
Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe.
Shanif Mansoor (CCM) (katikati) akinawa mikono wakati wa sherehe za
kupokea mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji, Wilaya ya
Kwimba, Mkoani Mwanza. Kulia ni Diwani wa Kata ya Kikubiji, Alfred
Luteja.

Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe.
Shanif Mansoor (CCM) (katikati) akinywa maji ya Mradi wa Kijiji cha
Shilima wakati wa sherehe za kupokea mradi huo.

Wananchi wa Shilima wakijipatia
huduma ya maji kutoka kwenye mradi uliyozinduliwa hivi karibuni ambao
unatoa maji kutoka Ziwa Victoria.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha
Shilima na vijiji vya jirani wakimsikiliza Mbunge wao Shanif Mansoor
(hayupo pichani) wakati wa sherehe za kuupokea mradi wa maji wa
Shilima.
***********************
Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe.
Shanif Mansoor (CCM) ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa
kukamilisha mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji Wilaya
ya Kwimba, Mkoani Mwanza.
Ametoa pongezi hizo jana
alipojumuika na wapiga kura wake wa Kijiji cha Shilima kusherehekea
kukamilika kwa mradi huo ambao ulipaswa kukamilika tangu mwaka 2013
lakini kutokana na udhaifu wa Mkandarasi haukuweza kukamilika kwa
wakati.
Alisema Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni ya vitendo, ikiahidi
inatimiza kwani ameshuhudia miradi mingi ikitekelezwa kwa ufanisi na kwa
wakati na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni kama ndoto ambayo
wananchi wake wamekuwa hawana uhakika wa lini itatokea hasa ikizingatiwa
kwamba kero ya maji kwa wananchi hao ilikuwa ni kubwa.
Akizungumzia historia ya mradi
huo, Mhe. Mansoor alisema ulianza kutekelezwa mwaka 2013 lakini
Mkandarasi alikua akisuasua na baada ya Waziri kufika kwenye eneo hilo
alifanikisha kuvunja mkataba na kazi ya ujenzi wa mradi huo kukabidhiwa
rasmi kwa MWAUWASA. “Namshukuru sana Profesa Mbarawa, alifika hapa na
kujionea hali halisi na hatimaye alifanikiwa kusitisha mkataba na
Mkandarasi na kukabidhi rasmi ujenzi wa mradi kwa MWAUWASA,” alisema.
Mhe. Mansoor alitoa shukrani
zake kwa Serikali kwa niaba ya wananchi wa Shilima ambapo alielezea adha
waliyokuwa wakiipata kabla ya kukamilika kwa mradi huo, alisema
shughuli nyingi za kimaendeleo zilisuasua kutokana na kukosekana huduma
ya maji ya uhakika kwani wananchi walitumia muda mwingi kufuata maji
umbali mrefu na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu shughuli nyingine
za maendeleo.
“Kwa niaba ya wananchi wa
Shilima naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, Waziri Mkuu alifika
hapa na baadaye Waziri wa maji, waliahidi na wametimiza,” alisema Mhe.
Mansoor.
Kwa upande mwingine Mhe.
Mansoor aliipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini
Mwanza (MWAUWASA) chini ya aliyekuwa Mkurugenzi wake, Mhandisi Anthony
Sanga ambaye sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kukamilisha
mradi huo kwa wakati kama ilivyokuwa imeagizwa na Waziri wa Maji,
Profesa Makame Mbarawa. “Kwakweli MWAUWASA inafanya kazi kubwa na nzuri
sana, kwa kipekee nampongeza sana Mhandisi Sanga kwa kuusimamia mradi
huu kwa weledi mkubwa na sasa umekamilika,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya
Kikubiji, Alfred Luteja aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kupitia
Wizara ya Maji ambayo ilielekeza mradi huo ukamilishwe na MWAUWASA.
“Serikali yetu ni sikivu, tumeieleza na imesikia na imefanyia kazi kilio
chetu, hatimaye sasa tunatumia maji kutoka Ziwa Victoria,” alisema
Luteja.
Mradi wa Shilima ulizinduliwa
rasmi na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa Septemba 14, 2019 ikiwa
ni utekelezaji wa Sera ya Maji pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
inayoelekeza kuwapatia huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85
wakazi wote waishio vijijini ifikapo mwaka 2020.
0 comments:
Post a Comment