Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof.
Costa Ricky Mahalu akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo
jijini Mwanza kuhusu uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 kuelekea miaka
25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT)
utakaofanyika Julai, 2 mwaka huu jijini Mwanza ambapo Mgeni Rasmi
anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin. Kulia ni
Mratibu wa Kamati ya Habari-Maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya miaka
20/25 ya chuo cha SAUT Padre Titus Ngapemba na Rais wa Serikali ya
wanachuo Elian Rodrick (kushoto).
………………
Na Eleuteri Mangi- SAUT
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa anatarajiwa kuwa
Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 kuelekea miaka 25
tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT).
Kwa mujibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo
hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu amesema kuwa chuo kimemualika Rais
Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kwa kutambua na kuthamini
mchango wake katika elimu ya juu ambapo uzinduzi wa maadhimisho hayo
unatarajiwa kufanyika chuoni hapo Julai, 2 mwaka huu jijini Mwanza.
Akiongea na waandishi wa habari leo
chuoni hapo makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Mahalu amesema
kuwa yapo mafanikio mengi ambayo chuo kinajivunia tangu kuanzishwa kwake
mwaka 1998. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka udahili
wa wanafunzi kutoka wanafunzi 204 hadi wanafunzi 11400 kwa mwaka wa
masomo 2018/2019 licha ya kwamba katika mwaka wa masomo 2012/2013
udahili uliwahi kufikia wanafunzi 13121 kabla ya kuongezeka kwa matawi
13 ya chuo hicho.
“Katika mtaala wa chuo, wanafunzi
wanapata fursa ya kusoma masomo ya ujasiriamali na kujiajiri baada ya
kuhitimu masomo yao na hivyo kuondokana na dhana ya kungoja kuajiriwa.
Chuo kimeboresha kiwango cha elimu inayotolewa kuhakikisha wahitimu
wanahimili soko la ushindani Afrika Mashariki na duniani kote pia
kutokana na elimu ya dini na maadili kwa wanafunzi wote.” Amesema Balozi
Prof. Mahalu
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali,
Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa chuo kimefanikiwa kuanzisha kituo cha
kuzalisha na kuwawezesha wajasiriamali ambapo wanafunzi wanaohitimu
masomo yao wanapata fursa ya kuandika mawazo ya biashara na baada ya
mawazo yao kukubalika hupatiwa mafunzo maalumu juu ya mawazo hayo na
kisha wanapatiwa mtaji kati ya shilingi milioni 25 hadi 30 kwa ajili ya
kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.
Aidha, chuo hicho kimefanikiwa kuongeza
vitivo vingine vinne (4) kutoka kitivo kimoja ambacho kilikuwa cha
Sayansi ya Jamii na Mawasiliano kilichokuwa na shahada moja ya
Mawasiliano ya Umma na kuongezeka kwa Kitivo cha Biashara na Utawala,
Kitivo cha Ualimu, Kitivo cha Sheria na Kitivo cha Uhandisi.
Zaidi ya hayo Balozi Prof. Mahalu amesema
chuo cha SAUT kina mchango mkubwa katika kutoa wanataaluma na wataalam
katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wahadhiri, Wanahabari,
Wanasheria, Wasimamizi katika taasisi za Fedha na Wakaguzi wa Fedha,
Walimu, Wahandisi, Wafanyabiashara, Watunza amani katika majeshi ya
Ulinzi na Usalama pamoja na Wanasiasa. Miongoni mwa wahitimu hao ni Mhe.
Dotto Biteko Waziri wa Madini, Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan
Abbasi, Zawadi Machibya na Sammy Awami ambao ni watangazaji wa BBC,
pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi.
Chuo cha SAUT nje ya taaluma pia kinatoa
huduma kwa jamii ambapo kimefanikiwa kuanzisha mradi mkuwa wa umeme wa
kutumia nishati ya jua kwa kushirikiana na nchi ya Ujerumani ambapo
mradi huo unatekelezwa katika vijiji mbalimbali katika mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Kagera na Geita.
Naye Mratibu wa Kamati ya
Habari-Maandalizi ya kuelekea miaka 20/25 ya chuo cha SAUT Padre Titus
Ngapemba amesema kuwa Rais Mtaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu
katika sekta ya Elimu nchini katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Padre Ngapemba amesema kuwa Rais mstaafu
Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu katika sekta ya elimu nchini na kwa
namna ya pekee katika chuo cha SAUT, akiwa madarakani alifanikisha
ujenzi wa barabara ya kutoka jijini Mwanza kuingia chuoni hapo ambapo
ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ulianza mwaka 2002 na
kuzinduliwa mwaka 2004.”
“Mzee Mkapa anakumbukwa sana kwa kuwa
mwasisi wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa vyuo vyote
vya umma na binafsi. Uamuzi huu wa Mzee Mkapa wa kuwapatia mikopo
wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi umesaidia Watanzania wengi kusoma elimu
ya juu. Kwa hili utakumbukwa Mzee Mkapa” alisisitiza Padre Ngapemba.
Padre Ngapemba aliendelea kusema “Kwa
mara ya kwanza mwaka 2005 Serikali ya Awamu ya Tatu ilibadilisha Sera ya
mikopo ya elimu ya juu na kuanza kutoa mikopo kwa vyuo vikuu binafsi
ikiwemo SAUT baada Makamu wa Mkuu wa chuo wa wakati huo Padre
Deogratius Rweyengeza kutoa ombi hilo wakati wa mahafali ya kwanza mwaka
2001 tangu kipandishwe hadhi.”
Chuo Kikuu cha SAUT kinamilikiwa na
kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa kwa mujibu
wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu Tanzania
(TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka 2005
ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa
katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa
chini ya Askofu Mkuu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu la Mwanza.
0 comments:
Post a Comment