METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, August 25, 2019

PROGRAMU YA MAFUNZO YA UJASIRIMALI NA USIMAMIZI WA BIASHARA KUWANUFAISHA VIJANA MKOANI GEITA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, akizungumza na vijana wa Mkoa wa Geita alipokuwa akizindua Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana inayoratibiwa na kusimamiwa na ofisi yake.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Hamim Gwiyama akitoa taarifa fupi kuhusu fursa zilizopo katika Mkoa wa Geita zinazoweza kuwanufaisha vijana wa mkoa huo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa akielezea kuhusu Programu hiyo ya ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara kwa vijana wa Geita ambapo vijana 150 walihudhuria mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Sehemu ya Vijana Wajasiriamali wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo Mkoani Geita.
Baadhi ya vijana wajasiriamali wakimsikilza kwa makini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizindua awamu ya tatu ya utekelezaji wa Programu ya Mafunzo na Usimamizi wa Biashara kwa vijana wa Mkoa wa Geita.
Sehemu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Geita.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akigawa cheti cha Ushiriki kwa mmoja wa vijana aliyeshiriki katika mafunzo hayo Bw. Daniel Ntigizu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na Vijana alipokuwa akizindua awamu ya tatu ya utekelezaji wa Programu ya Mafunzo na Usimamizi wa Biashara kwa vijana wa Mkoa wa Geita.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na Wawezeshaji wa Mafunzo ya Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Hamim Gwiyama mara baada ya kuwasili katika Mkoa huo kwa ajili ya uzinduzi wa awamu ya tatu ya utekelezaji wa Programu ya Mafunzo na Usimamizi wa Biashara kwa vijana wa Mkoa wa Geita. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Deogratius Kayango.
…………………………………………………..
Na; Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imedhamiria kuwawezesha vijana kupitia programu ya mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamaizi wa Biashara kwa lengo la kuwawezesha kukuza na kurasimisha biashara zao.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa programu ya mafunzo hayo katika Mkoa wa Geita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa mafunzo hayo ni mahususi kwa vijana na yatawawezesha vijana kupata elimu juu ya masuala mbalimbali ya ujasiriamali na biashara ikiwemo urasimishaji wa biashara, kutambua ushindani, upatikanaji wa mitaji,  masuala ya uchambuzi wa masoko, mikakati na uendeshaji wa biashara.
“Mafunzo haya yanamanufaa sana kwenu ninyi vijana kwa kuwa yatawawezesha kukua kwa kasi katika biashara zenu mnazoziendesha na hivyo kuwajengea wigo mpana wa kuendeleza shughuli za kiuchumi mnazozifanya,” alisema Mhagama
Alifafanua kuwa Ujasirimali ni moja ya nguzo za sera ya taifa ya uwezeshaji ambayo inalenga kuinua viwango vya ujuzi na uzoefu wa masuala ya biashara nchini.
Alieleza kuwa, kupitia programu hiyo vijana 4,000 watanufaika na Mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo vijana nchini kuwa na uelewa juu ya masuala ya biashara ikionesha utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli katika kuwawezesha vijana.
“Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuwajengea uwezo vijana kote nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kujiajiri, kuajiri wenzao kwa ujumla pamoja,” alisisitiza Mhagama
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali katika kuwawezesha vijana inatekelezwa kwa vitendo kupitia programu mbalimbali ikiwemo ya ukuzaji ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, mmoja wapo ikiwemo ya Mafunzo ya Ujasirimali kwa vijana.
Sambamba na hayo, Mhe. Mhagama aliwasihi vijana walioshiriki mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kuwa ni chachu ya mageuzi katika kuboresha biashara zao. Pia aliwataka vijana hao kueneza ujuzi waliopata kupitia mafunzo hayo kwa vijana wenzao.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa maagizo kwa viongozi wa Mkoa huo kuhakikisha vijana wanashiriki kwa wingi katoka mafunzo hayo kwa kuwa yataleta matokeo chanya kwa jamii na yatakuwa ni chachu kwa vijana katika kujiletea maendeleo sambamba na kuwawezesha kuchangia pato la Taifa.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Hamim Gwiyama ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa vijana maana wao ndio nguvu kazi ya taifa, hivyo kijana akiwa na ujuzi wa mambo mbalimbali ya biashara ni faida kwake kutambua njia bora za kukuza shughuli zao za uzalishaji mali.
“Katika Mkoa wa Geita vijana walikuwa na mawazo kuwa dhahabu ndio biashara pekee itakayowapa faida, ila kupitia mafunzo haya wataweza kutambua kuwa biashara yoyote wakisimamia vizuri itakuwa na manufaa kwao,” alisema Gwiyama
Naye, Mmoja wa Vijana walioshiriki katika Mafunzo hayo Bw. Salim Hassan aliweza kutoa shukrani zake kwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yameweza kuwatoa katika sehemu moja na kuwapeleka hatua nyingine.
“Leo tumepata stadi za msingi katika masuala ya ujasirimali na biashara, tumeweza kuelewa umuhimu wa kutunza kumbukumbu, usimamizi wa fedha, taratibu za kurasimisha biashara na jinsi ya kutafuta masoko,” alisema Hassan
Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, Jijini Dodoma Julai 29, 2019. Mafunzo hayo yanasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) katika Mikoa nane (8) ya Tanzania Bara ikiwemo Dodoma, Ruvuma, Geita, Mwanza, Lindi, Mbeya, Arusha na Tanga. Tayari vijana kutoka Mkoa wa Dodoma na Ruvuma wamekishwa nufaika na mafunzo hayo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com