mfumo wa kuomba vibali vya kusafiri nje ya nchi kwa watumishi wa umma (https://safari.gov.go.tz) unaotumiwa na taasisi 436 , Mfumo wa Ajira (http://portal.ajira.go.tz)
unaotumika katika kuratibu zoezi zima la kupokea na kuchakata maombi ya
ajira katika taasisi zote za umma, Tovuti Kuu ya Taifa (www.tanzania.go.tz)
iliyohuishwa kutokana na tovuti ya Serikali inayosimamiwa na Wizara ya
Habari, Utamaduni na Michezo, ambayo ni dirisha moja la kutolea huduma
kwa wananchi na Mfumo wa Huduma kwa Wateja unaotumiwa na taasisi 392
ambao hadi sasa umepokea na kushughulikia maombi ya misaada 6230 ya
wateja.
Mfumo mwingine ni Mfumo
Shirikishi wa Kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (ERMS) ambao
ulitengenezwa kwa matumizi ya Wakala pia unaweza kutumiwa na taasisi
nyingine za umma baada ya marekebisho kidogo. Kwa sasa unatumiwa
nataasisi (4) ambazo ni Wakala yenyewe, Bodi ya Taifa wa Wahasibu na
Wakaguzi, Tume ya Ushirika na Tume ya Sayansi na teknolojia.
Akiuelezea kwa kina mfumo wa ERMS,
Dkt Bakari anasema, mfumo huu una moduli kumi na nane (18)
zinazotegemeana na zinazounganisha shughuli mbalimbali za utendaji kazi
ili kuwezesha kubadilishana taarifa miongoni mwa idara/vitengo na
kusimamia raslimali kama vile watu, fedha na vitendea kazi, ankra za
bidhaa na huduma, mapato na matumizi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa
shughuli kulingana na mipango na bajeti, usimamizi wa utekelezaji wa
majukumu ya watumishi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi, utekelezaji
wa shughuli za ununuzi na utayarishaji wa taarifa mbalimbali za
utendaji.
Aidha, Dkt. Bakari anafafanua
zaidi kuwa, mfumo huu una “dashboard” ambayo inawawezesha Maafisa
Masuuli na watumiaji wengine wa mfumo kupata taarifa mbalimbali
kulingana na mahitaji yao. Taarifa hizo zinaweza kuwa za fedha, vifungu
vya bajeti na bakaa ya fedha, hali ya matumizi ya fedha, taarifa
zinazosaidia katika upimaji wa utendaji wa watumishi, na hivyo kusaidia
katika utoaji wa maamuzi sahihi.
Kutilia mkazo maelezo yake,
Dkt. Bakari anasema ERMS pia inaweza kuunganishwa na kubadilishana
taarifa na mifumo mingine Mikuu ya Serikali kama vile Mfumo mkuu wa
uhasibu, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Rasilimaliwatu (HCMIS), Mfumo
wa Malipo ya Serikali
Kielektroni (GePG), Mfumo wa
Barua pepe Serikalini (GMS), Mfumo wa Ofisi Mtandao na kadhalika. Aidha
Moduli za Mfumo huu zinaweza kuongezwa au kupunguzwa bila kuathiri
utendaji kazi wa moduli nyingine au mfumo kwa ujumla.
“Mfumo huu unasaidia kuongeza
ufanisi katika matumizi ya rasilimali za TEHAMA, kuwezesha mifumo ya
taasisi za umma kuwasiliana, kuongeza uwazi, uwajibikaji, kuaminika kwa
mifumo ya Serikali na kuimarisha udhibiti wa taarifa kwa kuwa watumishi
wa Serikali tu waliopo ofisini ndio watakaopata data na mafaili”,
anasisitiza Dkt. Bakari.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi
wa Huduma za TEHAMA wa Wakala Injinia Benedict Ndomba anaeleza kuwa
katika eneo hili la mifumo tumizi, Wakala pia imetoa ushauri na msaada
wa kiufundi katika taasisi 350 kwa kutengeneza mifumo tumizi ya kisekta
40 inayoboresha utendaji kazi wa taasisi, tovuti zaidi ya 400, na kutoa
mafunzo kwa watumishi wa taasisi hizo katika kutekeleza jitihada za
serikali mtandao.
