METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 26, 2016

CHAMA CHA MAPINDUZI ZANZIBA CHATOA MASHARTI ILI KUZUNGUMZA NA CUF


Na Masanja Mabula –Pemba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Visiwani Zanzibar kimetoa masharti matatu iwapo chama Cha wananchi CUF kitayatekeleza kinaweza kulitafakari ombi la chama hicho la kutaka kukaa kwenye meza ya mazungumzo .

Kimesema masharti hayo iwapo yatatekelezwa CCM wanaweza kukaa meza ya mazungumzo na CUF lakini si kwa ajili ya kuunda serikali ya mpito , bali ni kwa ajili ya ushirikiano wa kutekeleza ilani ya uchaguzi na kuwaletea maendeleo wananchi.

Masharti hayo ni kumtaka Katibu Mkuu wa CUF kutangaza hadharani kuitambua Serikali ya Mapinduzi inayoongozwa na Rais Dk Ali Mohammed Shein na pia wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakiongoza migomo kuomba radhi wananchi walioathirika na mgomo huo .

Akizungumza na wanaCCM wa Jimbo la Kojani , Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema sharti jengine ni wafuasi wa CUF waliowahi kuhujumu mali za wananchi kwenda na kuwaomba radhi wahusika walioharibiwa mali na vitu vyao .

“Tunaweza kufikiria uwezekano wa kukaa meza ya CUF , ili kushirikiana kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 na sio kuunda serikali ya mpito iwapo masharti hayo yatatekelezwa ”alifahamisha.

Aidha Naibu Katibu alieleza kuwa CCM pamoja na Serikali zake hakina chuki na chama cha Siasa wala wafuasi wao , na kitaendelea kuwapatia huduma muhimu wa kijamii popote walipo na bila ya ubaguzi .

Aliongeza kuwa suala la kuunda Serikali ya mpito Zanzibar haliwekani kwani CCM baada ya kupata ushindi katika uchaguzi Mkuu wa Marejeo iliunda serikali ambayo imezingatia pia matakwa ya kikatiba kwa kujumuisha vyama vya siasa .

Alisema kinachooneka kwa Viongozi na wachama wa CUF kuomba mazungumzo na CCM ni kujutia maamuzi waliyoyafanya ya kugoma kushiriki uchaguzi mkuu wa marejeo baada ya Tume ya Uchaguzi ZEC kufuta uchaguzi wa Oktoba mwaka 2015.

Sambamba na hayo Naibu Katibu Pia alisema CCM inaheshimu sheria na hata Serikali iliyoundwa imefuata taratibu zote kwa mujibu wa katiba ya nchi , kwani hata nafasi ya Makamo wa kwanza imebaki wazi baada ya wagombea kutotimiza idadi ya kura zinazotakiwa katika katiba .

Hivyo amewataka wanachama cha chama cha Mapinduzi CCM , kuendelea kushirikiana na wafuasi wa vyama vya upinzani katika shuhuli za kijamii ambazo zinasaidia kupatikana na maendeleo yao na taifa kwa ujumla
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com