
Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa ili Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi inahitaji
watumishi takribani 7000 wa kada mbalimbali za kiutumishi.
Hayo yamebainishwa Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
(Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Tunza Malapo,
aliyetaka kujua ni watumishi wangapi wanahitajika na TRA ili iweze
kufanya kazi kwa ufanisi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Mamlaka
ya Mapato Tanzania haina upungufu mkubwa kama inavyoelezwa, kwa kuwa
idadi ya watumishi wa TRA walioajiriwa ni 4,751 kati ya 7000
wanaohitajika hivyo kufanya upungufu kuwa asilimia 28 tu.
Alisema jitihada za kukamilisha
idadi ya watumishi wa Mamlaka hiyo kufikia 7000 zinafanywa kwa hatua,
lengo likiwa kuongeza ufanisi wa kiundendaji na kuendelea kuleta matokeo
chanya katika maendeleo ya nchi.
Alifafanua kuwa tangu Serikali ya
Awamu ya Tano imeingia madarakani imejitahidi kwa kiwango kikubwa
kukabiliana na suala hilo, tayari imeajiri watumishi 692 na katika mwaka
wa fedha 2019/20 Mamlaka hiyo imeweka Bajeti ya kuajiri watumishi
takribani 150.
0 comments:
Post a Comment