Anaeleza zaidi kuwa, Wakala ni msajili rasmi wa anuani
za tovuti zenye majina yanayoishia na “.go.tz’’ inayoitambuliwa na
Kituo cha Taarifa za Kimtandao Tanzania (TzNiC), ambapo kazi ya kusajili
tovuti zote za taasisi za umma ikiwemo zile zilizokuwa na majina
yanayoishia na .com na .org inafanyika.
Aidha, Dkt. Bakari anasisitiza
kuwa maendeleo ya serikali mtandao pia yanahitaji miundombinu ya TEHAMA
madhubuti, ambapo katika eneo hili Wakala imefanikiwa kusimamia ujenzi
na uendeshaji wa miundombinu shirikishi ya TEHAMA kwa ajili ya matumizi
ya taasisi mbalimbali za umma. Miundombinu hiyo ni pamoja na Mfumo wa
Huduma za Serikali kupitia simu za Mkononi (mGov) *152*00# ambao
unatumiwa na Taasisi 157 ambapo huduma mbalimbali ikiwemo malipo ya
Serikali (Maji, Umeme, Ardhi, ada za shule), zinapatikana kwa haraka,
gharama nafuu, na kufikika kwa urahisi moja kwa moja kupitia simu yenye
mtandao wowote wa simu za mkononi kama vile Tigo, Voda, TTCL, Halotel,
Airtel na Zantel.
Mingine ni Mtandao wa
Mawasiliano Serikalini (Govnet) ambao umeunganisha taasisi 147 za
Serikali kuu na Serikali za Mitaa zikiwemo hospitali na shule, na Kituo
cha Serikali cha Kuhifadhi Mifumo (GDC) kinachotumiwa na taasisi za umma
53 na kuhifadhi 230. Dkt. Bakari anaainisha.
Kama ilivyo katika jitihada
nyingine za maendeleo, utekelezaji wa Serikali Mtandao wenye ufanisi na
endelevu unahitaji utafiti na uchunguzi wa kina ili kubaini kiini cha
vikwazo vya uendeshaji na kupata ufumbuzi unaofaa na wenye manufaa kwa
Serikali na wananchi, Meneja wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa
Serikali Mtandao Bw. Leopold shayo, anasema Wakala imeanzisha Kituo cha
Utafiti na Ubunifu wa Serikali Mtandao kilichopo Chuo Kikuu Cha Dodoma
(CIVE), kwa ajili shughuli za utafiti na ubunifu wa maendeleo ya
serikali mtandao kitakachokutanisha wadau mbalimbali wenye mawazo ambayo
yakiendelezwa yataleta maboresho katika jitihada za utekelezaji wa
serikali mtandao katika taasisi za umma.
Aidha, Dkt. Bakari anaeleza
kuwa, katika miaka saba ya utekelezaji wa jitihada hizi zote, changamoto
mbalimbali zilijitokeza kama vile usalama wa mifumo na miundombinu
pamoja na
taarifa zilizomo, umadhubuti
wake, urudufu, rasilimali watu wenye ujuzi wa kutosha, usahihi wa
matumizi na gharama kubwa za utekelezaji wa jitihada za serikali
mtandao.
Anaendelea kueleza kuwa, masuala mengine yaliyohitaji kuwekwa
sawa ni pamoja na namna ya kukabiliana na wakandarasi wa mifumo tumizi
na vitumi vya aina mbalimbali kama vile kompyuta, seva na vinginevyo,
ikiwemo gharama kubwa za usimikaji na usanikishaji iliyokuwa inaamuliwa
kwa manufaa ya watu binafsi.
Dkt. Jabiri Bakari akihutubia
washiriki kuhusu uwezo wa Mifumo ya TEHAMA inayotengenezwa nchini katika
nchi zinazoendelea wakati wa Mkutano wa 15 wa Kimataifa wa Athari za
Kijamii za Kompyuta kwenye nchi zinazoendelea uliofanyika Dar es Salaam,
tarehe 2 Mei, 2019 anasema kuwa, ni lazima izingatiwe kuwa matatizo
yetu si makubwa, hivyo hayahitaji ufumbuzi unaotumia mifumo mikubwa,
Ila, tunaendelea kuyafanya yawe makubwa kwa kuendelea kutumia mifumo
iliyotengenezwa bila kuzingatia mahitaji halisi ya taasisi husika.
