
Mtaalam kutoka Taasisi ya
Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na
Gesi Asilia (TEITI) Erick Ketagory (kushoto) akielezea majukumu ya TEITI
kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri (kulia) kwenye Banda la Wizara
ya Madini katika Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Madini
yaliyofanyika mjini Geita tarehe 22 Septemba, 2019

Mhandisi Migodi wa Wizara ya
Madini, Johnbosco Karungamye (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) alipotembelea banda hilo katika Maonesho
ya Teknolojia na Uwekezaji katika Madini yaliyofanyika mjini Geita
tarehe 22 Septemba, 2019

Waziri wa Madini, Doto Biteko
akitoa hotuba kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia
na Uwekezaji katika Madini yaliyofanyika mjini Geita tarehe 22
Septemba, 2019.

Kutoka kushoto Waziri wa Nishati,
Dkt. Medard Kalemani, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhandisi Robert Gabriel wakiwa katika picha ya pamoja na
watendaji wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini mara baada ya kumalizika
kwa ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Madini
yaliyofanyika mjini Geita tarehe 22 Septemba, 2019.

Kutoka kushoto Waziri wa Nishati,
Dkt. Medard Kalemani, Waziri wa Madini, Doto Biteko, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhandisi Robert Gabriel wakiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa
mikoa na wilaya waliohudhuria ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia na
Uwekezaji katika Madini yaliyofanyika mjini Geita tarehe 22 Septemba,
2019.

Wakazi wa mjini Geita wakisikiliza
hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) kwenye ufunguzi wa maonesho
hayo

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa mjini Geita
katika uzinduzi huo (hawapo pichani)
…………………..
Asteria Muhozya na Greyson Mwase, Geita
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Septemba 22, 2019 amefungua Maonesho
ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yaliyoanza tarehe 20
Septemba, 2019 na kutarajiwa kumalizika tarehe 29 Septemba, 2019.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
maonesho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pongezi kwa Wizara ya Madini
na Tume ya Madini kwa kuboresha shughuli za madini kupitia kuongeza
ajira na vitendea kazi kama vile magari kama njia mojawapo ya kuboresha
ukusanyaji wa maduhuli.
Akielezea mafanikio ya Soko la
Madini Geita tangu kuanzishwa kwake Majaliwa amesema kuwa ni pamoja na
kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu kutoka takribani kilo 100 hadi kilo
200 na zaidi kwa mwezi na kusisitiza kuwa, tangu kuanzishwa kwa soko la
madini la Geita kiasi cha kilo 1,573 zimezalishwa na kuuzwa.
Katika hatua nyingine, ameitaka
Tume ya Madini kuongeza kasi kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili Sekta ya
Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi .
Aidha, amewataka wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini kuyatumia vyema masoko ya madini
yaliyoanzishwa nchini na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha
yanalindwa.
Pia, amewataka wachimbaji wa
madini kutumia tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini (GST) kubaini maeneo yanye madini na kuanza kuchimba ili kuepuka
uchimbaji wa kubahatisha.
Amesema serikali itaendelea
kuboresha Sheria na Kanuni ili kuleta tija zaidi na hivyo kuwataka
wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini ikiwemo
kutoa taarifa kwenye vyombo vya udhibiti.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuachana na matumizi ya
zebaki na badala yake watumie njia nyingine mbadala kulingana na
miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Madini pamoja na Tume ya
Madini.
Akizungumzia nafasi ya sekta
ya madini katika kuchochea ukuaji wa viwanda, Waziri wa Madini Doto
Biteko amesema kwamba hadi sasa wizara kupitia Tume ya Madini
imekwishatoa leseni mbili za usafishaji wa madini (Refinery Licence)
moja ikiwa mkoani Dodoma na nyingine mkoani Geita
Ameongeza kuwa, Wizara ya Madini
kupitia Tume ya Madini imetoa leseni nne za uyeyushaji wa madini ya
Shaba na Bati ( Smelting Licence )
Kuhusu changamoto ya usafirishaji
nje madini ya bati amesema Wizara kwa kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za
Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) zipo katika hatua ya mwisho kuwezesha
upatikanaji wa Hati ya kusafirisha madini ya bati nje ya nchi na
kuongeza kwamba, hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu, hati hiyo
itakuwa tayari.
Akizungumzia uanzishwaji wa masoko
ya madini, Waziri Biteko amesema masoko hayo yameleta matokeo chanya
huku nidhamu ya watanzania kusimamia masoko na rasilimali ikiwa
imeongezeka hali ambayo imepelekea baadhi ya nchi zikiwemo za Kongo,
Zambia na Msumbiji kutaka kuyatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa
katika mikoa mbalimbali nchini.
‘’ Wanaotaka kuhujumu masoko
waache. Ukifanya hivyo utaambulia vitu viwili tu, kufilisiwa na kufungwa
jela,’’ amesisitiza Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteko amebainisha
kuwa, wadau wa madini nchini hawakatazwi kuingiza madini nchini kutoka
nchi mbalimbali zikiwemo sampuli isipokuwa tu madini yote yanayopelekwa
nje ya nchi ni lazima yazingatie sheria na taratibu.
Katika hatua nyingine, Waziri
Biteko ameupongeza Mkoa wa Geita kwa kuwa kinara kwenye usimamizi wa
fedha zinazotokana na mpango wa utoaji wa huduma kwa wananchi
wanaozunguka kampuni za madini (CSR) na kuzitaka kuendelea kufuata
sheria na taratibu zinazowekwa na serikali kwenye usimamizi wa sekta ya
madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa soko
la madini mkoani humo, madini ya dhahabu yameanza kupatikana kwa wingi
na kueleza kwamba kwa mwezi Agosti mwaka huu jumla ya kilo 504 zimeuzwa
sokoni hapo, na kabla ya kuisha kwa mwezi Septemba tayari kilo 340
zimeuzwa sokoni.
Akizungumzia lengo la maonesho
hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Chacha Wambura amesema kuwa ni
pamoja na kukuza teknolojia ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo
na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa wa Geita.
Katika hatua nyingine ikiwa ni
sehemu ya ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amezindua mwongozo wa uwekezaji katika mkoa huo.
Maonesho hayo yemehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa jirani na Geita,
Viongozi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Wawakilishi wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Taasisi za Kifedha, wadau
mbalimbali wa madini na wananchi.
Kaulimbiu ya maonesho hayo
‘’Madini ni Chachu ya Ukuaji wa uchumi wa Viwanda. Tuwekeze kwenye
Teknolojia bora ya Uzalishaji na Tuyatumie Masoko ya Madini’’
0 comments:
Post a Comment