**************
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TANTRADE) imesema itaendelea kuimarisha mitandao ya wadau na
makampuni mbalimbali wafanyabiashara ili kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchini wanapatiwa fursa za
masoko ili kuweza kukuza sekta ya biashara nchini.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi (Julai
11, 2019) na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Zanzibar, Latifa Khamis
wakati wa mkutano wa ana kwa ana baina ya wafanyabiashara, wazalishaji
na wanunuzi wa bidhaa za ngozi na shule katika Maonesho ya 43 ya
Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja
vya Julius Nyerere.
Latifa alisema kuwa Serikali
kupitia TANTRADE itaendelea kutumia majukwaa na fursa mbalimbali za
kibiashara kwa ajili ya kuwawezesha wajasirimali na wafanyabiashara
kuweza kutumia fursa zilizopo ikiwemo kupata masoko ya uhakika ya
biashara zao kupitia kwa wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya nchi.
“TANTRADE imeandaa mkutano huu
maalum kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo
kuweza kupata fursa za masoko ya kuuzia masoko yao ambapo utaratibu huu
utakuwa endelevu, hivyo kampuni ya DHL kupitia Market Plaze Africa
wametoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa hapa nchini
kutangaza biashara zao” alisema Latifa.
Aidha Latifa alisema mara baada ya
kuisha kwa maonyesho ya 43 ya DITF, TANTRADE imeandaa mkakati maalum wa
kuwaunganisha wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara kupitia maonesho
ya bidhaa za wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchi nzima ambapo
wataanzia katika Mkoa wa Ruvuma na baadae Zanzibar.
Aidha Latifa alisema katika
mkutano huo pia TANTRADE imewakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali
wadogo na taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki ya NMB ambayo
imekuwa na utaratibu wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali kuanzia kiwango
cha Tsh 500,000 hadi Milioni 50,000,0000.
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa
Kampuni ya DHL Tanzania, Paul Makolosi aliwataka wajasirimali na
wafanyabiashara wadogo kutangaza bidhaa zao katika taasisi hiyo kwa kuwa
masoko ya bidhaa zao yapo kwani nchi nyingi za mabara ya Ulaya na
Amerika yamekuwa wakivutiwa na bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Bara
la Afrika ikiwemo Tanzania.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo ina
uzoefu wa miaka 30 ya kufanya biashara duniani, ambapo katika utendaji
kazi wake imekuwa ikiwasaidia zaidi wajasiriamali wadogo waliopo katika
Bara la Afrika, hivyo ujio wa taasisi hiyo hapa nchini ni fursa kwa
wajasiriamali na wafanyabiashara hao.
“Katika Nchi za Bara la Ulaya na
Amerika, bidhaa za ngozi hususani viatu vimekuwa na soko kubwa sana, na
kwa kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wa hapa Tanzania
wamekuwa wakizalisha bidhaa hiyo, sisi DHL kupitia Market Place Africa
tupo tayari kuwasaidia ili kupata masoko ya uhakika” alisema Makolosi.
0 comments:
Post a Comment