Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia Mkutano wa Hadhara kwenye uwanja wa Ilula Sokoni wilayani Kilolo, Septemba 27, 2019.
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary
Majaliwa akiwasalimia wananchi katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Uwanja wa Ilula Sokoni wilayani
Kilolo, Septemba 27, 2019. Kulia ni Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto na
wa pili kushoto ni Mwenyekititi wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Abel
Nyamahanga.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaonya baadhi ya Watendaji Kata na askari nchini ambao wamekuwa
wakishindwa kuzifikisha sehemu husika kesi za watu waliowapa ujauzito
wanafunzi na amesema watakaobainika watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Ameyasema hayo jana jioni (Ijumaa,
Septemba 27, 2019) wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika katika uwanja wa Ilula Sokoni, kata ya Nyalumbu wilayani
Kilolo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.
“Wanafunzi bado wanaendelea kupewa
ujauzito na kukatishwa masomo yao huku watu waliohusika na vitendo
hivyo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu baadhi ya
watendaji na askari wamezikalia kesi zao na kushindwa kuwafikisha
polisi.”
“Watoto wa kike lazima walindwe
ili wamalize masomo yao waje kulitumikia Taifa lao. Serikaliimeweka
sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize
masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi.”
Waziri Mkuu alisema watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na adhabu iliyowekwa na Serikali ni kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayemuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amewataka wananchi hususan waishio vijijini wasikubali kurubuniwa na
kugawa ardhi yao kwa watu mbalimbali wanaofika kwenye maeneo yao na
kutaka wauziwe ardhi bila ya kuzihusisha mamlaka husika.
“Eneo lenu hili la Ilula ni zuri
hivyo msikubali kurubuniwa kuuza ardhi yenu kwa sababau inathamani
kubwa. Viongozi wa Kata na Vijiji hakikisheni mnaratibu vizuri na
muandae mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro.”
Waziri Mkuu alisema wananchi hao
wanatakiwa wawe makini na ardhi na mamlaka zinazohusika na ardhi lazima
zihusishwe katika ugawaji wa ardhi kwa sababu wakigawa hovyo
watasababisha vijana wao hapo baadaye wakose maeneo ya kilimo.
Akizungumzia kuhusu uboreshwaji wa
huduma za afya, Waziri Mkuu ameahidi ujenzi wa kituo cha afya katika
kata ya Ilula ili kuwapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu hadi
Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma hizo.
Alisema kituo kitakachojengwa
kitakuwa na chumba cha kujifungulia, chumba cha maabara kwa ajili ya
vipimo mbalimbali, huduma za mama na mtoto, mapasuaji, wodi ya wanaume
na wanawake, aliwataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Waziri Mkuu alisema suala la
kuboresha na kusogeza huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi zikiwemo
za afya limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli ambaye anataka kuona wananchi wakiwa na afya
nzuri ili waweze kushiriki ipasavyo katika shughuli zao za kimaendeleo.
Kabla ya kuhutubia wananchi kwenye
mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa mradi wa maji Ilula
na kuweka jiwe la msingi. Pia, Waziri Mkuu alikagua shughuli za
ukarabati wa chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ilula.
Awali, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege aliwahimiza wananchi hao wajiunge
katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa kupata huduma
za matibabu ya bure wao na familia zao.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally
Happi alisema kuwa awali eneo la Ilula lilikuwa linakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo yam ogogoro ya ardhi ambayo kwa
kushirikiana na watendaji wenzake walifanikiwa kuitatua.
0 comments:
Post a Comment