
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa
anatoka kwenye jengo la kituo cha afya Mkuyuni, baada ya kukagua ujenzi
wa kituo hicho, katika Wilaya ya Morogoro, Septemba 18.2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi wa Mkuyuni, wilayani Morogoro, Septemba 18.2019.

Wananchi wa Mkuyuni, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wilayani Morogoro, Septemba 18.2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro,
Injinia, Godfrey Mlowe (kulia), baada ya kukagua jengo la kituo cha afya
Mkuyuni, kilichopo katika Wilaya ya Morogoro, Septemba 18.2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na Chifu Kingalu Mwanabanzi wa kumi na tano, Hussein Ally
Machaga (kulia), nje ya jengo la kituo cha afya Mkuyuni, katika Wilaya
ya Morogoro, Septemba 18.2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akikagua ujenzi wa kituo hicho, katika Wilaya ya Morogoro, Septemba
18.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
…………………..
*Amwagiza Mkuu wa Mkoa aungalie vizuri mkoa wake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa wilaya ya Morogoro, Brown
Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo
usimamizi mbovu wa ujenzi wa kituo cha afya Mkuyuni.
Amemsimamisha kazi Mhandisi
huyo leo (Jumatano, Septemba 18, 2019) baada ya kukagua ujenzi wa kituo
hicho cha afya akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani
Morogoro. Amesema hajaridhishwa na aina ya milango iliyotumika.
“Milango yote katika jengo
hili ing’olewe leo leo, huwezi kuweka milango ya hovyo namna hii yaani
mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha kuendelea kukagua jengo.
Yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya hovyo kama hii.”
Waziri Mkuu amesema aina ya
milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya haiwezi kutumika hata
kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na uangalizi mbovu kutoka
kwa watendaji walikubali kuweka milango hiyo mibovu.
Amesema Serikali imeamua
kujenga vituo vya afya vitano kwenye wilaya hiyo ili kusogeza huduma za
afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma
za afya, hivyo amewataka watendaji wasimamie ipasavyo miradi hiyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha
huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao waendelee kuwa
na imani na Serikali yao.
Baada ya kukagua ujenzi wa
kituo hicho cha afya, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa hospitali ya
wilaya, ambako nako ameagiza kuong’olewa kwa mbao zote zilizotumika kwa
ajili ya kupaulia jengo la mama na mtoto la hospitali hiyo kwa kuwa
hazina viwango. “Fundi usiendelee na kazi hii ya upauaji kwa sababu mbao
unazotumia hazikidhi viwango.”
Kwa upande wake, fundi
anayejenga jengo hilo la mama na mtoto, Johnson Ishengoma amesema
changamoto kubwa anayoipata katika ujenzi huo ni ucheleweshwaji wa vifaa
pamoja na kulazimishwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.
Fundi huyo ametolea mfano
suala la mbao za kupaulia kuwa aliomba mbao za urefu wa futi 20 lakini
aliletewa mbao zenye urefu wa futi 12 na kulazimishwa azitumie hivyo
hivyo. “Mhandisi wa wilaya Brown Undule na mtu wa manunuzi Grace ndio
wanaoniletea vifaa hivi. Baadhi ya vifaa huwa navikataa kutokana na
kutokuwa na ubora.”
Katika hatua nyingine,Waziri
Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe kuuangalia
vizuri mkoa wake na kuhakikisha anauchunga vizuri kwa sababu umekithiri
kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Wakati nikiendelea na ziara
mkoani hapa, nimepata taarifa kwamba zaidi ya sh.milioni tisa zimetumika
kwa ajili ya kilipana posho katika Halmashauri ya mji Ifakara . Posho
hizo ni kwa ajili ya ziara ya Waziri Mkuu na imetoka kwa mtendaji wa
kata ya Viwanja 60, hili jambo halikubaliki. Nakukabidhi risiti zote na
uwachukulie hatua wote waliohusika. Mkoa wa Morogoro ni shida”
Wakingumzia kuhusu utendaji wa
Serikali ya Awamu ya Tano na ujenzi wa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika maeneo yao, wakazi wa Tarafa ya Mkuyuni
wameipongeza Serikali kwa namna inavyowajali wananchi wake ikiwa ni
pamoja na kuboresha huduma.
Mmoja wa wananchi hao, Uwesu
Mwichumu (71) mkazi wa kijiji cha Kibungo ameipongeza Serikali kwa
usimamizi wa miradi na hatua inazochukua kwa baadhi ya watendaji
wanaojihusisha na wizi wa fedha za umma.
Amesema Serikali inajitahidi
kuwaletea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao tatizo lililopo ni kwa
watendaji wa chini. “Watendaji wengi huku chini wanashindwa kutekeleza
majuku yao ipasavyo, wanashirikiana na wazabuni kuiibia Serikali.”
Mkazi mwingine wa Tarafa hiyo,
Hanifa Shaban amesema anaishukuru Serikali kwa kuboresha huduma
mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na
zahanati. Amesema awali walikuwa wanakwenda zahanati na kuandikiwa vyeti
bila ya kupewa dawa , hivyo walilazimika kwenda kununua kwenye maduka
ya dawa jambo ambalo kwa sasa halipo.
0 comments:
Post a Comment