Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu wa
ngozi walio kwenye ‘summer camp’ katika Chuo cha Ualimu Butimba Jijini
Mwanza. Ametumia fursa hiyo kuelezea juhudi ambazo Serikali imekuwa
ikizifanya katika kutatua changamoto za watoto wenye ulemavu ili waweze
kupata elimu.
Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole
Nasha wakati alipokutana nao kuzungumzia juhudi ambazo Serikali imekuwa
ikizifanya kutatua changamoto za watoto wenye ulemavu katika kupata
elimu.
………………………
Serikali imesema inatambua changamoto
zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum na ndio maana inachukua
juhudi za makusudi kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili
yawe rafiki kwao kupata elimu.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa jijini
Mwanza na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha
wakati akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi walio katika
Kambi ya Joto (Summer Camp) inayoratibiwa na Taasisi ya Under the Same
Sun.
Naibu Waziri Ole Nasha alisema katika
kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji
maalumu kwa sasa Wizara anayoiongoza inatekeleza Programu ya Elimu
Jumuishi ambayo inamuweka shuleni mtoto mwenye ulemavu na yule asie na
ulemavu kwa lengo la kuondoa fikra za kunyanyapaliwa lakini pia kujenga
umoja upendo na urafiki baina yao utakaowawezesha kulindana kwani siku
zote mlinzi mzuri ni rafiki na ndugu hivyo inasaidia kuondoa changamoto
zilizopo.
Aidha, Serikali pia inatoa mikopo kwa
asilimia mia moja kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma elimu ya
juu kwa lengo la kuwasadia waweze kupata elimu zaidi kwani watu wenye
ulemavu wakipata elimu wanaweza sio tu kujikomboa wenyewe lakini
kuwasaidia watu wengine wenye changamoto hizo.
“Ninyi wenyewe mtakuwa mashahidi Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika
Serikali yake kuna viongozi ambao wana ulemavu lakini kutokana na
umahiri na uwezo walio nao katika utendaji wameteuliwa katika nafasi
hizo. Tambueni kuwa watu wote wana haki sawa na hilo liko wazi,” alisema
Naibu Waziri ole Nasha.
Kiongozi huyo amewataka wanafunzi hao
kutambua kuwa wao ni watoto wa kitanzania hivyo wanatakiwa kuwa huru
kwenye nchi yao na kwamba Serikali itaendelea kuwalinda ili waweze
kuishi lakini pia kusoma kama watu wengine bila kudhuriwa na kitu
chotote.
”wote ni mashahidi kwamba kwa sasa
Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba mnakuwa na
usalama wa maisha yenu, sidhani kama kuna kosa ambalo sasa ukipatikana
nalo unachukuliwa hatua kubwa zaidi kama kujaribu kuwadhuru watu wenye
ualbino, na ndio maana sasa mnapata ulinzi kaeni mkiwa huru kwa kuwa
serikali inawajali,”aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole
Nasha amelitaka Shirika la Under The Same Sun kutambua kuwa Serikali
inathamini mchango mkubwa wanaoutoa katika kuwasaidia wanafunzi na
watoto wenye mahitaji maalum hasa watoto ambao wana changamoto ya
ulemavu wa ngozi na kuwataka kuhakikisha mafunzo wanayoyatoa katika
kambi za joto (summer camp) kila wanapokutana pamoja na mambo mengine
yalenge katika kuwaonesha watoto hao kuwa jamii inawajali na sio
vinginevyo.
Nae Afisa kutoka Idara ya Elimu ya
Shirika la Under the Same Sun Omary Mfaume amesema Shirika hilo
linafadhili wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kupitia programu za elimu
zinazojihusisha na ufadhili wa elimu na ile ya uhamasishaji jamii ambayo
inayowafundisha kwanini mtu anazaliwa na ualbino, changamoto zake na
namna ya kuzikabili changamoto hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi
wenzake Clara Maliwa ameiomba Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatambua
Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wanaofanya vizuri katika masomo ili
kutoa changamoto kwa wengine ili waweze kufanya vizuri zaidi.
0 comments:
Post a Comment