METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, July 7, 2019

WENYEJI MISRI YAPIGWA 1-0 NA BAFANA BAFANA NA KUTUPWA NJE MICHUANO YA AFCON

WENYEJI, Misri wametupwa nje ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuchapwa 1-0 na Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ katika mchezo wa hatua ya 16 Bora usiku wa Jumamosi Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Shujaa wa Bafana Bafana ni nyota wa Orlando Pirates ya nyumbani, Afrika Kusini, Thembinkosi Lorch aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 85 akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Lebo Mothiba wa Strasbourg ya Ufaransa baada ya shambulizi la haraka wakitoka kushambuliwa.
Mshambuliaji wa Liverpool na mshindi wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mohamed Salah alishindwa kuzuia machozi baada ya mchezo huo timu yake, Misri ikitolewa mapema mno baada ya kushinda mechi zote za Kundi A.

Misri wameungana na wana fainali wenzao, Cameroon kuishia hatua hii katika AFCON ya mwaka huu baada ya Simba Wasiofungika nao kuchapwa 3-2 na Nigeria katika mchezo uliotangulia Jumamosi. Ikumbukwe Cameroon walitwaa taji la AFCON Februari 5, mwaka 2017 baada ya kuichapa Misri 2-1 katika fainali Uwanja wa l’Amitié mjini Libreville nchini Gabon.
Uwanja wa Alexandria mabao ya Nigeria yalifungwa na Odion Jude Ighalo wa Shanghai Shenhua ya China dakika ya 19 na 63 na Alex Iwobi wa Arsenal dakika ya 66, wakati ya Cameroon yalifungwa na Stephane Bahoken wa Angers SCO dakika ya 41 na Clinton Mua N’Jie wa Olympique Marseille zote za Ufaransa dakika ya 44.
Nigeria na Afrika Kusini zinaundana na Benin na Senegal zilizokuwa za kwanza kufuzu Robo Fainali Ijumaa baada ya kuzitoa Morocco na Uganda.
Hatua ya 16 Bora ya AFCON 2019 inaendelea leo kwa mechi mbili pia, Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Algeria na Guinea.
Hatua hiyo itahitimishwa Jumatatu kwa mechi nyingine mbili; Mali na Ivory Coast na Ghana na Tunisia.

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com