METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 3, 2019

DKT.KALEMANI AMSIMAMISHA KAZI ALIYESABABISHA UMEME KUKATIKA KWA UZEMBE


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,( kulia) akielezwa namna Mfumo wa Gridi ya Taifa,unavyofanya kazi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,( kushoto)akitoa maelezo kwa baadhi ya watendaji katika kituo cha umeme cha umbongo, huku akiwa ameshika kifaa kilichokatika baada ya kuungua na kusababisha kukatika kwa umeme usiku wa octoba, 03,2019.
Transifoma kubwa namba sita( T6) inayozalisha umeme wa Megawati 120 iliyopata hitilafu baada ya kifunga stimu(Fuse) kuungua na kukatika.
Mafundi wakiendelea na kazi ya kufunga mtambo mkubwa mpya wa umeme wa Megawati 240, utakaoimarisha huduma ya umeme kwa Mikoa wa Dar es salaam na Pwani.
Mmoja wa wasimamizi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza  Umeme cha Ubungo akimuonyesha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, sehemu ambayo kifunga stimu( fuse)iliyoungua na kukatika ilipokuwa imekaa.
………………..
Na Zuena Msuya, Dar es salaam,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amemsimamisha kazi kwa uzembe, Mhandisi Samson Mwangulume wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) baada ya umeme kukatika kutokana na hitilafu iliyotokea katika Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Ubungo, Jijini Dar es salaam.
Umeme huo ulikatika usiku wa Octoba 03, 2019 na kusababisha Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar kukosa huduma ya umeme kwa muda.
Aidha aliwataka watumishi 6 wa TANESCO, wanaosimamia Mifumo ya Gridi ya Taifa kuhamia katika nyumba zilizojengwa na Serikali katika Kituo cha Kupoza na kusambaza umeme cha  Ubungo, hadi kufikia saa nane mchana ya Octoba 03,2019 akiwemo Mkuu wa mfumo huo.
Dkt. Kalemani alisema hayo  baada ya kufanya ziara ya kutaka kujua tatizo lililosababisha umeme kukatika, pamoja na laini ya kusafirisha umeme kutoka katika Gridi ya Taifa juzi, octoba 1,2019, katika sehemu ya Ubungo umbali wa kilometa 22 kuelekea mkoani Morogoro.
Baada kutembelea kituo hicho na kuona mfumo mzima wa kusafirisha umeme kwa njia ya Kieletroniki( SCADER) na kupata maelezo kutoka kwa wataalam, imebainika kuwa chanzo cha hitilafu hiyo ni uchafu katika vikombe(Broker) katika Transifoma kubwa namba sita( T6) inayozalisha umeme wa Megawati 120 hivyo kusababisha kifunga stimu( Fuse)kuungua na kukatika.
Dkt.Kalemani, alisema kutokea kwa tatizo hilo ni uzembe uliofanywa na msimamizi aliyekuwa zamu siku hiyo pia kutofanya kazi yake kwa ufanisi, pamoja na kutofanyika kwa ukaguzi na matengenezo ya mitambo hiyo mara kwa mara.
“ Wataalamu wangu wamenambia kuwa kuna fyuzi ilikatika, lakini nimetaka kujiridhisha, nimetembelea mfumo wa usafirisha nimeona, nimekuja katika transifoma nimeona,sababu kubwa waliyonieleza ni uchafu, sasa hili swala la uchafu ni uzembe uliofanywa na aliyekuwa zamu kushindwa kubadilisha na kufanya usafi katika vikombe hivyo, nimetoa maelekezo huyu Samsoni  aliyekuwa zamu namsimamisha kazi kutokana na uzembe wake, atupishe watasimamia wengine,” alisema Dkt. Kalemani.
Akizungumzia wasimamizi wa mfumo wa gridi ya taifa kuishi katika nyumba zilizopo katika kituo cha ubungo, Dkt.Kalemani alisema kuwa dhimuni la watumishi hao kuishi katika nyumba hizo, ni kuweza kutatua kwa haraka na kwa wakati tatizo lolote linaloweza kutokea katika mitambo hiyo, badala ya kuanza kutafutwa na kutembea umbali mrefu kuja kutatua tatizo.
Vilevile kuimarisha  na kuongeza udhibiti na usimamizi katika Gridi ya Taifa.
Pia ametoa onyo kwa msimamizi wa mfumo wa Gridi ya Taifa kutoka Ubungo hadi Kidato mkoani Morogoro, kuhakikisha changamoto ya kukatika umeme kwa wakazi wa Kimara na maeneo jirani halitokei tena na endapo litatokea aache kazi mwenyewe.
Dkt.Kalemani alilazimika kutoa ovyo hilo, baada ya msimamizi huyo kusema kuwa tayari ameweza kudhibiti tatizo lililokuwa likitokea mara kwa mara na kuleta adha kwa wakazi wa eneo hilo.
Alisema kwa sasa umeme upo mwingi nawa kutosha hivyo hakuna sababu ya kukatika, na hitilafu zinazotokea ni kutokana na uzembe wa wahusika  kutosimamia mitambo vizuri na kusababisha uharibufu .
Kuhusu kuimarisha huduma ya umeme kwa Jijini la Dar es salaam, na Mkoa wa Pwani, Dkt. Kalemani alisema kuwa tangu mwezi uliopita wameanza kufunga mtambo mpya mkubwa wa megawati 240 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Mtambo huo utakuwa mbadala wa mitambo miwili ya zamani iliyoanza kufanya kazi tangu mwaka 1975, hivyo kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme Dar es salaam na Pwani kwa kiasi kikubwa.
Vile vile amemuagiza Kaimu Mkuu Msaidizi wa Kituo cha Ubungo pamoja na usambazaji wahakikishe wanasimamia zoezi la kutoa mizigo yote iliyopo bandarini ili kuweza kurahisisha ukamilishwaji wa ufungaji wa mtambo huo mpya ambao umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 16.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com