Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,anaye maliza muda wake hapa
Nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez .kwa ajili ya kumuaga Waziri Mkuu
ofisini kwake .Magogoni jijini Dar es Salaam.leo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akutana na Balozi wa Afrika Kusini, Thamasanqa Dennis Mseleku kwa
ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini
Tanzania. amekutana naye ofisini kwake .Magogoni jijini Dar es
Salaam.leo Agosti 21.2019
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
……………..
UMOJA wa Mataifa (UN) umeipongeza
Serikali ya Tanzania kwa namna inavyotumia vizuri rasilimali zake za
ndani na hivyo kuiwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo
sambamba na kupunguza utegemezi kutoka nje.
Pongezi hizo zimetolewa leo
(Jumatano, Agosti 21, 2019) na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,
Bw. Alvaro Rodriguez alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Mratibu huyo Mkazi wa Umoja wa
Mataifa ambaye alikwenda kumuaga Waziri Mkuu, amesema kuwa Tanzania
imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa kuimarisha
miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na vituo vya
afya.
“Katika kipindi changu cha miaka
mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania, nimeshuhudia mabadiliko makubwa
ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano
kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa na taasisi zake nchini.”
Katika hatua nyingine, Bw.
Rodriguez ameisifu Serikali ya Tanzania kwa namna ilivyoweza kuandaa na
kuendesha vizuri mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Agosti 17 na 18 mwaka
huu.
Mbali na kuisifu Serikali pia
kiongozi huyo amevipongeza vyombo vya habari kwa jinsi vilivyoshirikiana
na Serikali kuripoti matukio mbalimbali ya mkutano huo. “Nawapongeza na
wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa Serikali wakati wote wa mkutano
wa SADC.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu
amemshukuru kiongozi kwa pongezi alizozitoa ambazo ni ishara kwamba
anatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika kutumia vizuri rasimali
zake.
Waziri Mkuu amesema “maelezo
yaliyotolewa na Bw. Rodriguez yanaakisi kauli za Mheshimiwa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli kwamba Tanzania si nchi masikini na inayo uwezo wa
kutoa misaada kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo. Watanzania
waendelee kuiunga mkono Serikali yao.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kumpongeza kiongozi huyo kwani alikuwa kiungo kizuri kabaina ya
Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa. Pia atakumbukwa sana kutokana
na mambo mengi aliyoyafanya kipindi cha utumishi wake nchini Tanzania.
Awali, Waziri Mkuu alikutana na
kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Balozi
Thamasanqa Dennis Mseleku ambaye alikwenda kwa ajili ya kumuaga baada ya
kumaliza muda wake wa kufanya kazi nchini Tanzania.
Waziri Mkuu alimpongeza Balozi
huyo kwa ushirikiano na mchango alioutoa kwa Serikali ya Tanzania katika
shughuli mbalimbali za kimaendeleo zikiwemo za kiuchumi, elimu, afya,
maendeleo ya jamii pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya nchini mbili
hizo.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi
Mseleku ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa
uliompatia katika kipindi chake cha utumishi akiwa nchini na kwamba
alitamani aendelee kubaki Tanzania.
0 comments:
Post a Comment