Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua
kitabu cha muongozo wa uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma, kwenye maonesho
ya viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma. Julai 25.2019. Tokea
kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje John Ndumbalo na Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma, Christina Mndeme.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza
na wananchi, baada ya kufungua maonesho ya viwanda na kongamano la
uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai 25.2019..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimsikiliza
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa China Tanzania, Bwana Xian Ding,
wakati alipoipongeza Serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea wananchi
wake maendeleo, kwenye maonesho ya viwanda na kongamano la
uwekezaji,yaliyofanyika katika Mkoa wa Ruvuma, Julai 25.2019..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia
mkaa wa mawe, uliyotengenezwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na
wajasiriamali wa kikundi cha Mbalawala Women Group, wakati akikagua
mabanda kwenye maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani
Ruvuma, Julai 25.2019. Tokea kulia ni Meneja wa Fedha wa kikundi hicho,
Esta Silas na Msimamizi wa Mradi, Hajra Yakub.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa
amebeba mkaa wa mawe, wakati akikagua mabanda kwenye banda la TANCOAL,
katika maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma,
Julai 25.2019. Tokea kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme
na kulia ni Mkuu wa Jiolojia TANCOAL.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa na
mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme (kushoto),
akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Mbinga Coffee Curing Company,
kabla ya kufungua maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani
Ruvuma, Julai 25.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa na
mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme, akiangalia na
vikundi vya ngoma, kwenye maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji
mkoani Ruvuma, Julai 25.2019.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
………………
WAZIRI MKUU ATAKA RUVUMA IONDOE VIKWAZO VYA UWEKEZAJI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka
uongozi wa mkoa wa Ruvuma uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo
na kuondoa vikwazo vyote ili kuvutia wawekezaji zaidi.
“Mkoa wa Ruvuma kama ilivyo mikoa
mingine, unazo fursa ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia
kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Nitoe rai kwa mkoa
uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa
vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji
wa ndani na nje,” amesema.
Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi,
Julai 25, 2019) wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji
mkoani Ruvuma linaloendelea kwenye uwanja wa Majimaji, Manispaa ya
Songea. Pia amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa huo.
Amesema katika ustawi wa uchumi, nchi
nyingi hapa duniani zimeweza kukuza uchumi wao kupitia ujenzi wa viwanda
na zikafanikiwa kupunguza umasikini katika jamii zao. Amezitaja nchi
hizo kuwa ni Marekani, China, Japani, Korea ya Kusini na Ujerumani.
“Tunapaswa kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo
maana Tanzania pia tunahamasisha ujenzi wa viwanda kuanzia ngazi ya
vijiji mpaka mikoa ili tulete mageuzi ya kiuchumi yatakayowezesha
upatikanaji wa ajira na hatimaye kuondoa umaskini,” amesema Waziri Mkuu
na kuongeza:
“Kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni “Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda, wekeza sasa,”
imelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani humu,
na inajipambanua vema na kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano
ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025.”
Amesema mchango wa sekta ya viwanda
kiuchumi na kijamii nchini ni pamoja na kuongeza pato la Taifa na
kupandisha hali ya maisha ya wananchi; kusaidia nchi isiyumbe kiuchumi
ikizingatiwa kuwa viwanda vingi havitegemei hali ya hewa kama kilimo;
kuboresha urari wa biashara (improve balance of trade) kwa sababu tija yake ni kubwa na hasa zikiuzwa bidhaa nyingi nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Amezitaja faida nyingine kuwa ni
kuchangia maendeleo ya sekta nyingine kama za kilimo, uvuvi, elimu na
madini; kutengeneza ajira kwa wananchi; kuchagiza na kuharakisha
maendeleo ya teknolojia na rasilimali watu na kuwezesha matumizi mazuri
ya maliasili zilizopo kwa faida zaidi.
Nyingine ni kuleta uhakika wa soko la
mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa sababu hutumika
kama malighafi na kuwepo kwa uhakika wa kuingiza fedha za kigeni nchini
kupitia mauzo ya bidhaa nje ambapo husaidia kuagiza mitambo, malighafi
na bidhaa nyingine ambazo hazizalishwi nchini.
Mapema, akitoa salamu
kwa niaba mabalozi wengine, Mwakilishi wa Balozi wa China, Bw. BW. XIAN
DING alisema ana uhakika kuwa kongamano hilo litafanikiwa kuleta
mabadiliko mkoani humo kwa sababu wana bidii ya kazi.
“Ninaahidi kuleta wawekezaji kutoka China
kwa sababu tunataka waje kuleta teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na
Watanzania na wawafundishe teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma
iwe model (mfano) kwa mikoa mingine,” alisema.
Akielezea kwa kifupi
kuhusu mwongozo uliozinduliwa na Waziri Mkuu, mtafiti kutoka Taasisi ya
Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Hoseana Lunogelo alisema
walitumia mfumo shirikishi ili kupata mwongozo unahusisha wawekezaji wa
ndani.
“Mwongozo huu umezingatia Dira ya Taifa
ya 2025 katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwa nchi ya uchumi na
viwanda, tumeshirikisha wananchi wa mkoa wa Ruvuma ili wasibakie kuwa
watazamaji,” alisema.
0 comments:
Post a Comment