Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasalimia na Mkuu wa Wilaya ya
Malinyi, Majura Kasika, kwenye jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi,
mkoani Morogoro, Septemba 16.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiweka jiwe la msingi, wa jengo la
Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro, Septemba 16.2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi, la jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro, Septemba 16.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu aelekeza
weledi wao kiutendaji uchunguzwe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu
wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya hiyo Mussa Mnyeti, hivyo kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda
kuchunguza weledi wa utendaji kazi wao.
“Ni aibu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amewateua vijana wawe
viongozi lakini leo hadi wananchi wa kawaida wanajua mgongano wenu maofisini.
Ni aibu Mkuu wa Wilaya ya Mkurugenzi mnagombana tena wakati mwingine
mnagombania miradi, mmesahau kutekeleza majukumu yenu.”
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo (Jumatatu, Septemba 16, 2019)
wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Toboa, akiwa katika siku ya
tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
Amesema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya
wananchi na inapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya jamii kama
kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara lakini wao
wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.
Waziri Mkuu amesema mbali na CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi
na Utawala Bora kwenda kuchunguza utendaji wa viongozi hao, pia ameuelekeza
uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakakague miradi ya ujenzi
inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo kama ubora wake unalingana na thamani
halisi.” Baada ya kupata majibu ya uchunguzi na kubaini kiini cha tatizo ndani
ya wilaya hii hatua zitachukuliwa.”
Awali, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dkt. Haji Mponda alimweleza Waziri Mkuu
kwamba kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya Serikali na
Halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.
Mbunge huyo alisema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo Mkuu wa
Wilaya na Mkurugenzi kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza la
Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivvyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie
katika. Kilipatia ufumbuzi suala hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema
kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara ya viongozi wakuu
kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa Halmashauri hawawatembelei
wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
“Watendaji hamuendi kuwatembelea
wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekana wawe wanawasubiri viongozi wa
juu na kuwasilisha kero zao kwa njia ya mabango, sasa jipangeni haya mabango
yote mtakuja kuyajibu kwa sababu katika mabango yao hakuna hoja hata moja
inayomuhusu Waziri Mkuu zote ni za ngazi ya halmashauri.”
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika
kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila
mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.
Mapema alipowasili wilayani
Malinyi, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi ya
Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa
gharama ya sh. bilioni 3.9. Ujenzi huo ulianza 29/11/ 2017 na utakamilika
29/09/ 2019.
0 comments:
Post a Comment