MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiraia ijulikanayo Kama Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja amemshauri aliyewahi kuwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa katika serikali ya awamu ya nne Benard Membe afuate nyayo za Waziri mkuu mstaafu Mhe. Edward Ngoyai Lowassa kuiga mfano wake wa kuwa na ustaarabu na uungwana wa kisiasa na akubali yaishe.
Mwenyekiti huyo wa Taasisi hiyo inayoshughulika na masuala ya haki, Demokrasia na utawala bora, Mgeja amesema Membe amekuwa akitoa matamko mbalimbali yaliyojaa ukakasi, maudhi, dharau, kiburi, kejeli, vijembe pamoja na kujiamini kulikopitiliza na kuongeza kuwa amekuwa akimfuatilia mara kwa mara kauli zake anazozitoa kupitia vyombo vya Habari pamoja na mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Tweeter hivyo anapaswa kuheshimu Mamlaka ya Serikali.
Mgeja amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Nyanhembe Kata ya Kilago Halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga ambapo amezungumzia kauli tata za mara kwa mara za mwanachama wa CCM Benard Membe alizozitoa hivi karibuni nakudai kuwa kauli hizo zimekosa uadilifu ndani ya chama na serikali pamoja na utu na heshima kwa mtu aliyejaa imani za dini.
Aidha,mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Mzalendo Foundation , ambaye pia Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mgeja ametolea mfano wa kauli tata zilizojaa ukakasi alizotoa hivi karibuni Waziri huyo wa zamani katika serikali ya awamu ya nne Membe kuwa “BORA UFE UMESIMAMA KULIKO KUISHI UMEPIGA MAGOTI HAYUKO TAYARI KUOMBA RADHI”.
Mgeja amesema Membe amekuwa Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifana kupata hadhi ya kuwa mwanadiplomasia lakini kauli anazozitoa hazilingani na hadhi yake kama mwanadiplomasia wala mtu aliyeishi na imani ya dini utu na uungwana.
“Mfano wanadiplomasia kama Membe wote Duniani hupenda kufanya kazi za kupigania maridhiano na mapatanisho na pale wanapokoseana huwahi kuombana radhi inasikitisha kuona matendo na kauli anazoto marakwa mara Membe inawezekana kabisa hakuiva vizuri katika masuala ya Diplomasia,” alisema mwenyekiti wa Mzalendo Foundation Khamis Mgeja huku alitolea mfano.
Mgeja ameendelea kusema kuwa kauli nyingine tata ya Membe kama mwanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia mtandao wake Tweter amediriki kusema kuwa CCM imekatika vipande na kama kanga haiwezi tena kushoneka.
Pia Mgeja amewaambia waandishi wa habari kuwa Membe kama mwanachama hai wa CCM hakustahili kabisa kutoa maneno hayo labda awe rangi mbili aliyejificha kwa kimvuli cha CCM na kauli hizo zinamvunjia heshima na uadilifu mbele ya chama chake na kumuondolea hadhi na heshima ya mwanadiplomasia na kugeuka hivi sasa kuwa mwanaharakati.
Sanjari na hayo Mgeja amewataka Watanzania Kuunga mkono Juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Wa Awamu ya Tano Dokta.John Pombe Magufuli.
0 comments:
Post a Comment