
**********
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema kaya zinazoishi kwenye makazi bora zimeongezeka kwa asilimia 16
katika kipindi cha miaka sita ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka
2011/2012.
“Kaya zinazoishi kwenye nyumba
zenye paa la kisasa zilizoezekwa kwa bati zimeongezeka kutoka asilimia
68 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2017/2018 wakati kuta
za kudumu zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2011/2012 hadi kufikia
asilimia 79 mwaka 2017/2018,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni
(Jumamosi, Juni 29, 2019) wakati akizungumza na viongozi na wananchi
mara baada ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu lililoko
Makulu, Manispaa ya Jiji la Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye
alimwakilisha Dkt. John Pombe Magufuli, pia alizindua ripoti ya matokeo
ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi
Tanzania Bara ya mwaka 2017/18.
Waziri Mkuu alisema takwimu
hizo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na
zinaonyesha jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kujenga Tanzania ya
Viwanda zinaendelea kuwanufaisha wananchi kwa zinagusa moja kwa moja
katika sekta ya ujenzi kama vile viwanda vya saruji, mabati, nondo, na
vinginevyo.
Waziri Mkuu alisema lengo la
Serikali ni kuona kila Mtanzania anaishi kwenye makazi bora kwani makazi
bora huimarisha afya za wakazi na afya bora ni mtaji wa msingi kwa kila
mwanadamu kwa kufanya kazi na hivyo kukuza uchumi.
“Tuendelee kuunga mkono jitihada
za Serikali kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje waje wawekeze kwenye
viwanda vya saruji, mabati, na marumaru ili kuongeza uzalishaji na
kuleta ushindani wa bei ambao utawanufaisha watu wengi na kuwapatia
fursa za kujenga makazi bora ya kuishi,” alisema.
Waziri Mkuu alisema mbali na
makazi bora, utafiti huo umebainisha uwepo wa ongezeko la kaya
zilizounganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa kutoka asilimia 18 mwaka
2011/2012 hadi kufikia asilimia 29.1 mwaka 2017/2018. “Jitihada za
Serikali chini ya Mpango wa Umeme Vijijini (REA), zinaendelea na
utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati
vijijini unaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya
Tanzania Bara ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ulioanza
mwaka wa fedha 2016/17 na unategemewa kukamilika mwaka 2020/2021,”
alisema.
Akizungumzia hali ya umaskini
barani Afrika, Waziri Mkuu alisema kiwango cha umaskini wa kipato cha
Watanzania hakitofautiani sana na nchi nyingine ndani ya bara hilo.
“Tukiangalia hali ya umaskini katika nchi nyingine za Bara la Afrika kwa
miaka ya hivi karibuni, nikianza na Kenya kiwango cha umaskini wa
mahitaji ya msingi ni asilimia 36.8 (mwaka 2015), Afrika ya Kusini
asilimia 55.5 (mwaka 2015), Rwanda asilimia 38.2 (mwaka 2016), Zambia
asilimia 54.4 (mwaka 2015), Ethiopia asilimia 23.5 (mwaka 2015) na
Zimbabwe asilimia 72.3,” alisema.
Alisema kupunguza umaskini kwa
nchi yoyote ile kunapaswa kuhusishwa na uwekezaji kwenye sekta nyingine
za kiuchumi ambazo hugusa na kuwanufaisha wananchi walio wengi.
“Nitumie fursa hii kusisitiza kuwa umaskini ni changamoto kwa dunia
nzima na hasa kwa nchi zinazoendelea. Nchi zilizo na hali mbaya zaidi ni
zile zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara kama takwimu rasmi
zinavyoonesha.”
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema ni lazima Serikali iimarishe upatikanaji wa takwimu kwa
kuajiri maafisa takwimu wanaowajibika moja kwa moja na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu badala ya kumtegemea mtu anayewajibika kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri.
“Leo hii hatuna Afisa Takwimu
katika kila Halmashauri, na matokeo yake hatuna mfumo mzuri wa kupata
taarifa kuanzia ngazi ya chini. Tuweke utaratibu ili hawa watu wawepo na
kila Afisa takwimu awajibike kupeleka taarifa yake kwa Mtakwimu Mkuu
kila wakati.”
“Nilipokuwa Naibu Waziri
TAMISEMI ninayeshughulikia elimu, nikiagiza takwimu fulani, kuzipata
ilikuwa inachukua zaidi ya wiki mbili, na hiyo ni kwa Halmshauri moja
tu. Na wakati mwingine, taarifa inakujia wakati umeshasahau kuwa ulitoa
agizo uletewe.”
Mapema, akitoa taarifa juu ya
utafiti huo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema
Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo kiwango cha umaskini
kimeendelea kushuka na kufikia tarakimu moja.
Alisema utafiti huo uliofanywa
na ofisi yake kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, baadhi ya balozi na
mashirika ya Umoja wa Mataifa ulilenga kupata makadirio ya viwango vya
umaskini ili kufuatilia, kupima na kutathmini mipango mbalimbali ya
kitaifa, kikanda na kimataifa.
Alisema katika utafiti huo, walitumia teknolojia ya kisasa iitwayo survey solution
ambayo imesaidia kupunguza gharama za utafiti za kupeleka madodoso na
magari. “Tulitumia vishkwambi (tablets) na kupunguza mzigo wa kubeba na
makaratasi au kukaa kujumlisha taarifa,” alisema,
0 comments:
Post a Comment