Na. Antonia Mbwambo – Mbeya
Tarehe 19 Oktoba, 2026
Mwakilishi wa Katibu Mkuu -UTUMISHI, ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Ufuatiliaji wa Sera katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Olgatho Mwinuka, amezitaka Wizara na Taasisi za Umma kuimarisha afua za kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY), pamoja na kuweka mikakati ya kulinda afya ya akili ya watumishi mahali pa kazi, kwa lengo la kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Bw. Mwinuka ameyasema hayo Oktoba 19, 2026, wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi, katika ufunguzi wa kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 cha Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Amesema kuwa hatua za kudhibiti magonjwa hayo zinapaswa kujumuishwa katika mipango, bajeti na shughuli za kawaida za Wizara na Taasisi za Umma ili kulinda afya za watumishi na kuongeza ufanisi kazini.
“Afya ya mtumishi ni sehemu muhimu ya mafanikio ya Taasisi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha afua hizo zinatekelezwa kwa vitendo, pamoja na kuimarisha huduma za afya ya akili na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watumishi,” amesema Bw. Mwinuka.
Katika kuimarisha utekelezaji wa afua hizo, Bw. Mwinuka amewahimiza waajiri kutoa elimu na mafunzo kwa watumishi na kujenga uwezo wa kamati, waratibu na waelimishaji rika wanaohusika na kazi hiyo.
Amebainisha kuwa Ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara na Taasisi za Umma katika kufuatilia utekelezaji, kutathmini mafanikio na kubaini changamoto zinazohitaji ufumbuzi.
Kadhalika Bw. Mwinuka amezitaka Wizara kuhakikisha Taasisi za Umma zilizo chini yake zinatekeleza Mwongozo wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2014 na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati. Hatua hiyo itaiwezesha Serikali kutathmini maendeleo, kubaini changamoto na kupanga maboresho yanayohitajika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Anuai za Jamii ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi Bi. Juliana Ntukey ametoa wito kwa wajumbe wa kikao hicho kushiriki kikamilifu ili kupata maazimio yatakayoimarisha utendajikazi katika maeneo yao ya kazi kwa ustawi wa Taifa.





0 comments:
Post a Comment