*Unatarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 10
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekagua ujenzi wa mradi wa maji wa Kintiku – Lusilile ulioko Manyoni
ambao awamu yake ya kwanza inatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 22,
mwaka huu.
Akizungumza na watumishi na
wakadarasi leo (Ijumaa, Oktoba 4, 2019) mara baada ya kukagua mradi huo
akiwa njiani kuelekea Manyoni, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na
ujenzi huo pamoja na kasi ya mkandarasi.
Waziri Mkuu ambaye ameanza
ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Singida, alielezwa kwamba mradi huo
utahudumia vijiji 11 vya Kintinku, Lusilile, Maweni, Mvumi, Ngaiti,
Chikuyu, Mwiboo, Mbwasa, Mtiwe, Makutupora na Chilejeho ambavyo viko
kando ya barabara kuu itokayo Singida kwenda Dodoma.
Akitoa taarifa ya mradi mbele
ya Waziri Mkuu, Meneja wa RUWASA, Injinia Gabriel Ngongi alisema
wananchi zaidi ya 55,000 watanufaika na mradi huo pindi utakapokamilika.
Alisema awamu ya kwanza imegharimu sh. bilioni 2.46.
Akizungumzia halia halisi ya
utekelezaji wa mradi huo, alisema ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la
lita 300,000 limekamilika lakini bado liko kwenye hatua ya umaliziaji.
“Birika la kuhifadhia maji lemye ujazo wa lita milioni mbili
limekamilika, bado shughuli za umaliziaji,” aliongeza.
Alisema ujenzi wa uzio, nyumba
ya kuhifadhia mitambo na nyumba ya mlinzi umekamilika licha ya kuwa
bado kuna kazi ndogo za umaliziaji.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Itigi.
0 comments:
Post a Comment