Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihesabu
vipande vya dhahabu baada ya kukabidhiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Kenya Monica Juma wa pili kushoto. Wa kwanza kushoto ni Makamu wa Rais
Mama Samia Suluhu Hassan na kulia ni Waziri wa Madini Doto Biteko kulia
kwake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba Kabudi.
………………..
Na Issa Mtuwa “WM”– Ikulu DSM
Tukio kubwa la kihistoria lililofanyika
Ikulu jijini Dar es salaam tarehe 24/07/2019 la kupokea na kukabidhiana
dhahabu yenye uzito wa Kg. 35 iliyokamatwa Kenya ikitokea Tanzania ndio
lililo wafanya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli na Waziri wa Madini Doto Biteko kuongelea sekta ya madini kwa
lugha ya “kitakwimu” (Namba).
Katika tukio hilo Rais Dkt. John Pombe
Magufuli alipokea na kukabidhiwa dhahabu hiyo iliyokamatwa Kenya baada
ya kutoroshwa kutoka Tanzania siku ya tarehe 15/02/2018 baada ya kuvuka
mipaka ya Tanzania na kukamatwa Kenya. Dhahabu hiyo ililetwa Tanzania na
mjumbe maalum ambae pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Monica Juma
alie tumwa na Rais Uhuru Kenyata kuja kukabidhi dhahabu hiyo.
Akizungumzia mafanikio katika sekta ya
madini mara baada ya kupokea na kukabidhiwa dhahabu hiyo, Rais Magufuli
alisema, tangu afanye mageuzi makubwa katika sekta ya madini sambamba na
marekebisho ya sheria kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Alisema kuanzishwa kwa wizara maalum ya
kusimamia madini, ujenzi wa ukuta huko Mirerani, uanzishwaji wa masoko
ya madini na marekebisho ya sheria vimekuwa chachu ya mafanikio katika
sekta hiyo.
Rais Magufuli aliyataja baadhi tuu ya
mafanikio hayo kuwa ni kupunguza kodi nyingi kwa wachimbaji wadogo, pia
tangu mwezi Machi 2019 jumla ya masoko 28 ya madini yameanzishwa nchini
kote, ongezeko la mapato kutoka sekta ya madini ambapo mwaka 2017/2018
malengo ya makusanyo yalikuwa bilioni 191 lakini wizara ilikusanya
bilioni 301 sawa na ongezeko la bilioni 110, mwaka 2018/2019 malengo
yalikuwa kukusanya bilioni 310 lakini ikakusanywa bilioni 335 sawa na
ongezeko la bilioni 25 na mwaka wa fedha 2019/2020 imekadiriwa kukusanya
bilioni 470.35.
Kwa upande wa udhibiti wa matukio ya
utoroshwaji wa madini, Rais Magufuli alisema, katika kipindi cha miaka
mitatu jumla ya matukio 102 yaliripotiwa ambayo yalihusisha madini yenye
uzito wa gramu 163, 566,416.45 na Carat 6826.68 huku thamani ya madini
yote ikikadiriwa kuwa na zaidi ya bilioni 45.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto
Biteko akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Magufuli, alisema takwimu za mauzo
kwenye masoko ya madini kumekuwa na mafanikio makubwa. Alisema mpaka
sasa zaidi madini yenye thamani ya bilioni 136.7 yameuzwa kwenye masoko
yote nchini na serikali imepata mrabaha na clearance fee ya jumla ya
bilioni 7.7. Aliongeza kuwa dhahabu iliyokuwa inakusanywa kwa mwaka sasa
wanakusanya kwa siku moja kutokana na uwepo wa masoko hayo.
“Mhe. Rais pale Chunya kwa mwaka tulikuwa
tunakusanya Kg. 12 lakini tunavyo zungumza tangu kuanzishwa kwa soko
lile tarehe 21/03/2019 mpaka leo tarehe 24/07/2019 jumla ya Kg. 270
zimeuzwa kwenye soko hilo”. Alisema Biteko.
Kwa upande wa utoaji wa leseni za
uchimbaji, Biteko alisema tangu mwaka 2010 wizara haijawahi kutoa leseni
kubwa zenye gharama ya USD 100, lakini mwaka huu wanakwenda kutoa
leseni mbili kubwa ambapo mchakato wake umekamilika. Aliongeza kuwa
leseni 2673 za wachimbaji wadogo zimetolewa huku leseni za uchimbaji wa
kati 32 na leseni 105 za utafiti wa madini zimetolewa. Biteko aliongeza
kuwa mwaka huu pia watatoa leseni 2 ya Refinery kwa ajili ya dhahabu na
1 ya Smelter.
Kuhusu wanao hujumu masoko ya madini
alisema teyari wamesha ukamata mtandao wa wanaohujumu masoko hayo na
mpaka sasa watu 12 wamekamtwa wanaendelea “kupatiwa elimu” polepole na
vyombo vya dola.
Akimalizia maelezo yake ya kitakwimu kwa
Mhe. Rais, Biteko alimwambia Rais kuwa wizara yake inakabiliwa na
upungufu mkubwa wa watumishi na kwa upande wa Tume ya Madini pekee
inahitaji watumishi 220 hivyo anaomba kibali chake waweze kuajiri
watumishi hao ili kuongeza ufanisi wa wizara yake.
0 comments:
Post a Comment