Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.
Hassan Abbasi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo
jijini Dodoma wakati wa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Serikali
katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali
inayofanywa na Rais Dkt.Pombe Magufuli
……………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.
Hassan Abbasi,amesema kuwa Tanzania imeendelea kupanda kutokana na nia
njema na shughuli kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwaletea
wananchi Maendeleo kupitia miradi mbalimbali.
Hayo ameyasema leo jijini Dodoma
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utekelezaji wa
Serikali kwa mwezi Agosti 2019.
Dkt.Abbasi,amesema kuwa kwa mujibu
wa Ripoti iliyotolewa Julai 12, 2019 kwa pamoja kati ya Transparency
International na Afro-Barometer, Tanzania imeongoza katika nchi 35 kwa
kuonesha juhudi za wazi katika kupambana na rushwa.
“Mafanikio haya yanatokana na
msimamo thabiti wa Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake katika kuimarisha
taasisi muhimu kama vile TAKUKURU, Kuanzisha Mahakama ya Ufisadi na
Uhujumu Uchumi, mfumo wa udhibiti wa rushwa katika manunuzi kupitia
PPRA”, amesisitiza Dkt. Abbasi.
Hata hivyo ametolea mfano kwa
TAKUKURU kuwa imeokoa jumla ya shilingi bilioni 86 zilizotokana na
mishahara hewa na ukwepaji kodi.
Dkt.Abbasi amefafanua kuwa jumla
ya shilingi bilioni 25.5 zimerejeshwa Serikalini kwa mchanganuo ufuatao;
bilioni 14.6 ikiwa ni urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya
uhalifu na bilioni 10.9 zilizotokana na thamani ya mali zilizotaifishwa
yakiwemo magari, vituo vya mafuta, nyumba nane, magari nane na Bilioni
20 ambazo ni mali zilizozuiwa kesi zikiendelea.
Amesema kuwa kwa upande wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeokoa takribani shilingi
bilioni 46.9 zilizokuwa zipotee kutokana na kutofuatwa taratibu za
ununuzi, malipo ya zaidi ya mkataba kwa wakandarasi au baadhi
kutorudisha fedha walizopewa kama dhamana na uzembe na rushwa.
Aidha ameelezea utekelezaji katika
sekta ya uchukuzi, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali imeanza zabuni ya
kuagiza vichwa 22 (vitano vya mafuta yaani Diesel Locomotive na 17 vya
umeme yaani Electrical Locomotive) na mabehewa ya abiria 60 na 1430 ya
mizigo.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali
imeanza zabuni ya treni tano (5) zilizokamilika (Electrical Multiple
Unit) za abiria zenye mabehewa nane (8) kila moja na vichwa viwili kwa
ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar es salaam
hadi Morogoro na kisha Dodoma.
Dkt.Abbasi ameongelea kuwa,
Serikali imetenga fedha za ndani shilingi Bilioni 71.4 kwa ajili ya
ujenzi wa Daraja jipya la Mto Wami lenye urefu wa Mita 513.5
litakalojumuisha ujenzi wa barabara za KM 4.3 kwa kila upande ambapo
kazi ya ujenzi huo imeshaanza.
Pia, Serikali imesaini mkataba wa
shilingi bilioni 699.9 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja refu zaidi Afrika
Mashariki na Kati la Kilometa 3.2 kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita
kwenye eneo la Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria.
Katika Sekta ya Afya, Dkt Abbasi
amesema kuwa, Serikali imeshatoa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Ujenzi
wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (RHH) na sehemu nyingi ujenzi
umekamilika. Mikoa husika ni; Mwanza, Simiyu, Njombe, Songwe, Katavi,
Geita na Dar es Salaam (Mwananyamala) na kuna Bilioni 3 imetolewa
Kujenga Hospitali ya Kanda ya Wazazi Mbeya na shilingi bilioni 6.32
kujenga Hospitali ya Kanda Mtwara.
katika kuwekeza katika maisha ya
watu ngazi ya Wilaya, Serikali mapema mwaka huu ilitoa shilingi Bilioni
105 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 ambapo katika miaka
zaidi ya 50 ya Uhuru tumekuwa na Hospitali katika Wilaya 77 tu; ndani ya
mwaka huu mmoja zinajengwa 67 ambapo ujenzi umekamilika kwa zaidi ya
asilimia 90.
Hata hivyo Dkt.Abbasi
amewahakikishia Watanzania kuwa azma yetu ya kuiendeleza nchi kwa kasi
chini ya Rais Dkt. Magufuli inaendelea kushika kasi na katika hili
hakuna mwanadamu wa kuzuia wala kuirudisha nyuma.
0 comments:
Post a Comment