Kutokana na hali hii, “tunalazimika kutumia rasilimali nyingi, kama vile
fedha, muda, watu na hata miundombinu yenye uwezo mkubwa sana usio wa
lazima ambao hauendani na mahitaji na mazingira halisi ya taasisi
husika.” Anaeleza Dkt Bakari.
Aidha anongeza kuwa, uzoefu
unaonesha kuwa michakato mingi ya utendaji shughuli za Serikali
haikuungana, imekuwa migumu bila ya sababu na haiendani na mtiririko wa
kawaida wa utendaji kama ilivyo na kusababisha matatizo kutokana na
mazoea ya kutumia mikono. Kinachotakiwa ni kufanya jitihada ya dhati ya
kufanya marekebisho ya kiufundi ya uendeshaji kazi ili kupata michakato
iliyosanifiwa upya na kujumuishwa itakayoboreshwa kwa kutumia TEHAMA.
Dkt. Bakari anasema katika
kipindi cha miaka saba iliyopita, Wakala ya Serikali Mtandao imefuatilia
na kutengeneza mifumo na huduma mbalimbali za serikali mtandao
zinazomilikiwa na Serikali kwa asilimia mia (100%).
Anaendelea kusema
“Sifa muhimu za mifumo yetu ya serikali mtandao ni pamoja na urahisi
wake kulingana na mazingira yetu ya utendaji, gharama ndogo za
uendeshaji, ukubwa wake unaolingana na ukubwa wa kazi na mahitaji na
uwezo wa ndani uliyoimarishwa”.
Naye Meneja Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Wakala Bi. Suzan Mshakangoto anasema kuwa, Wakala pia
imekuwa ikishirikiana kikamilifu na wadau wake wote kama vile Taasisi za
Umma, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti, (Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Habari na Teknolojia ya Mawasiliano (CoICT)
cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Wadau wa Maendeleo na Wananchi
ili kuwa na uekelezaji madhubuti wa Serikali Mtandao nchini
Aidha Bi Suzan anasema kuwa
Wakala imeendelea kuelimisha umma kuhusu utekelezaji wa Serikali Mtandao
kwa kuandaa Vikao Kazi viwili vya mwaka vya Serikali Mtandao kwa lengo
la kubadilishana uzoefu, kujadili njia mbalimbali za kutatua changamoto
na kuleta uelewa wa pamoja wa hali ya matumizi ya TEHAMA katika taasisi
za umma. Vikao hivyo vimesaidia kuweka mkakati wa pamoja wa namna ya
kuzitatua changamoto za TEHAMA na kuona jinsi TEHAMA inavyoweza kutumika
katika kuijenga Tanzania ya viwanda.
“Kikao Kazi cha kwanza
kilifanyika Arusha kuanzia Agosti 17 hadi 20, 2015 na kilihudhuriwa na
washiriki zaidi ya 700 na Kikao Kazi cha pili cha Serikali Mtandao
kilifanyika Januari 30 hadi Februari 2, 2019 katika Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM) katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na
Mawasiliano na kilihudhuriwa na washiriki 786 kutoka taasisi mbalimbali
za Serikali. Aidha taarifa zote zimekuwa zikiwekakatika tovuti ya Wakala
http://www.ega.go.tz, na mitandao ya kijamii kwa jina la tzegovernmen”, anasema Bi. Mshakangoto.
“Sisi kama Wakala tutaendelea
kubuni, kusanifu na kutengeneza mifumo kwa kutumia wataalamu wetu wa
ndani ili kukidhi mahitaji yetu halisi, tutaendelea kuwajengea uwezo
wataalamu wa TEHAMA Serikalini katika maeneo mbalimbali ikiwamo eneo la
usalama wa mifumo na taarifa zilizomo, tutaendea kujenga mazingira
wezeshi kwa taasisi za umma ili ziweze kuwahudumia wananchi kwa kutumia
TEHAMA na pia tutaendelea kushirikiana na wadau wetu wote ili kuona
namna bora ya kutumia TEHAMA katika kutoa huduma kwa umma”, Dkt. Bakari
anamalizia kwa msisitizo.
0 comments:
Post a Comment