Na Emmanuel Michael Senny
Uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba na miundo mbinu
katika huduma za kibingwa kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), umeifanya
serikali ya Rais Dk.John Magufuli kuacha alama isiyofutika kwa miongoni kadhaa
ijayo.
Moja ya mambo yanayovuta hisia na hamasa ya
wagonjwa kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yanayohusu
huduma ya mama na mtoto ni uwepo wa vifaa tiba vya kisasa, vitendanishi na
watalaam wabobezi katika idara mbalimbali ikiwamo huduma ya mama na mtoto.
Jana, Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa
Hospitali ya Benjamin Mkapa, Karim Meshack aliieleza timu ya wanahabari
waliofanya ziara ya mafunzo hospitalini hapo kwamba uwekezaji huo ni mkubwa
kufanyika katika utawala wa serikali ya awamu ya tano.
Akitoa taarifa kuhusu uwekezaji huo, Karim
alieleza: “Kumekuwepo na mafanikio chanya katika utoaji huduma na mpaka sasa
imefanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 7 uliofanyika kwa mafanikio makubwa
huduma ambayo awali ilikuwa ikifanyika nje ya nchi.
Zaidi alisema, “Kwa sasa hospitali hiyo ina kitengo
cha wagonjwa wa ajali ambacho ni maalumu kwa majeruhi hasa ikizingatiwa Dodoma
ni mkoa ulio katikati ya nchi kwa hiyo itakuwa rahisi kuhudumia watanzania
kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.”
Kwa mujibu wa sera ya taifa ya afya ya mwaka
1990 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2007, inaeleza kuwa serikali itajielekeza
katika mabadiliko ya magonjwa yanayotokea, sayansi na tekonolojia, kwa kuwa
serikali inatambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi wake kwani afya bora ni
rasilimali muhimu kwa maendeleo.
Serikali inafanya maboresho hayo ili kwenda
sawa na sera hiyo ili kuzingatia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 na
malengo ya milenia.
Pamoja na mambo mengine, serikali inaelezwa
kuwekeza rasilimali watu, fedha na miundo mbinu ya kisasa katika Kitengo cha
Kupandikiza Uroto cha Hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa ili kukabiliana na
ugonjwa wa selimundu.
Mbali na uwekezaji huo, yamo pia matibabu ya
kibingwa ya magonjwa ya moyo ambapo mtaalam mbobezi wa magonjwa hayo, Dk.
Andrew Kasambala alisema kitengo cha moyo kimepanuliwa na kufanyiwa maboresho
makubwa yanayoipa heshima kutokana na shughuli za kibingwa kutoa matokeo
yaliyokuwa yakitarajiwa.
Lucy Baraka aliyemleta mama yake hospitalini
hapo kwa matibabu ya Miguu akitokea wilayani Gairo Mkoani Morogoro na Kayaya
Santa ambao walifika hospitalini hapo kwaajiri ya matibabu wamesifu huduma
zinazotolewa hospitalini hapo huku akiiomba Serikali kuboresha huduma katika
maeneo mengi zaidi ili kuweza kupata matibabu ya uhakika kwa ukaribu zaidi.
Hospitali hiyo iliyopo kilomita 25 kutoka
katika viunga vya Jiji la Dodoma, inafanya upasuaji wa matundu unaotumia vifaa
vya kisasa.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment