Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifunga
rasmi mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC katika Ukumbi
wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere leo Jumapili Agosti
18, 2019.
****************
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
18.8.2019
RAIS Dkt. John Magufuli amewataka
Wakuu Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendelea
kuimarisha Umoja na Mshikamano na kuwa na sauti moja katika kusimamia
maslahi mapana ya Jumuiya hiyo katika kuleta maendeleo kwa wananchi
wake.
Akifunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa
Nchi za Jumuiya hiyo, leo Jumapili (Agosti 18, 2019), Jijini Dar es
Salaam, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo alisema
Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitaji ili kuharakisha
jitihada za kuleta maendeleo katika jumuiya hiyo.
Aliongeza kuwa Umoja ni kiungo
muhimu cha maendeleo katika ushirikiano wa Jumuiya yoyote, hivyo ili
kuleta kasi ya mabadiliko ndani ya Jumuiya hiyo ni wajibu wa Nchi
wanachama kuhakikisha inatumia vyema rasilimali zake pamoja na kuweka
mkazo wa maazimio na agenda za Mkutano wa 39 kwa kutafakari masuala
muhimu ya maendeleo.
Rais Magufuli alisema chini ya
Uongozi wake, jumuiya hiyo itaendelea kusimama imara na kuwa na nguvu ya
pamoja katika kutetea maslahi ya Nchi wanachama ikiwemo vikwazo
ilivyowekewa Nchi ya Zimbabwe na kusema Viongozi wa Jumuiya hiyo kwa
kauli moja wameungana katika kuitaka jumuiya ya kimataifa kuondoa
vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
“Tutahakikisha kuwa jumuiya yetu
inaondoa changamoto mbalimbali zinazozuia ukuaji wa uchumi ukiwemo
vitendo vya rushwa na ukiritimba vinavyokwamisha sekta ya sekta ya
biashara baina ya nchi zetu” alisema Rais Magufuli.
Akifafanua zaidi, Rais Magufuli
alisema katika mkutano huo wa 39, Wakuu wa Jumuiya hiyo kwa pamoja
wameweza kuwa na mjadala wa pamoja uliowawezesha Viongozi hao kutoa
maoni, ushauri na michango yao na pamoja kusaini itifaki mbalimbali
zilizoridhia agenda na mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuharakisha
maendeleo ya Jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli
alisema kutokana na kasi ndogo ya ukuaji uchumi iliyopo kwa sasa ndani
ya jumuiya hiyo, aliwataka Viongozi hao kuhakikisha wanaweka mkazo
katika kukuza na kuimarisha sekta ya miundombinu pamoja na kuboresha
sera za kifedha na kiuchumi ili kukuza kiwango cha ukuaji wa Pato la
Taifa kwa kila Nchi mwanachama.
Rais Magufuli pia aliitaka
Sekretarieti ya Jumuiya kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa badala
ya fedha hizo kutumika katika kuandaa makongamano, warsha na semina
mbalimbali na sasa zielekezwe katika utekelezaji wa miradi inayoweza
kuleta manufaa kwa nchi wanachama ndani ya jumuiya hiyo.
“Katika Bajeti yetu ya mwaka
2019/2020 tumepanga kutumia Dola Milioni 74, mchango wa Dola Milioni 43
zinazotolewa nan chi wahisani tunaweza kujenga vituo 17, nitafurahi
kuona siku moja Sekretarieti ya jumuiya yetu ikiwaalika wanachama katika
uzinduzi wa vituo hivyo” alisema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli aliwakaribisha wawekazaji waliopo ndani ya SADC kuja kuwekeza
katika miradi ya sekta mbalimbali iliyopo nchini ikiwemo nishati,
madini, utalii, mifugo, kilimo pamoja na utalii kwani Tanzania imeweka
mazingira bora na wezeshi kwa kwa ajili ya wawekezaji na
wafanyabiashara.
Akizungumzia kuhusu maombi ya Nchi
ya Burundi kujiunga na Jumuiya hiyo, Rais Magufulli alisema
Sekretarieti ya jumuiya hiyo imepanga kutuma timu ya uchunguzi katika
nchi hiyo kwa ajili ya kujiridhisha na masuala muhimu ya kimsingi
yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kukubaliwa kwake kujiunga na Jumuya
hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Jumuiya hiyo, Dkt. Stegomena Tax alisema Mkutano huo wa 39 wa SADC
umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Nchi wanachama ambapo wameweza kuweka mikakati ya pamoja
itakayosaidia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na maendeleo ya Nchi hizo.
Dkt. Tax alisema kuwa katika
mkutano huo pia, Viongozi wa Jumuiya hiyo waliweza kufanya maamuzi ya
kuchagua viongozi wa ndani katika Jumuiya hiyo ikiwemo Nafasi ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndani ya Jumuiya hiyo
(TROIKA) aliyokwenda kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.
0 comments:
Post a Comment