**************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amezionya Halmashauri za Wilaya na Manispaa zilizoshindwa kufikisha
malengo ya makusanyo ya kodi na kuzitaka zijitathmini ni kwa nini
hazijafikisha malengo hayo.
“Kuna Halmashauri zimetajwa
hapa kwamba hazijafikisha malengo ya makusanyo ya ndani. Fanyeni
tathmini, ni kwa nini hamjafikia malengo na mhakikishe kuwa mwakani
hamji kutajwa tena kwenye mkutano kama huu,” alisema. Halmashauri hizo
ni Kakonko, Buhigwe, Madaba, Kigoma, Momba na Songea.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumanne, Julai 23, 2019) wakati akizungumza na washiriki wapatao 700
ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT)
unaoendelea jijini Mwanza.
Waziri Mkuu ambaye amefungua
mkutano huo wa siku tatu kwa niaba ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe
Magufuli, amewataka washiriki wa mkutano ambao ni Mameya, Wenyeviti wa
Halmashauri, Wakurugenzi wa Majiji, Miji na Manispaa, wasimamie
makusanyo ya mapato kupitia vyanzo vyao ili waweze kupanga mipango ya
maendeleo. “Lengo la Serikali ni kuwezesha kila Halmashauri zijitegemee
kwa asilimia 80-100 ifikapo 2025,” amesema.
“Katika makusanyo hayo,
hakikisheni kuwa mnatenga asilimia 40 kwa ajili ya shughuli za
maendeleo. Na hili ni tatizo kwa Halmashauri nyingi zikiwemo zile kubwa.
Ukifuatilia kwa makini huoni miradi inayogusa maisha ya wananchi wa
kawaida.”
“Ukichukulia Dar es Salaam au
Arusha ambao wanakusanya kati ya shilingi bilioni tano na 10, ni mradi
gani wa thamani kubwa uliojengwa kwa kutumia fedha zenu za ndani,
ukiacha hii mikubwa ya stendi za mabasi au barabara za lami ambayo
inajengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu?” alihoji.
“Hivi kuna Halmashauri ambayo
imejenga kituo cha afya cha kisasa kwa kutumia fedha zake za makusanyo?
Afadhali hawa wa Dodoma ambao wameanza kujenga stendi ya mabasi na
hoteli mbili za kitega uchumi,” amesema.
“Uamuzi wa Mheshimiwa Rais Magufuli wa kukusanya fedha zote na kuziweka kwenye chanzo kimoja ulitokana na study
ya muda mrefu iliyofanyika na kubaini kuwa fedha zinazokusanywa
haziendi kwenye miradi inayogusa wananchi. Niwasihi sana, fanyeni miradi
ambayo kila Mtanzania angependa kuiona kwenye Mamlaka zenu za Serikali
za Mitaa,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Serikali iliamua kumuondoa
aliyekuwa Katibu Mkuu wa ALAT, Bw. Abraham Shamumoyo kwa sababu ya
utendaji mbovu.
“Kuna maamuzi alikuwa
akiyafanya bila kuishirikisha Kamatai ya Utendaji. Kuna mikataba ilikuwa
ikifanyika na mingine inahusisha hadi mataifa ya nje. Kuna fedha
zilitolewa, zikawekwa kwenye akaunti binafsi na siyo akaunti ya ALAT,”
amesema.
Amesema ALAT ni taasisi kubwa
ya Serikali ambayo inahitaji kuheshimiwa, na siyo ya kuancha iendeshwe
na mtu mmoja kama atakavyo. “ALAT ni taasisi kubwana Serikali
inaitegemea. Niwahakikishie kuwa Mheshimiwa Rais, anawathamini,
anawapenda na anataka mchape kazi kuisaidia Serikali yenu,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri
Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais –TAMISEMI, Bw. Suleiman Jafo alisema Serikali inajivunia ujenzi wa
shule za sekondari za kata ambazo mwaka huu zimefanya vizuri kwenye
mitihani ya kuhitimu kidato cha sita.
“Kati ya shule bora 100, shule
64 ni za Serikali na kazi ya shule hizo 64, shule 54 ni za kata. Na
kwenye matokeo ya masomo ya sanaa, kati wanafuzi bora 10 wa kiume,
wanafunzi saba wanatoka kwenye shule za kata,” alisema.
Alisema Serikali ya awamu ya
tano imewekeza sana kwenye sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule za
sekondari na ukarabati wa shule kongwe za sekondari.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza
Serikali kwa kutenga sh. bilioni 268.8 kwa ajili ya ujenzi wa miradi 38
ya kimkakati kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kama vile ujenzi wa
masoko, machinjio na stendi za mabasi.
0 comments:
Post a Comment