
Waziri wa Maji, Prof. Makame
Mbarawa akizungumza na wafanyakazi kutoka Kampuni ya Shanxi
inayotekeleza Mradi wa Maji wa Tandangongoro katika Manispaa ya Lindi.

Ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji
wa Nandambi katika Manispaa ya Mji wa Lindi ukiwa umekamilika ambapo
mradi wote utakapokamilika utagharimu jumla ya kiasi cha Shilingi
milioni 825.

Wakazi wa Kijiji cha Kineng’ene wakiteka maji katika Mradi wa Maji wa Kineng’ene katika Manispaa ya Lindi.

Waziri wa Maji, Prof. Makame
Mbarawa akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nandambi na
kuwahikikishia kuwa Serikali itatoa fedha ya kununua mabomba ya
kusambaza maji ili kazi hiyo iliyobaki iweze kukamilika haraka
iwezekanavyo na waanze kupata huduma ya maji.

Waziri wa Maji, Prof. Makame
Mbarawa akimuonyesha gharama za mabomba Mkandarasi wa Kampuni ya Canopy
inayotekeleza Mradi wa Maji wa Ng’apa Vijijini. Kulia ni Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Lindi, Shaibu Ndemanga.

Mkandarasi akiendelea na kazi ya ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Tandangongoro katika Manispaa ya Lindi.
………………….
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa amesema kuanzia sasa amesitisha kutoa vibali vya ujenzi wa
miradi ya maji kwa wakandarasi kutokana na wengi wao kuwa wadanganyifu
katika makadirio ya gharama za utekelezaji wa miradi hiyo na
kuisababishia Serikali mzigo mkubwa na kukwama kwa miradi mingi katika
maeneo mbalimbali nchini.
Kauli imekuja akiwa ziarani
mkoani Lindi akitembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maji katika
Manispaa ya Mji wa Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi katika
kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo inaenda kwa kasi na kukamilika
kwa wakati.
Profesa Mbarawa amesema baada
ya kutembelea miradi mingi ya maji amegundua tabia ya wakandarasi wengi
wasio waadilifu kuweka gharama kubwa ili kupata faida kubwa, na kumfanya
kuchukua uamuzi wa kusitisha vibali vya ujenzi kwa wakandarasi na kutoa
kazi hizo kwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA) pamoja na Mamlaka za Maji.
Akifafanua kuwa maamuzi hayo
yamelenga kukomesha tabia hiyo ya wizi wa fedha za Serikali na kuokoa
fedha nyingi zinazoweza kutumika katika utekelezaji wa miradi katika
maeneo mengine mengi na pia kuipa nafasi Serikali kukamilisha ujenzi wa
miradi yake kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Profesa
Mbarawa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi na Mkandarasi wa
Kampuni ya M/S Halem Construction Co. Ltd wakae chini na kufikia
makubaliano ya kuiacha Wizara ya Maji ifanye utaratibu wa manunuzi ya
bomba za kusambaza maji kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Nandambi kwa
dhumuni la kuhakikisha unakamilika kwa wakati kutokana na mkandarasi
huyo kusuasua.
Profesa Mbarawa amesema fedha za ununuzi wa mabomba hayo zipo na ndani ya wiki mbili mabomba yatakuwa yamefika site kwa ajili ya kukamilisha mradi huo unaotakiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Septemba, 2019 kwa gharama ya Shilingi milioni 825.
Aidha, wakazi wa Kijiji cha
Nandambi wamweleza Waziri wa Maji, Prof. Mbarawa kuwa hatua hiyo itakuwa
na msaada mkubwa kwao ikizingatiwa kuwa mradi huo ulioanza utekelezaji
wake Agosti, 2018 na unatakiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019 bado
mkandarasi hatoi matumaini ya kukamilisha mradi huo kwa asilimia 100
pamoja na ujenzi wa tenki kuwa umekamilika.
Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa
Mkoa ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema Serikali ya Mkoa wa Lindi
itahakikisha mazungumzo hayo yanafanyika pasipo kupoteza muda ili hatua
iliyobaki ikamilike na wananchi wa Nandambi wanufaike na maji.
0 comments:
Post a Comment