Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akisalimiana na Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya
Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini
Dodoma, Septemba 9.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akizungumza na ujumbe kutoka nchini Cuba, ukiongozwa na Naibu Waziri
wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez, kwenye
ukumbi wa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 9.2019. (Picha na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Kwanza wa
Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez ambapo
amewakaribisha Wacuba waje wawekeze kwenye sekta ya kilimo, hususan cha miwa.
Amekutana na
kiongozi huyo leo (Jumatatu, Septemba 9, 2019) ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni
jijini Dodoma. Waziri Mkuu ameishukuruSerikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri
inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kuboresha maendeleo ya jamii.
“Tanzania na
Cuba zina uhusiano wa kihistoria. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati
nchi zote mbili, yaliyokuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya
uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Cuba,
hayati Fidel Castro.”
Waziri Mkuu
amesema Serikali ya Cuba imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa sukari, hivyo
amewakaribisha Wacuba waje nchini washirikiane na Serikali ya Tanzania
katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha
viwanda vya sukari.
Kadhalika, Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na
Serikali ya Cuba kwa kuwa nchi hiyo ni mojawapo
kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania katika masuala ya
kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.
”Mfano katika
sekta ya afya, madaktari wengi kutoka Cuba wamekuwa wakija Tanzania kutibu
wagonja waliokuwa na maradhi makubwa na pia Serikali ya Cuba imekuwa ikitoa
fursa kwa Watanzania kwenda kusomea fani ya udaktari.”
Pia Waziri
Mkuu amewakaribisha Wacuba waje wawekeze katika sekta ya utalii hususani wa
fukwe kwa sababu Tanzania ina fukwe nzuri. Amesema mji mmoja wa Varadero wa
nchini Cuba unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea
kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.
Akizungumzia
kuhusu ofisi ya ubalozi wa Tanzania zilizofunguliwa nchini Cuba, Waziri Mkuu
amesema zimesaidia kurahisisha mawasiliano kwa sababu awali kulikuwa na balozi
mmoja tu ambaye alikuwa akiwakilisha nchi ya Cuba nchini Tanzania.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri
ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez alisema Serikali ya Cuba itahakikisha
uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unakuwa endelevu. Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na
kukuza uchumi.
Kadhalika
kiongozi huyo amesema Serikali ya Cuba imefurahisha na kitendo cha Serikali ya
Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi nchini Cuba kwa sababu imezidi kuimarisha
mahusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili. Kiongozi huyo pia
amefanya ziara Zanzibar kabla ya kuja Dodoma.
0 comments:
Post a Comment