METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 11, 2019

Mkandarasi Mradi wa umeme Mtera atakiwa kumaliza kazi Oktoba, 2019

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tatu kutoka kulia) akikagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mtera.Wengine katika picha ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kituo cha kupoza umeme cha Mtera ambacho kinafanyiwa upanuzi ili kuweza kuhudumia Vijiji takribani 70 katika mkoa wa Iringa na Dodoma.


Teresia Mhagama na Hafsa Omar

Mkandarasi anayetekeleza mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mtera, ameagizwa kumaliza kazi hiyo ifikapo tarehe 4 Oktoba mwaka huu ili kuwezesha vijiji takribani 70 katika mkoa wa Iringa na Dodoma kupata umeme wa uhakika kwani sasa wanapata umeme wenye nguvu dogo.

Maagizo hayo yalitolewa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 10 Septemba, 2019 mara baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika kituo hicho na kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi, kampuni ya SUNIR kutoka Iran.

“Mwaka 2017, Novemba tulimpa mkandarasi huyu kazi ambayo alipaswa kumaliza  ndani ya miezi 18 lakini hajafanya kazi vizuri na kazi zinazofanyika hapa haziendani na hatua ambayo ilibidi ifikiwe kwa sasa.” Alisema Dkt Kalemani.

Aidha, baada ya kufika kwenye eneo la mradi huo, Dkt Kalemani alikuta vibarua wanne tu wapo kazini na mkandarasi wa kampuni hiyo kutoka nchini Iran hakuwepo eneo la kazi, hivyo alimuagiza msimamizi wa mradi huo kutoka TANESCO kuhakikisha kuwa mkandarasi huyo anaongeza vibarua.

Vilevile aliagiza kuwa, Mkandarasi huyo kutoka Iran ahakikishe anafika nchini ndani ya siku tatu ili kuweza kuchukua hatua zitakazowesha mradi huo kutekelezwa kwa kasi.

Alisema kuwa,  kituo hicho kitafungwa transfoma mbili zenye uwezo wa 10MVA kila moja na fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo ni Dola za Marekani milioni 3.2.

“Transfoma hizi kwa sasa bado zipo bandarini lakini natoa maelekezo kwa TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuhakikisha kuwa transfoma hizo zinatolewa bandarini ndani ya siku Tano ili zifungwe na ziweze kufanya kazi.”Alisema Dkt Kalemani.

Alieleza kuwa, awali Kituo cha kupoza umeme cha Mtera kilijengwa kwa ajili ya kuhudumia eneo hilo lenye mitambo ya kuzalisha umeme pekee lakini Serikali iliamua kukipanua kituo hicho ili kuweza kuhudumia pia maeneo na Vijiji vya jirani.

Katika ukaguzi huo wa kushtukiza, Waziri wa Nishati, aliambatana na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com