Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo wakati
akifungua mkutano wa Wafanyabiashara wa Madini uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo na
baadhi ya Wafanyabiashara wa Madini,. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula.
Sehemu ya Wafanyabiashara wa Madini wakifuatilia mkutano
baina yao, Wizara ya Madini na Taasisi zake.
Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Waziri
wa Madini Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuandaa haraka utaratibu
utakaowawezesha Wafanyabiashara wa Madini nchini kufanya shughuli zao katika
ngazi ya Kanda tofauti na ilivyo sasa ambapo taratibu zinawataka kufanya
shughuli hizo katika Mikoa zilipotolewa leseni zao.
Aliyasema
hayo Septemba 7, 2019 wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao na wizara uliofanyika
jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi
na Wataalam wa wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Aidha,
Waziri Biteko alieleza kuwa, endapo wadau hao watafanya shughuli zao kwa kuzingatia
Sheria na taratibu zilizowekwa, serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea
kutanua wigo kuwawezesha kufanya biashara ya madini katika maeneo mengi zaidi.
Waziri
Biteko alisisitiza kuhusu ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Magufuli ya kutaka rasilimali madini kulinufaisha taifa na watanzania na kueleza kuwa, ndoto hiyo ndiyo iliyopelekea
kufanyika kwa mageuzi mkubwa katika
Sekta ya Madini.
Alikiri
kuwa, kabla ya mabadiliko hakukuwa na mfumo rasmi uliowaonesha wachimbaji kujua
sehemu sahihi ya kuuzia madini yao vivyo hivyo kwa wanunuzi wa madini suala
ambalo lilipelekea kuwepo vitendo vya utoroshaji madini jambo ambalo
lilionekana ni la kawaida.
Waziri Biteko aliwataka wafanyabishara hao kuyatumia
masoko yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini na kusisitiza
kuwa, serikali itaendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini na
kueleza kuwa, waliobainika kufanya vitendo hivyo wataanza kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria na hivyo kuwataka kuwa
chanzo cha mabadiliko ili kuzuia
vitendo vya utoroshaji madini.
‘’
Tumekutana mpaka na wakemia wanaotengeneza madini feki. Kuna wengine wataanza
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunataka chumba cha madini kiwe na hewa ya
kutosha,’’ alisisitiza Biteko.
Akijibu
hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabishara wa Madini ya Vito
(TAMIDA) Sam Mollel, kuhusu changamoto ya ucheleweshaji wa vibali vya
kusafirisha madini nje ya nchi, Waziri Biteko aliwataka kuwa na subira wakati serikali
ikishughulikia suala hilo.
Aidha,
akijibu changamoto ya Masonara kusimamiwa na
wizara nyingine, Waziri Biteko
aliwataka wafayabiashara hao kuwasilisha maoni kuhusu suala hilo kama ilivyofanyika katika kuandaa Kanuni za
Masoko na kuongeza kwamba, ‘’ Tunataka
kuwa wizara ambayo inatatua matatizo’’.
Naye,
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisisitiza kuhusu suala la kulipa kodi
kama inavyowapasa na kuwataka kuyafahamu mabadiliko yaliyofanywa katika sekta
na kuwa sehemu ya mabadiliko hayo.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
Dustan Kitandula, aliipongeza wizara kwa kazi ya kuwalea wadau wa madini na
kueleza kwamba, miaka ya nyuma mambo kwenye sekta hayakuwa yakienda vizuri.
Aidha,
aliwapongeza wafanyabiashara wa madini na kueleza kuwa, hivi sasa wameanza
kubadilika huku tabia ya kufanya biashara ya madini kiholela ikianza kutoweka.
‘’ Sisi
Kamati tunapoona mambo yanakwenda vizuri mnaturahisishia kazi yetu’’, alisisitiza
Mwenyekiti wa Kamati.
Kikao
hicho kimefanyika ikiwa ni jitihada za wizara
za kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini ikiwemo kusikiliza na kutatua changamoto kwenye sekta ili kuwezesha biashara ya madini kufanyika
katika mazingira mazuri yanayoleta tija kwa pande zote.
Aidha,
sambamba na mkutano huo, imefanyika Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya
Nishati na Madini kubwa ikiwa ni serikali kueleza nia yake ya kukifanya Chuo
Cha Madini Dodoma kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akifunga
semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Dustan Kitandula alitaka mchakato wa wa
kukilea Chuo hicho kutochukua muda mrefu na alikitaka kijisimamie chenyewe
ndani ya muda mfupi baada ya kulelewa na
kutoa elimu bora.
Pia,
alitaka kozi ya Mafundi Mchundo kuwekewa msingi mzuri. Pamoja
na hayo, Mwenyekiti wa Kamati aliitaka wizara kukiongezea nguvu Kituo Cha
Jimolojia Tanzania (TGC) ikiwemo bajeti ya kutosha kukiwezesha kuboresha miundombinu
yake.
0 comments:
Post a Comment