Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na
Biashara Mhe. Mhandisi Stella Manyanya akisikiliza maelezo kuhusu
majukumu ya Wakala wa Vipimo katika uhakiki wa mizani ya kupimia vito na
madini
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga
Mpina akisikiliza majukumu ya Wakala wa Vipimo alipotembelea banda letu
katika maonesho ya nanenane Simiyu
Elimu ya matumizi ya vipimo sahihi kwa wanafunzi katika maonesho ya nanenane Simiyu
Wananchi wakipewa elimu kuhusu utambuzi wa dira za maji zilizohakikiwa na Wakala wa Vipimo
Mkurugenzi wa Ufundi Bi. Stella Kahwa akitoa elimu kwa Wakulima waliotembelea banda letu wakati wa maonesho ya nanenane Simiyu
………………………….
Wakala wa Vipimo (WMA) inaendelea kutoa
elimu ya matumizi ya vipimo sahihi kwa wananchi wote wa Simiyu na Mikoa
ya karibu katika maonesho ya sherehe za Wakulima (Nanenane) ambayo
yanafanyika katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu.
Lengo kubwa la Wakala wa Vipimo kushiriki
katika maonesho haya ni kusogeza huduma karibu kwa wananchi na kuwapa
elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo pamoja na majukumu yetu kwa
ujumla katika sekta za Kilimo, Biashara, Afya, Madini na Usafirishaji.
Akizungumza na mwandishi wetu, Bi. Stella
Kahwa ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi Wakala wa Vipimo, amesema Wananchi
wanapotembelea banda letu katika maonesho ya nanenane, wanapata fursa
ya kujifunza namna sahihi za kufungasha bidhaa za wajasiriamali kwa
kutumia vipimo sahihi na kuandika alama kwa usahihi katika kifungashio
kwa lengo la kuongeza thamani za bidhaa wanazozalisha. Pia, kwakuwa
mikoa ya kanda ya ziwa Wakulima bado wanaendelea na zoezi la kuuza
pamba, katika banda letu tutakuwa tunatoa elimu ya utambuzi wa mizani
sahihi iliyohakikiwa na iliyoidhinishwa kutumika katika zoezi la ununuzi
wa zao la pamba katika vyama vya msingi.
Bi. Stella Kahwa ameendelea kusema, kwa
sasa Wakala wa Vipimo inafanya uhakiki wa Dira za maji hivyo wananchi
watapata nafasi ya kujifunza namna ya uhakiki unavyofanyika katika dira
za maji na namna ya kutambua dira ambazo zimehakikiwa na kufungwa lakiri
ya Wakala wa Vipimo ili kuhakikisha kunakuwa na biashara ya haki ambapo
mamlaka za maji zinatoza fedha kwa usahihi kulingana na matumizi ya
wateja wao.
Hivi sasa Serikali inafanya jitihada za
kuanzisha masoko ya madini katika kila mkoa ili kuhakikisha kuwa madini
yetu hayatoroshwi na yanauzika kwa urahisi, wananchi watakapo tembelea
banda letu watapata kufahamu mchango wetu katika sekta ya madini ambapo
tunafanya uhakiki wa mizani zinazotumika kwa kutumia vigezo vya kisasa
na kuweka alama zetu ambazo ni lakiri na stika ili kuilinda isiweze
kuchezewa na kuweka haki katika biashara inayofanyika ili muuzaji na
mnunuzi waweze kunufaika kwa kuhakikisha haki inatendeka katika wafanya
biashara hao.
Bi. Stella Kahwa amewataka
wafanyabiashara kufanya kazi zao kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria
na taratibu zilizowekwa kwani adhabu zitolewazo kwa wakiukaji wa Sheria
ya vipimo ni kali. Kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Vipimo sura na. 340 na
mapitio yake ya mwaka 2002, endapo mfanya biashara atabainika kutenda
kosa kinyume na Sheria hiyo na akakiri kutenda kosa husika, atapaswa
kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi
milioni ishirini (20,000,000/=) kwa kosa la kwanza kulingana na idadi ya
makosa aliyotenda. Na endapo mtuhumiwa atakataa na kufikishwa
mahakamani kwa kosa la kwanza atatozwa faini isiyopungua Shillingi
300,000/= na isiyozidi shilingi millioni 50 au kifungo kisichozidi miaka
miwili (2) au vyote kwa pamoja. Aidha endapo mtuhumiwa atakamatwa na
kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa Mahakamani akakutwa na
hatia adhabu ni faini isiyopungua Shillingi 500,000/= na isiyozidi
shilingi millioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote
kwa pamoja.
Kwa kumalizia Bi. Stella amewataka
wananchi kutokuwa waoga wa kutoa taarifa zitakazo wafichua wale wote
wanaojihusisha na uchezeaji/ uharibifu wa vipimo katika sekta mbalimbali
kwa lengo la /kuwapunja/kuwaibia wanunuzi/wauzaji wa bidhaa mbalimbali.
Taarifa hizi zitolewe kwa kupitia ofisi zetu zilizopo katika mikoa yote
ya Tanzania Bara au kupitia namba yetu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97
ili hatua kali ziweze kuchukuliwa dhidi ya wachezeaji/waharibifu wa
vipimo.
0 comments:
Post a Comment