******************
TAASISI ya Association of African
Economy and Development in Japan (AFRECO) imeahidi kuipatia Hospitali ya
Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma basi ambalo ni hospitali kamili
litakalotoa huduma za matibabu kwa Manispaa ya Dodoma, Mikoa na Wilaya
zinazoizunguka Mkoa wa Dodoma.
Basi hilo litakapowasili
nchini kutoka Japan linatarajiwa kuwa ni mkombozi kwa wananchi waishio
vijijini na katika maeneo ambayo hayana hospitali kwani kila
litakakokwenda kutoa huduma litakuwa na madaktari waliobobea katika
utaalamu wa tiba mbalimbali, vifaa tiba, maabara pamoja na dawa.
Hayo yamebainishwa leo
(Jumapili, Septemba 1, 2019) na Rais wa AFRECO, Bw. Tetsuro Yano
katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyofanyika
kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan.
Bw. Yano amesema wameamua
kuanza kutoa misaada na huduma zao nchini Tanzania baada ya kufurahishwa
na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Ameongeza kuwa anaamini siku
moja Tanzania itakuwa nchi ya mfano kwa Afrika Mashariki na Afrika yote
kwa kutoa huduma bora za tiba kwani itakuwa na vituo vingi vya Afya na
hospitali zenye uwezo wa kutibu magonjwa kama vile ya moyo na figo.
Hata hivyo tayari wagonjwa toka nchi jirani wameanza kuja kutibiwa
nchini.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu
amesema mbali na kutoa basi ambalo litakuwa linatoa huduma za matibabu,
pia taasisi hiyo ya AFRECO itasaidia katika kupandisha hadhi hospitali
ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa Shule kamili ya tiba.
Amesema hospitali hiyo ya
Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma itapatiwa vifaa mbalimbali vya
tiba ambavyo vitaifanya hospitali hiyo kuwa ni shule bobezi kwa
utoaji wa tiba mbalimbali nchini Tanzania na Barani Afrika.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
kuwa wamekubaliana na AFRECO kuanzisha kitivo maalum cha Uhandisi wa
Vifaa Tiba ambacho kitafundisha uhandisi wa vifaa tiba ili nchi yetu iwe
na watalaamu wa kukarabati vifaa tiba pindi vinapoharibika badala
kuvipeleka nje ya nchi au kuagiza wahandisi na watalaamu kutoka nje ya
nchi kuja kuvitengeneza.
“Hivi sasa yanafanyika
makubaliano ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba na kwa
kuanzia wataanza kutengeneza maji ya drip ambayo huongezwa kwa wagonjwa
kwa maeelekezo ya madaktari na baadae watengeneza dawa mbalimbali.”
Naye,Naibu Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Dodoma, Mipango, Utawala na Fedha, Profesa Donald Mpanduji
amesema wametia saini hati ya makubaliano kati ya AFRECO na Chuo Kikuu
cha Dodoma ambayo yanalenga kuboresha hospitali ya Chuo Kikuu cha
Dodoma.
Awali, Dkt. Omary Ubuguyu
kutoka Wizara ya Afya amesema maboresho yaliyofanywa na Serikali ya
Awamu ya Tano katika huduma za tiba yameiwezesha Tanzania kupunguza
wagonjwa wanaopelekwa nchi za nje kwa matibabu kutoka 800 hadi
42 ambalo ni punguzo la asilimia inayotajwa kuwa 200.
Amesema hatua hiyo imeongeza
nafasi kwa watalaamu wetu wa tiba kujifunza zaidi pamoja na kuwapunguzia
wananchi gharama za kusafiri kwenda nje ya nchi kutafuta tiba na pia
imeipunguzia Serikali gharama ya fedha za kigeni ambazo zingetumika
kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.
0 comments:
Post a Comment