Na Shamimu Nyaki WHUSM- DODOMA
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amevipongeza Vyombo vya Habari
nchini kwa kazi kubwa ya kiuzalendo na weledi wa hali ya juu katika
kutangaza Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC) uliomalizika jana Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mwakyembe ametoa pongezi hizo
jana Jijini hapo ambapo amesema kuwa uandishi wa habari wa kujenga na
kukosoa ambao una lengo la kurekebisha unahitaji kupongezwa kwakua
unasaidia jamii na Serikali katika kuleta maendeleo ya haraka kwa Taifa.
“Waandishi wa habari mbali na
kuutangaza Mkutano wa 39 wa SADC lakini pia wametumia taaluma yao
kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini kupitia sekta
mbalimbali ikiwemo Uwekezaji katika viwanda, Utalii, Uchukuzi na
nyinginezo,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Ameongeza kuwa Uwenyekiti wa
Tanzania ambao unaendeshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli umeleta ari na matumaini mapya ambayo
yatasaidia nchi wanachama kuondoa vikwazo vingi vya kibiashara na
mawasiliano ya karibu baina ya nchi wanachama na kujenga ustawi wa
uchumi kwa nchi hizo.
Aidha Mhe. Mwakyembe amesema kuwa
baada ya lugha adhimu ya Kiswahili kutangazwa rasmi kuwa miongoni mwa
lugha nne zinazotumika ndani ya Jumuiya hiyo, amewataka Watanzania
kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa za lugha hiyo ikwemo uandishi wa
vitabu vya kiada, ufundishaji wa lugha hiyo, kuuza Sanaa zinazotokana na
lugha hiyo kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Mkutano wa Jumuiya ya Kusini mwa
Afrika SADC kwa Wakuu wa nchi na Viongozi wa Serikali umefanyika kuanzia
Agosti 17- 18,2019 ambapo mambo mbalimbali yanayohusu nchi hizo
yalijadiliwa ikwemo namna bora ya kuimarisha biashara ndani ya nchi
hizo ambapo Tanzania imeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa
kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment