








(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
……………………..
NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji nchini Mhe.Angellah Kairuki
ameutaka uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutembelea na
kugakua mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji wazawa waliopo mkoa
wa Ruvuma ndani ya siku saba.
Ametoa kauli hiyo alipotembelea na
kukagua kiwanda cha kutengeneza kahawa cha Wilaya ya Mbinga cha MCCCO
pamoja na kiwanda cha DAE kwa lengo la kukagua mazingira na utendaji wa
viwanda hivyo Mkoani Ruvuma.
Ziara hiyo iliambatana na Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina Mdeme pamoja na watendaji kutoka Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Viwanda,
Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Wizara ya Ardhi,
pamoja na baadhi ya taasisi za serikali ikiwemo na Kituo cha Uwekezaji
Nchini (TIC).
Waziri Kairuki alitoa maelekezo
hayo baada ya kubaini kuwa kituo hicho hakijawafikia wawekezaji wazawa
kikamilifu hususani waliopo mikoani ili kuwatambua na kuwaelimisha
kuhusu fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.
“Ninawaagiza TIC mfike katika
viwanda hivi ndani ya siku saba kuanzia sasa ili kuwatembelea na
kuwaeeleza huduma zinazotolewa na taasisi yenu ikiwemo fursa zilizopo na
endapo wataona inafaa wajisajiri kwa kuwa ni suala la
hiari,”alisisitiza Waziri Kairuki
Aidha alieleza kuwa ipo tija ya
kuwatambua wawekezaji wazawa waliopo nchini ka kuzingatia mchango wao
katika uchumi wa viwanda kwa kuzingatia mwaka 2019 ni mwaka wa
uwekezaji.
“Naelewa kuwa ipo miradi mingi
iliyofikiwa na TIC zaidi ya asilimia 72 hivyo niwatake mfike haraka
mkoani Ruvuma hususan katika viwanda hivi vya kahawa, ili kuvitambua na
kueleza fursa na umuhimu wa kujisajili na Taasisi hii ili kuendelea
kuchangia na kuwa na tija zaidi katika uchumi wa nchi,”alisisitiza
Mkurugenzi wa Sera Mipango na
Utafiti wa TIC Mafutah Bunini amesema katika kuboresha utendaji wao
wamefungua ofisi za kanda saba ili kuwafikia kwa urahisi wawekezaji wa
ndani na kwamba wanaotoa uzito sawa kwa wawekezaji wa ndani na nje.
“Na katika hili ndiyo maana
viwango vya mitaji ya uwekezaji vinatofautiana kwa wawekezaji wa nje na
ndani ambapo mwekezaji wa ndani anatakiwa awe na mtaji wa dola laki moja
lakini mwekezaji wa nje ni dola laki tano.
Naye Meneja wa Kiwanda cha
kutengeneza kahawa cha Wilaya ya Mbinga (MCCCO) amemuahakikishia Waziri
kuwa wataendelea kuboresha mazingira mazuri ya wafanyakazi na kuongeza
thamani ya bidhaa zao za kahawa na kuhakikisha jamii iliyowazunguka
inanufaika na kiwanda hicho.
“tunaishukuru Wizara ya Uwekezaji
kwa jitihada inazofanya za kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuondoa
vikwazo mbalimbali vilivyokuwepo awali hali inayosababisha uwekezaji
kukua kwa kasi”
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha kutengeneza kahawa cha DAE Bw. Danistan Komba
ambaye pia ni mkulima wa kahawa alimpongeza waziri kwa kutembelea
kiwandani hapo na kueleza changamoto za masoko ya kahawa na kuiomba
Serikali kuendelea kuwaangalia wawekezaji hao wazawa.
“Kipekee napongeza ujio wako, japo
tunachangamoto ya masoko kwa kuzingatia kiwanda kina uwezo wa kuzalisha
tani 36,000 kwa mwaka na kuuza katika baadhi ya nchi,”alieleza Komba
Alifafanua kuwa, pamoja na
changamoto za uhaba wa masoko, kiwanda kimekuwa kikishiriki katika
maonesho ya nchi zinazolima kahawa ikiwemo Kenya, Uganda,Rwanda,Burundi
na Ethiopia.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga
Cosmas Nshenye alieleza kuwa, ziara hiyo imeleta chachu kwa
wafanyabiashara na wawekezaji wazawa kwa kuzingatia kuwa, Serikali
imeahidi kutoa ushirikiano wa kina katika kutatua changamoto zao ikiwemo
kuwataka TIC kufika na kuwatembela katika muda alioagiza.
0 comments:
Post a Comment