
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo akiwa katika
ziara ya kikazi mkoani Iringa, Septemba 27, 2019


Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Kilolo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Iringa, Septemba 27,
2019. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happy na kulia ni
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Abel Nyamahanga


Baadhi ya watumishi wa wilaya ya Kilolo wakimsikiliza Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao, Septemba 27, 2019.
\Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
…………….
…………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi afuatilie utendaji kazi
kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo kufuatia watumishi 14 wa ofisi
hiyo wakiwemo madereva 10 kuhamishwa baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo Asia
Abdallah kudai kuwa hawafanyi kazi ipasavyo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ni
mhuimu kwa viongozi wakatambua dhamana zao katika utekelezaji wa
shughuli zao pamoja na kuwatambua, kuwajali na kuwathamini watumishi wa
kada zote wakiwemo madereva, hivyo ni vizuri wawaandae kwa kuwapa
maelekezo kwa wakati kwa kuwa nao ni binadamu na wanafamilia.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Ijumaa, Septemba 27, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya
Kilolo, Halmashauri ya wilaya ya Kilolo pamoja na Madiwani wa
Halmashauri hiyo akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani
Iringa. Amesisitiza umuhimu wa watumishi hao kushirikiana.
Waziri Mkuu amesema pamoja na
shughuli za maendeleo wanazofanya katika wilaya hiyo lakini hawana
mshikamano, hivyo amemtaka Mkuu wa Wilaya ahakikishe anashirikiana
vizuri na wenzake kwa sababu watumishi wengi wamehamishwa tangu aingie
katika ofisi hiyo na hata wanaoletwa wanalalamika na wanaomba
wahamishwe.
Amesema watumishi wengi katika
ofisi hiyo anawaona hawana uwezo wakiwemo wasaidizi wake kama madereva,
watunza kumbukumbu na makatibu muhtasi. “Hata aliyekuwa Katibu Tawala wa
wilaya hii alihamishwa kwa sababu na kutoelewana na DC, na hata huyu
Katibu Tawala wa Wilaya aliyepo sasa hana raha anataka kuhama kwa sababu
hizo hizo.”
“Lazima tuwatambue wasaidizi wetu
na majukumu yao. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi, lazima
kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya.
Hapa tujue mbovu ni nani Mkuu wa Mkoa tunataka tujue DC wako anataka
dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai?
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “ili
mfanye kazi vizuri mnatakiwa mshikamane mfanye kazi kama timu moja kwani
pamoja na shughuli mnazofanya hamna ushirikiano. DC (mkuu wa wilaya)
sasa utabaki peke yako utakuwa unaandika mwenyewe, unaendesha gari
mwenyewe maana wote hawafai. Mkuu Mkoa nakukabidhi majina ya watumishi
hao ushughulikie suala hili. Na Katibu Tawala wa Mkoa usilete watumishi
wengine hapa mpaka suala hili litakapopatiwa ufumbuzi”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
ameziagiza halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga kiasi cha
fedha katika makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa
miradi ya kimkakati kwenye maeneo yao kama ujenzi wa vituo vya afya,
barabara za halmashauri na masoko badala ya kutegemea fedha kutoka
Serikali Kuu pekee.
Amesema wilaya ya Kilolo ambayo
haina kituo cha mabasi inatakiwa itenge fedha kutoka kwenye makusanyo
yao na kuanzisha mradi wa kituo hicho ambao utekelezaji wake utaboresha
huduma kwa wananchi pia, mradi huo utasaidia katika kuongeza mapato ya
halmashauri. Halmashauri ya wilaya ya Kilolo inakusanya sh. bilioni nne
kwa mwaka.
Waziri Mkuu amesema watumishi
wanapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani wananchi wanahitaji
waone matokeo ya uwepo wao kutokana na dhamana waliyotewa na Serikali
katika wilaya hiyo. “Madiwani nanyi simamieni halmashauri yenu vizuri
kwa sababu nyie ndiyo wenye dhamana ya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa
vizuri.”
Awali, Mbunge wa jimbo la Kilolo,
Venance Mwamoto aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika wilaya yao ikiwemo ya umeme, ambapo kati
ya vijiji 94 vilivyoko vijiji 54 vimeunganishiwa huduma hiyo na
vilivyosalia vitakuwa viunganishiwa umeme ifikapo Desemba mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu miradi ya maji
mbunge huyo alisema kati ya vijiji 94 vya wilaya hiyo vijiji 15 tu ndio
bado havina maji ya uhakika lakini wanaendelea na mchakato wa
ufuatiliaji ili kuhakikisha navyo vipata maji safi na salama.”Kuhusu
sekta ya elimu tatizo tulilonalo ni madai ya walimu waliohama na
waliopandishwa madaraja.” Waziri Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa
kazi.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua mradi
wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kupokea taarifa ya ujenzi wa
hospitali hiyo ambapo alisema ameridhishwa na ujenzi huo uliogharimu sh.
bilioni nne na alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa wilaya hiyo
akiwemo Mkurugenzi pamoja na mkandarasi anayenga.
0 comments:
Post a Comment