Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Selemani Jafo,
ametangaza rasmi siku ya uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa kuwa
utakuwa siku ya tarehe 24 Novemba, 2019, uchaguzi utakao fanyika kote
hapa nchini.
Waziri Jafo ametangaza siku hiyo
Jijini Dodoma, wakati wa mkutano na wakuu wa mikoa wakati wa kuwapa
maelekezo na makabidhiano ya nyaraka zinazohusiana na uchaguzi huo
amesema ametangaza uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria.
Amesema uchaguzi utafanyika
novemba 24, 2019 kuanzia majira ya saa mbili kamili(12:00)hadi saa kumi
kamili (10:00) jioni na tayari maandalizi yote tayari yamekamilika kwa
ajiri ya uchaguzi huo.
“Tangu kurejeshwa kwa mamlaka za
Serikali za Mitaa katika mfumo wa utawala kupitia sheria ya Serikali za
Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na sheria ya Serikali za Mitaa
(Mamlaka za Miji), Sura ya 288, uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika
ngazi ya Mtaa, Kijiji na Kitongoji”
“Umekuwa ukifanyika katika kila
kipindi cha miaka mitano, uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwezi Oktoba
mwaka 2014 na hivyo uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika mwaka 2019, na
tarehe hiyo ni Novemba 24, mwaka huu” amesema Jafo.
Amesema uchaguzi huu unaongozwa
kwa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi
ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa katika mamlaka za Wilaya na mamlaka za
Miji, kwa mujibu wa matangazo ya Serikali Na. 371, 372 373 na 374 ya
mwaka 2019.
Amebainisha nafasi zitakazo
gombewa katika uchaguzi huo, “Mwenyeviti wa Kitongoji katika mamlaka za
Miji Midogo, kwa nafasi hiyo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni
za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za Miji Midogo za
mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 371 la Mwaka 2019)”. Amesema.
Pia wengine ni wenyekiti wa
Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (kundi mchanganyiko la wanaume na
wanawake) na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi la Wanawake) katika
Mamlaka za Miji, kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa
kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa kamati ya Mtaa
katika Mamlaka za Miji za mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 372 la
Mwaka 2019).
Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe
wa halmashauri ya Kijiji (Kundi mchanganyiko la wanaume na wanawake),
Wajumbe wa halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na Wenyeviti wa
Vitongoji katika mamlaka za Wilaya.
Kwa nafasi hizo, uchaguzi
utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji,
Wajumbe wa halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika
Mamlaka za Wilaya za Mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 373 la Mwaka
2019); na
Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe
wahalmashauri ya Kijiji (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake),
Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa
Vitongoji katika Mamlaka za Miji.
Kwa nafasi hizo, Uchaguzi
utaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji,
Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika
Mamlaka za Miji za Mwaka 2019 (Tangazo la Serikali Na. 374 la Mwaka
2019).
Waziri Jafo amewataka Wakuu wa
mikoa kuhakikisha wanasimamia na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi
juu ya uchaguzi huo sambamba na kuhakikisha vifaa vinafika kwa wakati
maeneo husika na kuratibu uchaguzi huo, na amebainisha kampeni zitaanza
siku saba kabla ya uchaguzi huo.
Akiongea kwa niaba ya wakuu wa
mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Singida Rehema Nchimbi amesema kama wakuu wa
mikoa wamepokea maelekezo yote na wataenda kuyafanyia kazi pamoja na
kuhakikisha uchaguzi huo unaenda kama ulivyopangwa na kuhakikisha vifaa
vinafika kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment