Thursday, September 5, 2019

VIJANA 60 KATI YA 100 WAWASILI NCHINI ISRAEL, WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AWAFUNDA KUHUSU NIDHAMU NA KUJITUMA

Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Israel wakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 mara baada ya kuwapokea vijana kutoka Tanzania waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo ya Agrostudies. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Israel Mhe Uri Yehuda Ariel HaCohen wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za wizara hiyo eneo la Bet Dagan 50250 nchini Israel, tarehe 5 Septemba 2019.
Sehemu ya vijana kutoka Tanzania waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo ya Agrostudies wakipokea maelekezo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv nchini Israel tarehe 5 Septemba 2019 mara baada ya kuwapokea 
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Balozi wa Tanzania nchini Israel wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Jengo la Wizara ya Kilimo na Maendeleo vijijini ya Israel, tarehe 5 Septemba 2019.

Na Mathias Canal, Jerusalem-Israel

Kundi la vijana wa kitanzania 60 limewasili nchini Israel kwa ajili ya kushiriki mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies katika kipindi cha mwaka mmojahuku wengine 40 wakitarajiwa kuwasili tarehe 11 Septemba 2019 kukamilisha idadi ya vijana 100.

Vijana hao wamewasili tarehe 5 Septemba 2019 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion Jijini Tel Aviv nchini Israel na kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb).

Waziri Hasunga amewataka vijana hao kutumia mafunzo hayo kama muarobaini wa kuendeleza sekta ya Kilimo watakaporejea nchini Tanzania hivyo kuwa chachu ya maendeleo yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli.

“Ninyi mmekuja Israel mkiwa katika mtazamo wa kujifunza hivyo mambo mengine yote wekeni pembeni mzingatie masomo na katika kipindi cha mwaka mmoja mhakikishe mmetumia muda wenu wa masomo vizuri kujifunza, kupata maarifa na ujuzi ili mtakaporejea nyumbani mlete mabadiliko makubwa kwenye kilimo” Alikaririwa Mhe Hasunga

Mhe Hasunga amewataka vijana hao kuwa waaminifu wakati wote wa masomo yao kwani wanaiwakilisha Tanzania hivyo vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu itakuwa ni sehemu ya kulizalilisha Tanzania.

Alisema kuwa vijana hao wanapaswa kuwa na bidii na kuweka pembeni tabia zisizofaa kwani kuwa na maadili mema itawarahisishia vijana hao kupata utaalamu jadidu ambao utakuwa na manufaa makubwa kwao na Taifa kwa ujumla wake.

“Tunataka mabilionea wanaoibuka Tanzania watokane na sekta ya kilimo hususani vijana ambao mmepata fursa ya masomo nchini Israel, Rais Magufuli alishatangaza kuwa wakati wa utawala wake lazima mabilionea wapatikane” Alisema

Aliongeza kuwa ni matarajio ya serikali kuona vijana hao watakaporejea Tanzania wanaanzisha viwanda mbalimbali kwani malighafi nyingi zinatokana na sekta ya kilimo.

Mhe Hasunga amewataka vijana hao kutojihusisha na siasa kwani hivi sasa ni kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Israel. “Acheni kabisa kujiingiza kwenye siasa maana siasa za huku haziwahusu, waacheni waendelee na mambo yao nanyi endeleeni na kilichowaleta” Alisisitiza Mhe Hasunga

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Balozi Job Daud Masima amewataka vijana hao kutekeleza maelekezo waliyopatiwa na Waziri wa Kilimo.

“Chochote mtakachofanya ni Mtanzania amefanya kwahiyo mkifanya mabaya mtasambaza sifa mbaya ya nchi katika Mataifa mengine jambo ambalo halitakiwi”

Balozi Masima hakusita kuwapongeza vijana 45 ambao wamerejea nyumbani Tanzania baada ya kuhitimu masomo yao kwani wameacha alama kubwa na nzuri inayoitangaza Tanzania.


Wakizungumza kwa niaba ya vijana waliowasili nchini Israel kwa ajili ya mafunzo hayo ya Kilimo ya Agrostudie, Janeth Patrick na Simion Jalusi wamemuhakikishia Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga kuwa wataiwakilisha vyema Tanzania ili liweze kufanikiwa kufika kwenye Taifa la Viwanda.


“Tutajifunza kwa bidii kubwa ili elimu tutakayoipata tuweze kuitumia vizuri kwa ajili ya kuboresha sekta ya Kilimo nchini Tanzania” Walikaririwa wakisema 

Vilevile, Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Israel Mhe Uri Yehuda Ariel HaCohen na kukubaliana kwa kauli moja serikali za nchi hizo mbili kuingia makubaliano ya kuendeleza kilimo hususani katika utafiti, Tija katika uzalishaji, na Teknolojia.

MWISHO

No comments:

Post a Comment