Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Israel wakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 mara baada ya kuwapokea vijana kutoka Tanzania waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo ya Agrostudies. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Israel Mhe Uri Yehuda Ariel HaCohen wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za wizara hiyo eneo la Bet Dagan 50250 nchini Israel, tarehe 5 Septemba 2019.
Sehemu ya vijana kutoka Tanzania waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo ya Agrostudies wakipokea maelekezo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 mara baada ya kuwapokea
Ujumbe
wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Balozi wa
Tanzania nchini Israel wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Jengo la Wizara ya Kilimo na Maendeleo vijijini ya Israel, tarehe 5 Septemba 2019.
Na Mathias Canal, Jerusalem-Israel
Kundi la vijana wa
kitanzania 60 limewasili nchini Israel kwa ajili ya kushiriki mafunzo ya Kilimo ya
Agro Studies katika kipindi cha mwaka mmojahuku wengine 40 wakitarajiwa kuwasili tarehe 11 Septemba 2019 kukamilisha idadi ya vijana 100.
Vijana hao wamewasili tarehe 5 Septemba 2019 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini
Tel Aviv nchini Israel na kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet
Hasunga (Mb).
Waziri
Hasunga amewataka vijana hao kutumia mafunzo hayo kama muarobaini wa kuendeleza
sekta ya Kilimo watakaporejea nchini Tanzania hivyo kuwa chachu ya maendeleo
yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe
Magufuli.
“Ninyi
mmekuja Israel mkiwa katika mtazamo wa kujifunza hivyo mambo mengine yote
wekeni pembeni mzingatie masomo na katika kipindi cha mwaka mmoja mhakikishe
mmetumia muda wenu wa masomo vizuri kujifunza, kupata maarifa na ujuzi ili
mtakaporejea nyumbani mlete mabadiliko makubwa kwenye kilimo” Alikaririwa Mhe
Hasunga
Mhe Hasunga amewataka
vijana hao kuwa waaminifu wakati wote wa masomo yao kwani wanaiwakilisha
Tanzania hivyo vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu itakuwa ni sehemu ya
kulizalilisha Tanzania.
Alisema kuwa vijana
hao wanapaswa kuwa na bidii na kuweka pembeni tabia zisizofaa kwani kuwa na
maadili mema itawarahisishia vijana hao kupata utaalamu jadidu ambao utakuwa na
manufaa makubwa kwao na Taifa kwa ujumla wake.
“Tunataka mabilionea
wanaoibuka Tanzania watokane na sekta ya kilimo hususani vijana ambao mmepata
fursa ya masomo nchini Israel, Rais Magufuli alishatangaza kuwa wakati wa
utawala wake lazima mabilionea wapatikane” Alisema
Aliongeza kuwa ni
matarajio ya serikali kuona vijana hao watakaporejea Tanzania wanaanzisha
viwanda mbalimbali kwani malighafi nyingi zinatokana na sekta ya kilimo.
Mhe Hasunga amewataka
vijana hao kutojihusisha na siasa kwani hivi sasa ni kipindi cha kuelekea
uchaguzi mkuu wa Israel. “Acheni kabisa kujiingiza kwenye siasa maana siasa za
huku haziwahusu, waacheni waendelee na mambo yao nanyi endeleeni na
kilichowaleta” Alisisitiza Mhe Hasunga
Kwa upande
wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima amewataka vijana
hao kutekeleza maelekezo waliyopatiwa na Waziri wa Kilimo.
“Chochote
mtakachofanya ni Mtanzania amefanya kwahiyo mkifanya mabaya mtasambaza sifa
mbaya ya nchi katika Mataifa mengine jambo ambalo halitakiwi”
Balozi
Masima hakusita kuwapongeza vijana 45 ambao wamerejea nyumbani Tanzania baada
ya kuhitimu masomo yao kwani wameacha alama kubwa na nzuri inayoitangaza
Tanzania.
Wakizungumza
kwa niaba ya vijana waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo hayo ya
Kilimo ya Agrostudie, Janeth Patrick na Simion Jalusi wamemuhakikishia Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga kuwa wataiwakilisha vyema Tanzania ili liweze
kufanikiwa kufika kwenye Taifa la Viwanda.
“Tutajifunza
kwa bidii kubwa ili elimu tutakayoipata tuweze kuitumia vizuri kwa ajili ya
kuboresha sekta ya Kilimo nchini Tanzania” Walikaririwa wakisema
Vilevile,
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) amekutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Israel Mhe Uri Yehuda
Ariel HaCohen na kukubaliana kwa kauli moja serikali za nchi hizo mbili kuingia
makubaliano ya kuendeleza kilimo hususani katika utafiti, Tija katika
uzalishaji, na Teknolojia.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment