METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 2, 2020

WAHANDISI WAZAWA WATAKIWA KUWA WAZALENDO


Wahandisi wazawa wametakiwa kuwa wazalendo kwa kuweka maslahi ya taifa mbele badala yao binafsi ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini.

Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo  jimboni humo ambapo amewataka wahandisi wataalamu washauri wa mradi wa stendi ya kisasa ya mabasi inayojengwa katika kata ya Nyamhongolo kuwa wazalendo kwa kurudi eneo la mradi haraka iwezekanavyo ili fedha iliyowekezwa na Serikali ya awamu ya tano kwaajili ya ujenzi wa stendi hiyo iweze kuleta tija baada ya wataalamu hao kutokuwepo eneo la kazi kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na  kuchelewa kwa malipo wanayodai

'.. Niwatake wahandisi wetu kuwa wazalendo na kurejea mara moja eneo la kazi  wakati mie nikifuatilia madai yao wizara ya fedha ..' Alisema

Aidha Mhe Dkt Mabula akiwa katika kituo cha afya buzuruga akaishukuru Serikali ya Rais Dkt John Magufuli kwa kutoa milioni mia nne kwaajili ya ujenzi wa kituo hicho na wadau kutoka Aga Khan Foundation waliofadhili ujenzi wa jengo la upasuaji huku akikemea vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya walinzi wa kituo hicho kwa kutoa lugha chafu kwa wateja wanaofuata huduma katika kituo hicho.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa manispaa Ilemela Ndugu Shukrani Kyando amemuhakikisha mbunge huyo kuwa manispaa yake itamalizia miradi yote iliyoanzishwa na wananchi baada ya mbunge huyo kutoa matofali ya ujenzi ili kwenda sambamba na Sera ya jimbo hilo ya utatu kwa wananchi kuanzisha misingi, mbunge kutoa tofali za ujenzi wa boma na manispaa kumalizia sanjari na kuandaa viwanja zaidi ya 500 kwaajili ya watumishi wa sekta ya afya na elimu.

Nae Mhandisi wa manispaa ya Ilemela mbali na kumshukuru mbunge Dkt Angeline Mabula kwa ahadi yake ya kufuatilia madai ya wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ndani ya jimbo hilo akaongeza kuwa mradi wa stendi ya Nyamhongolo umefikia asilimia 22 na utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 27 mpaka kukamilika kwake ukichukua muda wa miezi 18.

Katika ziara hiyo mbunge Dkt Mabula aliweza kutembelea shule ya sekondari Buswelu, shule ya msingi Gedeli, Zahanati ya Nyakato, Stendi ya Nyamhongolo na ujenzi wa mradi wa kisasa wa mzani wa mazao ya samaki Kirumba.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com